Raha ya muziki uwe ‘laivu’

Muktasari:

  • Watu wenye asili ya Kusini tunaoishi Dar es Salaam kwa pamoja na jamii ya marasta wa Tanzania tukafanya mkutano wa dharura ili kupata muafaka wa nini kifanyike ili kuwanusuru ndugu zetu. Tukaona njia pekee ni kuchangia. Lakini kwa jinsi hali ya uchumi ilivyokuwa, ilitulazimu kuwashawishi Watanzania watuchangie.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990 kulitokea janga la mafuriko katika mikoa ya Kusini. Nyumba nyingi zilisombwa na kusababisha wakazi kukosa makazi. Kutokana na uharibifu mkubwa wa miundombinu, shughuli muhimu za kila siku zilisimama.

Kulikuwa ukosefu wa chakula, mavazi na malazi. Serikali kwa upande wake ilijitahidi kurekebisha miundombinu ili misaada iwafikie walengwa, lakini kwa wakati ule ilikuwa sawa na kumpa miwani mtu asiye na macho. Hali ya barabara kwa enzi zile ilikuwa mbaya, hivyo mafuriko yakachangia kuharibu kabisa.

Watu wenye asili ya Kusini tunaoishi Dar es Salaam kwa pamoja na jamii ya marasta wa Tanzania tukafanya mkutano wa dharura ili kupata muafaka wa nini kifanyike ili kuwanusuru ndugu zetu. Tukaona njia pekee ni kuchangia. Lakini kwa jinsi hali ya uchumi ilivyokuwa, ilitulazimu kuwashawishi Watanzania watuchangie.

Tungewashawishi kwa njia ipi? Kwa bahati njema wengi wa wenye asili ya Kusini mwa Tanzania ni wasanii. Na bahati njema nyingine ni kwamba wengi wa marasta ni wasanii pia, wanamuziki, wachoraji, wachongaji na wabunifu mitindo. Tukawaalika wasanii wenzetu waliofanya vizuri kwenye tasnia na kuomba mawazo yao.

Kama utakumbuka vyema wakati huo ulikuwa wakati wa mapinduzi ya muziki. Dansi na disko vilikuwa vikigombania usukani, lakini muziki wa kizazi kipya ulikuwa umewasha indiketa ya kuomba njia. Wenyewe ulichukua tabia za disko na dansi kwa pamoja, kwa hiyo ulishaanza kukubalika kwa kiasi kikubwa.

Basi tukatoka na wazo kuwa tuunganishe aina zile za muziki zilizokuwa zikichuana sokoni, tufanye tamasha la bure la muziki na kuomba wahudhuriaji watusaidie kwa uwezo wao. Kile ambacho kingepatikana tungekikabidhi kwa viongozi.

Nakumbuka vizuri siku hiyo tulikutana kwenye ukumbi wa YMCA. Tukafuata taratibu zote za Serikali na kupata baraka za mkuu wa mkoa. Tukapata kibali cha kutumia bustani ya Mnazi Mmoja. Serikali ikakubali mwaliko ambapo mkuu wa mkoa angekuwa mgeni rasmi.

Basi jioni ya siku mahsusi tulifunga muziki wa kufa mtu pale bustanini. Muziki wa aina tatu ulikutana kwenye jukwaa moja. Bendi karibu zote maarufu ziliitikia wito, likawa tukio la kitaifa hasa.

Mzee Kassim Mapili aliongoza muziki wa bendi, Kwanza Unit wakaongoza wa kizazi kipya na Old Skool DJs wakisugua LPs kuubeba muziki wa disko. Ukweli palichimbika sio kidogo.

Tukio moja la bahati mbaya lilitokea, lakini lilinifurahisha kupita kiasi. Wakati bendi ya Tatu Nane ikiwa ndiyo kwanza inatupandisha mizuka ya Kipogoro, kulitokea hitilafu ya umeme na muziki ukazima. Sote tulichanganyikiwa. Mtu mmoja alimkosa kibao msichana aliyekuwa akicheza naye. Kuna mama mwingine alidondoka, wakasema ana mizimu. Taharuki ilikuwa kubwa.

Wakati huo hakukuwa na mgawo wa umeme, hivyo hatukujiandaa na jenereta. Tukavuka barabara ya Lumumba kwenda kuangalia maunganisho ya umeme tuliouchukulia kwenye jengo la Ushirika.

Kabla hatujafika tukasikia Sangura likiendelea. Tukadhani tatizo la umeme limekwisha. Lakini nikaisikia sauti ya kiongozi wa Tatu Nane, Manju Msitaaikitamba: “Uwake usiwake hapa ni muziki tu…” Kumbe kweli, walipiga muziki bila umeme! Lilikuwa somo kubwa katika maisha yangu. Hata jogoo akisusa kuwika kutakucha tu.

Hii ilikuwa ‘live music’. Kundi la watu saba lilikuwa likitawala jukwaa kama lilivyotaka. Nawakumbuka “Babu” Manju, Dulla, Naliene, Mahdi Tumbo, Seif Rengwe, Teddy na Charles Muhuto. Kila mmoja wao alikamata zana asilia na muziki ukawa na msisimko zaidi.

Siku hiyo isiyosahaulika kichwani kwangu ikaisha kwa mafanikio makubwa. Tulikusanya kiasi kikubwa, tukakiwakilisha kwa mkuu wa mkoa na ujumbe ukapelekwa kwenda kuwasilisha huko Lindi na Mtwara.

Tofauti kubwa ninayoiona kwenye miaka hii ni wasanii wetu kuogopa ala za muziki. Wengi wamejiwekea mipaka na kuishia kwenye muziki wa kompyuta. Si kwamba wanaogopa kujifunza matumizi ya ala tu, bali wanaziogopa hata ala zenyewe.

Historia ya muziki inaonyesha wazi kuwa muziki unaotengenezwa moja kwa moja studio haudumu. Linganisha muziki wa ‘laivu’ kama “Jazz” na muziki wa studio kama “House” kule Marekani. House ulipotea baada ya kitambo kifupi sana.

Kisha angalia umri wa muziki wa kizazi kipya unaoitwa “wa zamani” hapa nyumbani. Utagundua kuwa muziki huu unachoka katika kipindi kifupi sana.

Kote duniani wanamuziki huimba kwa ajili ya kutoa ujumbe, kutumbuiza na kuonyesha uwezo jukwaani. Pia hurekodi kwa ajili ya kuuza na kutunza kumbukumbu.

La ajabu hapa kwetu kila wanapotumbuiza, wasanii hucheza CD na kupiga kelele za “mikono juu…” wakiacha CD ifanye kile walichotakiwa kufanya. Hiyo ndiyo wenyewe huita “laivu”.

Siwashushi thamani, bali ninaona kuwa wangepata heshima na tuzo kubwa duniani iwapo wangepiga laivu. Si lazima wao wenyewe kushika ala, lakini wangeweza kuwaalika wapiga ala na kufanya mazoezi nao kabla ya kupiga kwenye maonyesho. Kwenye tamasha au tuzo inabidi muziki kupigwa laivu.