UCHAMBUZI: Profesa Kezilahabi alivyoiacha fasihi ya Kiswahili katika upweke

Tuesday January 14 2020Amani Njoka

Amani Njoka 

By Amani Njoka

Si kazi rahisi kuizungumza fasihi ya Tanzania na Afrika bila ya kumtaja Profesa Ephrase Kezilahabi.

Huu ni mwamba ambao fasihi iliegemea na ikajishika ikawa imara. Elimu ya Tanzania haiwezi kuzikwepa kazi zake nguli katika uwanja wa Kiswahili hasa kwa ngazi ya vyuo.

Wanafunzi, wasomi na wanazuoni wa Kiswahili, hawatokuwa wageni wa Roza Mistika, Gamba la Nyoka, Nje Ndani, Dunia Uwanja wa Fujo na kazi nyingine nyingi.

Kezilahabi aliyetutoka hivi karibuni, alikuwa mshairi, mtafiti, mwandishi wa riwaya na tamthiliya za Kiswahili. Pia alikuwa mkufunzi katika shule na vyuo nchini Tanzania na sehemu nyingine za Afrika.

Ama kwa hakika ni vigumu kuitenganisha Fasihi ya Afrika na Kezilahabi. Akiwa muumini wa Falsafa ya Kiafrika, mwanamapinduzi na mtu aliyeamini katika usawa katika jamii.

Aliitumikia fasihi kwa muda mrefu katika siku za uhai wake. Kama mwana wa Afrika alisisitiza suala la haki na usawa, uwepo wa Mungu, kifo, furaha, ukweli na maisha kwa jumla.

Advertisement

Mapinduzi katika ushairi, hiki ni miongoni mwa vipindi muhimu sana katika fasihi ya Tanzania hasa ushairi. Alikuwa miongoni mwa wanamapinduzi waliopambania uandishi huru wa mashairi.

Wakati ushairi wa Kiswahili ukitawala na ukale mpaka miaka ya 1970, Kezilahabi na wenzake wakaamua kubadilisha taswira ya ushairi na kuwa huria. Katika kipindi hiki ndipo alipoandika diwani ya Kichomi (1974).

Kuanzia wakati huo Kezilahabi na wenzake waliamini kwamba ushairi ukifikisha ujumbe kwa jamii inatosha, hakuna haja ya kufuata kanuni na taratibu na kanuni za ushairi wa kimapokeo kama walivyofanya nguli wengine kina Shaaban Robert.

Kwa hakika mapinduzi haya ambayo ni juhudi zake na wenzake, ndiyo mwanzo wa kuibuka kwa waandishi wengi wa kisasa ambao pengine awali walipata wakati mgumu wa kuchipuka katika ushairi kutokana na kukabiliwa na upinzani wa wanamapokeo.

Huenda ndiyo chanzo cha mashairi mengi ya leo zikiwamo nyimbo za Bongo Fleva.

Chanzo cha utafiti na uchunguzi wa kazi mbalimbali za kifasihi, inawezekana kuwa kabla ya Profesa Kezilahabi kujikita katika uandishi wa riwaya, watafiti, wanafunzi, wakufunzi na wahakiki hawakupata wakati mgumu sana katika kuzichambua na kuzielezea kazi mbalimbali za kifasihi hasa riwaya na tamthilia.

Hata hivyo, kazi ya usomaji, utafiti na uhakiki iligeuka kuwa ngumu zaidi pale ambapo riwaya kama Nagona (1990) na Mzingile (1991) zilipochapishwa.

Kezilahabi amekuwa gumzo katika shule na vyuo mbalimbali hasa pale msomaji wa vitabu anapokutana na vitabu vyake. Vitabu hivi vimejaa sanaa ya hali ya juu, jazanda, picha na taswira zilizotumika huwafanya wasomaji kuumiza vichwa kuliko kawaida na ndipo watafiti na wahakiki hujikita katika kutafuta maana ya vitabu hivyo.

Mathalani, kitabu cha Nagona huacha maswali mengi kwa wanafunzi na wakati mwingine kuwachanganya hata walimu. Katika kitabu hicho kuna wahusika Paa, Nabii, Jogoo, Aristotle na wenzake.

Msomaji anaposoma kilichoandikwa hujaribu kuwafikiria wahusika hawa kwa namna mbalimbali, lakini asilipate jibu la moja kwa moja.

Kazi yake ya uandishi ilikuwa moja ya viwanda bora vya kuzalisha nyenzo za maarifa miongoni mwa wasomi lukuki katika taifa la Tanzania na Afrika.

Vitabu vyake vya riwaya, tamthilia na ushairi vimekuwa nguzo muhimu katika taaluma ya Kiswahili hasa fasihi. Wanafunzi, watafiti na wahakiki huchota ukwasi wa maarifa yaliyo katika vitabu hivyo na kisha kuwasaidia katika maisha ya kila siku na hata masomo yao kwani hutumika kama marejeleo.

Baadhi ya kazi kama Roza Mistika (1971), Kichwa Maji (1974), Dunia Uwanja wa Fujo (1975), Gamba la Nyoka (1979), Nagona (1990) na Mzingile (1991) ni miongoni mwa kazi bora za mikono na kalamu ya Kezilahabi.

Licha ya mchango wa vitabu vyake katika elimu, Profesa Kezilahabi alikuwa mwalimu. Wasifu wake unaonyesha shule kadhaa na vyuo alivyofundisha ambapo kupitia yeye kama mwalimu na mkufunzi wataalamu wamepitia.

Huwezi kusita kumtaja Kezilahabi kama baba na mlezi wa wataalamu wengi kitaaluma. Ikumbukwe kuwa Kezilahabi alikuwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Botswana katika siku za mwisho wa uhai wake.

Hakika fasihi na taaluma ya Kiswahili imebaki na upweke, Kuna uwezekano wa kuchukua miaka kadhaa kuja kumpata Kezilahabi mwingine.

Haijulikani kama fasihi itaweza kuishi na kivuli cha Profesa Kezilahabi kupitia kazi zake. Daima ataishi na kukumbukwa kwa mchango wake katika taaluma ya fasihi ya Kiswahili.

Kazi zake zitasomwa vizazi na vizazi na kukumbukwa kama ambavyo tunamkumbuka mwamba na jabali la fasihi, Hayati Shaaban Robert.

Amani Njoka ni mdau wa lugha ya Kiswahili: 0672395558