MAONI: Polisi wasifanye upendeleo wala uonevu katika mikutano ya kisiasa

Tuesday January 21 2020

Jeshi la Polisi wilayani Kigoma hivi karibuni lilizuia mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kwa madai ya sababu za kiusalama.

Mkutano huo wa Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, ulipangwa kufanyika Ijumaa iliyopita katika Viwanja vya Mwanga Center, Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Kwa mujibu wa barua ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kigoma, Raphael Mayunga kwa ofisi ya mbunge huyo, Jeshi la Polisi lilizuia mkutano huo kwa sababu za kiusalama kutokana na taarifa za kiintelijensia lakini jambo hili lilitokea wakati ambao Katibu Mlkuu wa CCM. Dk Bashiru Ally alikuwa na ziara ya kikazi mkoani humo.

Katika ziara yake, Dk Bashiru amekuwa akikutana na wanachama, viongozi wa CCM na serikali bila ya kizuizi chochote.

Hii si mara ya kwanza kwa jeshi la polisi kuzuia mikutano ya viongozi vyama vya upinzani huku wale wa chama tawala wakiwa hawapati matatizo na vyombo vya dola.

Inafahamika tangu Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani mwaka 2015 ilitoa mwelekeo wake kuhusu suala la mikutano ya hadhara na maandamano.

Advertisement

Pamoja na kuwa mikutano ya vyama vya siasa inaruhusiwa kikatiba lakini serikali ilitoa mwongozo kuhusu namna wanavyotaka mikutano hiyo ifanyike katika awamu hii.

Kila chama cha siasa kina haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Wajibu wa viongozi wa vyama vya siasa ni kutoa taarifa polisi pale wanapotaka kufanya mkutano wa hadhara au maandamano.

Rais Magufuli ametaka watu wajikite zaidi katika kufanya kazi na akaelekeza viongozi waliochaguliwa na wananchi ndio wanaoweza kufanya mikutano ya hadhara.

Ina maana kuwa wabunge na madiwani, waliochaguliwa na wananchi ndio wana ruhusa ya kufanya mikutano ya kisiasa.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza jeshi hilo la polisi mara nyingi limekuwa likilalamikiwa kwa kuvizuia vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara.

Mara nyingi kumekuwa na malalamiko ya wawakilishi kupitia vyama hivyo kudai kunyimwa nafasi ya kufanya mikutano ya hadhara pamoja na kuwa ni wawakilishi halali wa wananchi.

Kinachojitokeza ni kinyume cha agizo la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali, Simon Sirro aliyepiga marufuku jeshi hilo kujiingiza katika masuala ya siasa.

Akizungumza na makamanda na viongozi waandamizi wa jeshi hilo, Septemba 24, mwaka jana, Sirro alisema moja ya mambo wanayolalamikiwa ni kujihusisha na siasa.

Tunaliomba Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria na bila ya upendeleo linapokuja suala zima la mikutano ya hadhara na maandamano.

Kubwa zaidi ni kufanya kazi bila upendeleo ikizingatiwa kuwa nchi inafuata mfumo unaoruhusu vyama vingi vya siasa.

Sasa iweje jeshi hilo kuendelea kuvizuia vyama vya upinzani kufanya siasa wakati navyo vina haki ya msingi katika siasa.

Moja ya sifa ya Tanzania duniani ni kuwepo amani na utulivu, Jeshi la Polisi linapaswa kuzingatia kuwa linawajibika kuwatumikia wananchi wote bila upendeleo katika suala zima la kuendesha siasa nchini.