Pilipili hoho hupunguza gesi, huimarisha kinga

Friday January 18 2019

 

Wengi tunafahamu kuwa pilipili hoho ni kiungo cha mboga katika mapishi mbalimbali, pia hutumika kwenye saladi.

Lakini hatufahamu kama ni miongoni mwa mboga yenye vitamin nyingi, achilia mbali uwezo wa kuboresha mifumo mbalimbali ya mwili.

Neema Joshua ambaye ni mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), anasema pilipili hoho zina vitamini A nyingi.

Mtaalamu huyo anasema pilipili hoho rangi ya njano ndiyo mboga pekee yenye zeaxanthin kwa wingi kuliko mboga yoyote ikifuatiwa na mahindi inayoshika nafasi ya pili.

Kwa wale wanaosumbuliwa na gesi tumboni, wanashauriwa kutengeneza juisi ya pilipili hoho wakichanganya na juisi ya spinachi.

Pia, inaongeza kinga ya mwili pamoja na kupambana na magonjwa ya saratani na moyo pamoja na kuboresha uwezo wa macho kuona vizuri.

Pilipili hoho zina rangi tofauti ambazo ni nyekundu, kijani, urujuani na njano na zinatajwa kuwa mboga yenye vitamin zaidi ya 30.

Miongoni mwa faida zilizopo katika hoho ni kutibu muwasho wa koo na vidonda vilivyopo kooni.

Pia, hutibu watu wanaotoka damu puani na huimarisha kinga ya mwili kutokana na wingi wa vitamin C iliyopo ndani ya kiungo hicho ambacho hupigana dhidi ya magonjwa na kujenga kinga imara.

Makala haya yameandikwa na mwandishi wa gazeti hili, Hadija Jumanne.