MAONI: Sababu za kuzuia mikutano ziwe wazi, haki

Gazeti hili toleo la juna Februari 22 lilikuwa na habari kwamba sababu za kiintelijensia zinazotolewa kila mara na polisi kuzuia mikutano ya vyama vya siasa, hasa vya upinzani zinazua maswali.

Bila shaka maswali yaliyoibuliwa na habari hiyo yanahitaji majibu yanayojitosheleza kutoka katika mamlaka husika, ili kuondoa sintofahamu na hivyo kuwezesha haki kutendeka na ikaonekana inatendeka.

Pamoja na majibu ya msemaji wa Polisi, David Misime kwamba mikusanyiko, maandamano au mikutano ya hadhara inatakiwa kufuata taratibu za kisheria.

Pia kwamba wasimamizi wa sheria wamepewa maelekezo ya kisheria na taratibu za kufuata wakati wote wa kusimamia mikusanyiko hiyo na si kufuata hisia za mtu au watu, majibu hayo hayawezi kutosheleza kueleza kile kinachofanyika wala kufafanua kinachotakiwa kufanyika.

Jeshi la polisi linatakiwa kueleza linapopata taarifa za kiintelijensia kuwa kuna viashiria vya uvunjifu wa amani, huwa linafanya nini kuongeza ulinzi katika eneo husika badala ya kuzuia mkutano.

Pia, linatakiwa kueleza kwamba baada ya kupata viashiria hivyo limefanya uchunguzi na watu wangapi wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kutaka kuhatarisha amani.

Si hayo tu, jeshi la polisi litakiwa kujibu hata malalamiko ya wanasiasa yaliyopo, kwamba inakuwaje viashiria vya uvunjifu wa amani vinajitokeza kwa upande wa mikutano ya upinzani, na si upande wa pili wa chama tawala.

Je, linafanya kitu gani ili hali hiyo isitokee katika mikutano ya chama tawala na ikiwa kuna jambo lolote linalosaidia hali isitokee huko, kwa nini jeshi hilo lisifanye hivyohivyo kwa wapinzani ili kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya mikutano yao kwa amani na usawa kama Katiba inavyoelekeza.

Tunazungumza masuala hayo sasa kutokana na matukio yanayoendelea sasa na miaka ya karibuni ya polisi kuzuia mikutano mingi ya upinzani kwa kinachoelezwa ni ‘taarifa za kiintelijensia zinazoonyesha viashiria vya uvunjifu wa amani.”

Kama ambavyo imekuwa inajitokeza, polisi juzi walizuia mkutano wa mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka kwa sababu hizohizo, wakiahidi mkutano huo kuruhusiwa pindi hali ya amani itakaporejea.

Ni kutokana na hali hiyo, wadau wa siasa wamekuwa wakieleza kuwa hali hiyo haiashirii haki katika usimamizi wa sheria.

Pamoja na mtazamo wa wadau hao, sisi tunadhani pia kuwa kazi ya polisi ni kutoa ulinzi wa kutosha ili kuhakikisha kila kitu kinafanyika kwa amani.

Hivyo kilichokuwa kinatakiwa ni polisi kuweka ulinzi ili kuhakikisha viashiria hivyo havigeuki kuwa halisi, la sivyo wananchi watazidi kupata hofu kuhusu hali ya usalama kutokana na taarifa za kila mara za “viashiria vya uvunjifu wa amani”.

Ni bahati mbaya hata agizo la Rais John Magufuli kwamba kila mbunge na diwani afanye mikutano katika eneo lake, polisi wameendelea kulikiuka kwa kuizuia.

Hii inafanya tujiulize, hivi kuna maagizo mengine ya ziada wanayopata?

Tungependa kuwashauri polisi wafuate sheria, Katiba na maelekezo halali katika utendaji wao wa kazi.

Ushauri muhimu kwao ni pamoja na uliowahi kutolewa na Jaji Mkuu wa zamani, Barnabas Samatta kwamba “polisi hawaruhusiwi kuzuia mikutano au maandamano kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.”

Kama alivyosema, Kamanda Misime “lengo la sheria ni kuhakikisha haki inatendeka na usalama wa nchi unazingatiwa bila kufuata matakwa ya watu,” basi hali hiyo izingatiwe bila upendeleo wowote.