UCHAMBUZI: Polisi, Sumatra mko wapi vurugu za bajaji Mbeya?

Sina shaka wengi wanaamini kwamba makao makuu ya wilaya, mikoa au nchi inabeba uhalisia wa tabia za waliopo katika eneo husika.

Kwa imani hiyo, pia ni ukweli kwamba kama makao makuu ya mkoa yatakuwa na uchafu mwingi ni wazi hali itakuwa mbaya zaidi kwenye wilaya, tarafa hadi vijijini.

Hali kadhalika kama mitaa ya makao makuu ya mikoa itakosa barabara nzuri au maji safi itakuwa dalili za wazi kwamba huko wilayani hakushikiki.

Kwa hali hiyo, miji mikuu ya mikoa iliyopo mipakani mwa nchi kama vile Musoma, Arusha, Moshi, Kigoma, Sumbawanga, Vwawa na Mbeya inayo kazi ya ziada ya kuhakikisha inajenga heshima kwa usafi wa mazingira yakiwamo majengo na ubora wa huduma za usafiri wa ndani ili wageni kutoka mikoa mingine au nchi jirani waone tofauti kati ya miji midogo na mikubwa.

Kwa mfano, Mkoa wa Mbeya unalo jiji ambalo ni kama linawakilisha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Kwa kuzingatia ukweli kwamba Mbeya ni jiji pekee kati ya miji saba ya mikoa ya kanda hiyo, ipo haja wananchi na viongozi wake kujitambua.

Viongozi wa Mkoa wa Mbeya hawana budi kuliangalia jiji la Mbeya kwa jicho la pili, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha linaboresha miundombinu yake na kutoa huduma nzuri tofauti na miji mingine ya mikoa.

Miongoni mwa huduma zinazotakiwa kuboreshwa kwa kiwango kikubwa ni usafirishaji wa abiria kwa kutumia pikipiki za miguu mitatu maarufu kama bajaji kutoka mitaa mbalimbali hadi Kabwe au Uhindini.

Jiji limejaa pikipiki hizi katika mitaa mingi na kuonekana kana kwamba usafiri ni mwingi, lakini ukweli usafiri huo unafanyika kienyeji kuliko inavyofikiriwa.

Miongoni mwa barabara zenye bajaji nyingi ni za kutoka Ituha hadi Kabwe, Isanga mpaka Kabwe, Isyenye Veta hadi Kabwe, Mwanjelwa kwenda Iyunga, Isanga hadi Uhindini, Sinde hadi Meta huku zingine zikitoka Mwanjelwa mpaka Uwanja wa ndege wa zamani.

Kwa kawaida uwezo wa babaji ni kubeba abiria watatu na dereva wa nne, lakini katika Jiji la Mbeya ambalo ni kioo cha Nyanda za juu bajaji zinabeba watu sita hadi 10.

Lakini kwa wanafunzi ndani ya bajaji hizo wanapakatana wawili wawili hadi zadi ya 10 huku wengine wakining’inia.

Yote hayo yanafanyika huku askari wa usalama barabarani wakiangalia kana kwamba ni kawaida. Hali kadhalika, maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) wapo jijini hapa wakishuhudia.

Polisi na Sumatra lazima waimarishe heshima ya jiji na kusimamia sheria za usalama barabarani kwa haki.

Sina uhakika kama wameacha hivyo wakimsubiri nani. Sitaki kuamini kwamba hata hili ni ni mpaka Rais John Magufuli aje akemee.

Kwa kweli usafiri wa bajaji jijini Mbeya ni wa ovyo na unaumiza wengi. Ukitaka kujua ajali za bajaji nenda kwenye gereji zake au tembelea hospitali kuomba taarifa za majeruhi wa kila siku.

Ni wazi vitendo vya bajaji kubeba abiria hadi 10 huku wengine wakibembea kwenye barabara kuu ya lami ni aibu na fedheha kwa viongozi wa Mkoa wa Mbeya.

Hivyo, nawasihi viongozi wa Mkoa wa Mbeya kuanzia wale wa Sumatra, kamanda Polisi mkoa na wale wa usalama barabarani waende mikoa ya Rukwa au Njombe wakajifunze ni vipi wenzao walifanikiwa bajaji za huko zinabeba abiria watatu tu bila shuruti.

Sumatra na Polisi Mbeya ni lazima wakumbuke kwamba wanavyoacha usafiri uwe wa ajabuajabu au ovyo ndivyo wanavyojenga picha mbaya kwa wageni kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Sumatra wanayo nafasi ya kusimamia taratibu zikiwamo za kuhakikisha bajaji zinapangiwa njia halali na kuendesha shughuli mwa mujibu wa sheria zilizopo za usafiri wa abiria.

Nimeutolea mfano Mkoa wa Mbeya na jiji lake, lakini ukweli ni kwamba usafiri huu umeshaenea karibu kila kona ya nchi yetu.

Kinachofanyika Mbeya kipo pia katika maeneo mbalimbali. Nitoe wito kuwa katu tusiruhusu uzembe tulioufanya kwa waendesha bodaboda ambao tuliwaachia wakawa na himaya yao badala ya kufuata sheria ukijatokeza katika usafiri huu.

Wahenga walisema samaki mkunje angali mbichi. Chondechonde viongozi wa Mbeya fanyieni kazi tatizo hili kabla halijaleta madhara au mnasubiri kupokea maagizo?

Lauden Mwambona ni mdau wa maendeleo anayeishia mkoani Mbeya