Presha ya mechi ya Simba, Yanga inavyoathiri afya za mashabiki

Matukio ya watu kubebwa kwenye machela wakiwa hawajitambui wakati wakipelekwa kupatiwa huduma ya kwanza, ni ya kawaida wakati wa mechi baina ya Simba na Yanga.

Na watu hao si kwamba wanaonekana wakati timu yao inaporuhusu bao tu, bali hata pale inapofunga hali ni kama hiyo.

Hayo ni kati ya matukio yanayopamba mechi za watani hao wa jadi. Licha ya Yanga kuanzishwa mwaka 1935 na Simba kuanzishwa mwaka mmoja uliofuata, klabu hizo zimegawanya karibu Watanzania wote katika makundi mawili.

Matukio hayo pia, yalijitokeza mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, unaochukua takriban watu 60,000. Siku hiyo mashabiki walikaribia kuujaza uwanja.

Mara kadhaa, kulionekana machela iliyobebwa na watu wanne wa huduma ya kwanza ikielekea maeneo ya vyumba vya kubadilishia nguo, ambako kuna chumba cha huduma ya kwanza. Gari la wagonjwa husubiri nje iwapo hali ya shabiki au mchezaji itahitaji uangalizi mkubwa zaidi.

Mechi hiyo haikuwa na kosakosa nyingi za mabao na Meddie Kagere aliifungia Simba bao hilo zikiwa zimesalia dakika 19 mchezo kumalizika, lakini kabla na baada ya goli hilo kulikuwa na matukio ya watu kupoteza fahamu.

“Sababu kubwa ya matukio ya namna hiyo ni kuzidiwa kwa mwamko uliopitiliza ambao huwa ni huzuni kubwa au furaha iliyopitiliza,” anasema Juma Sufiani, mmoja wa madaktari wa muda mrefu wa michezo aliyewahi kuitumikia Yanga na timu ya Taifa.

“Utakuta mtu anatoka nyumbani kwake akiwa na matokeo yake kichwani na inapokuwa kinyume huwa ni tatizo kwake. Anaweza kuwa na furaha au huzuni iliyopitiliza.”

Mwingine anayetoa huduma ya kwanza kwenye uwanja huo, Evance Ebeneza anasema kuna sababu mbili za watu kupoteza fahamu uwanjani hapo.

“Kitu cha kwanza huwa ni kukata kwa mawasiliano kwa sababu ya kukosa hewa,” anasema alipoulizwa na Mwananchi kuhusu hali hiyo inayojitokeza katika mechi baina ya watani hao wa jadi tu, au wanapokuwa na mechi za kimataifa.

“Pili ni mshtuko wa jambo fulani la huzuni au furaha kubwa.”

Wanaweza kuepuka kuzimia

Lakini Dk Sufiani anasema mashabiki wanaweza kuepukana na hali hiyo iwapo watajiandaa kisaikolojia.

“Hakuna dawa ya kujizuia kwa sababu hutokea ghafla, labda kabla (ya kwenda uwanjani) awe amejiandaa kisaikolojia,” anasema.

“Kila mtu ana namna yake anavyoishi na namna anavyouchukulia mambo. Katika mchezo kuna watu wanazipenda timu hizo kwa hisia kubwa na ni wanachama.”

Anasema badala ya kujiaminisha kuwa timu yake itapata ushindi, shabiki anaweza kutuliza akili yake na kuwa tayari kwa matokeo yoyote.

“Kikubwa kama mtu anakwenda katika matukio ya aina hiyo ajitahidi kutuliza akili yake ili asikutane na hayo,” anasema Dk Sufiani.

Naye Dk Ebeneza anawashauri mashabiki wasiwe na mwamko uliopitiliza.

Hakuna anayefariki

Pamoja na mechi hizo za watani wa jadi kutawaliwa na matukio ya watu kupoteza fahamu, kwa wengi hali haifikii kuwa mbaya kiasi cha kupoteza maisha.

“Kwa hapa uwanjani tangu nianze kufanya kazi hajawahi kufa mtu isipokuwa wapo wanaozidiwa na huwa tunawapeleka hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi,” anasema Dk Sufiani.

Anasema mara nyingi wanaozidiwa huwapeleka Hospitali ya Temeke, lakini wengi huzinduka baada ya saa moja au mbili.

Hata hivyo, wakati wa mechi ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika baina ya Simba na Nkana Red Devild kwenye Uwanja wa Taifa, shabiki na mwanachama wa muda mrefu wa Simba, Rajab Kessy alipoteza maisha baada ya hali kumzidia akiwa uwanjani.

Kessy pia alikuwa dereva wa kocha wa timu ya Taifa na ambaye amewahi kuwa meneja wa Simba.

“Kessy alizidiwa uwanjani na hakufia hapo,” alisema Dk Sufiani.

“Kutokana na tatizo lake aliwahishwa hospitali lakini mwisho wa siku yalitokea hayo; alifariki dunia.”.

Naye Ebeneza anasema mtu anapozimia ni rahisi kupoteza maisha kwa kuwa “sehemu ya ubongo huwa inakata mawasiliano hivyo hakuna kazi yoyote inayofanyika. Asipopata matibabu kwa wakati ni rahisi kupoteza maisha”.

Aina ya matibabu

Alisema baadhi ya matibabu hayo yanayotakiwa mapema ni kumuangalia mapigo yake ya moyo yanafanya kazi na anavyopumua.

“Ukijiridhisha, kitu cha kwanza unalegezea vitu vyote ambavyo vinaweza kuwa vimebana mwili wake,” anasema Dk Sufiani.

“Utamvua viatu, mkanda, tai kama atakuwa amefunga, nguo zilizombana kisha unamlaza chali na unainua miguu yake juu ili damu iweze kwenda kwa wingi kichwani.

“Damu ikitembea kwa wingi kwenda kichwani na oksijeni nyingi itakwenda, hivyo itamsaidia mgonjwa huyo kurudi katika hali yake kwa uharaka.”

Anasema, kama hatakuwa anapumua kuna taratibu za haraka zinazochukuliwa ambazo ni upumuaji bandia na kumkanda kifuani (cardiac massage).

Lakini kujua matibabu hayo ni vizuri kuingia darasani.

“Hii ni kwa sababu kama upumuaji bandia (namna ya kumpumulisha hewa), kuna namna ya kufanya, ukaaji na mambo mengi. Inawezekana mtu akaelewa tofauti halafu isimsaidie na mashine iko hivyo pia,” anaeleza Dk Sufiani.

Idadi ya wanazozimia

Mechi ya juzi kulikuwa na watu sita waliozimia, lakini Dk Sufiani anasema wakati mwingine hufikia hadi 40.

“Kulingana na idadi ya wagonjwa kwa upande wetu huwa tunajiandaa. Upande wa madaktari tunaokuwa hapa uwanjani ni kati ya mmoja hadi 10, wasaidizi wetu wa First Aid (huduma ya kwanza) huwa kati ya 20 hadi 30, kulingana na ukubwa wa mchezo,” anasema.