UCHAMBUZI: Sauti kubwa kwenye ‘earphone’ si ujanja ni maradhi

Katika dunia hii yenye vifaa vingi vya kuzalisha sauti, kumbi za muziki na vifaa vya kusikiliza sauti, basi hapana shaka yapo madhara yake.

Hatuwezi kuacha kumshukuru Mungu kwa uvumbuzi wa teknolojia hizi, lakini hatuwezi pia kuacha kuchukua tahadhari tukiangalia yale madhara yanayoweza kujitokeza katika teknolojia hizo.

Moja ya vifaa vya kiteknolojia vinavyopatikana kwa bei nafuu na kwa urahisi ni ‘earphones’ yaani vifaa maalumu vya kusikilizia masikioni.

Katika ulimwengu huu wa sasa wa simu za kisasa, vifaa hivi hutolewa pamoja na simu hizo, hivyo kuufanya upatikanaji wake kuwa rahisi.

Hata hivyo, matumizi mabaya ya vifaa hivi, yanatajwa kusababisha uziwi au ulemavu wa kusikia.

Juni 20, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema asilimia tatu ya wanafunzi wana matatizo ya usikivu, asilimia 24 ya wanaogua magonjwa ya mfumo wa maisha wana tatizo hilo na asilimia 50 ya wanaofanya kazi kwenye machimbo au viwanda vya nguo nao wana tatizo la usikivu.

Akaongeza kuwa, miongoni mwa vyanzo vya maradhi ya usikivu ni matumizi mabaya ya ‘earphones’

Hivyo basi kama ambavyo wahenga wanasema, “Ni bora kuziba ufa, kuliko kujenga ukuta” ni muhimu kupeana tahadhari kuhusu matumizi ya vifaa hivi.

Ukiachilia mbali kauli ya Waziri Ummy lakini pia Shirika la Afya Duniani, (WHO) Februari 2015 lilitoa taarifa likieleza kuwa vijana 1.1 bilioni wapo hatarini kupata matatizo ya usikivu kutokana na matumizi yasiyo salama ya vifaa vya sauti.

WHO ilitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na simu za kisasa (pamoja na earphone zake) na sauti katika kumbi za burudani (baa, klabu, harusini).

Kwa mujibu wa WHO, ulemavu wa kusikia una madhara mengi ikiwamo kusababisha maradhi ya akili na kuharibu fursa za ajira na elimu.

Najua vijana wanapenda zaidi kusikiliza muziki wenye sauti kubwa na wakati mwingine vifaa hivi vinakupa nafasi ya kusikiliza muziki katika hali ya faragha kidogo. Ingawa ni starehe kwako lakini ndicho chanzo cha ulemavu wako.

Matumizi salama ya vifaa hivi yatasaidia Taifa letu kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika kufanya upasuaji.

Pia, kitaokoa nguvu kazi ya vijana ambao watatumika kuijenga nchi.

Inaelezwa kuwa maradhi ya usikivu yanaweza kusababisha hasara ya Dola za Marekani 750 billioni kwa mwaka kwa ajili ya matibabu.

Mkuu wa idara ya pua, koo na masikio wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Edwin Liyombo aliwahi kusema kuwa gharama ya kununua kifaa cha usikivu ni Sh31 millioni na matibabu yake ni Sh 6 milioni. Hivyo humgharimu mtu kiasi cha Sh37millioni kupata matibabu endapo masikio yake yataharibika.

Kuna gharama kubwa kumtibu mtu aliyepoteza uwezo wa kusikia, kwa mfano atahitaji hivyo vifaa vya usikivu, elimu ya lugha ya ishara na elimu nyingine ili kumsaidia.

Je, unadhani ni rahisi kufanya haya kuliko kuacha tabia hii hatarishi?

Utafiti mwingi wa kisayansi unaonyesha kuwa maradhi yasiyo ya kuambukiza ikiwamo kupoteza uwezo wa kusikia ndiyo yanayoshika kasi zaidi katika nchi zinazoendelea.

Inawezekana kabisa vijana wa sasa wanajitahidi kupambana na maradhi mengine ya kuambukiza kama Ukimwi, kipindupindu na mengine ya zinaa lakini wanajisahau katika mienendo yao ya kila siku.

Tabia zetu za kila siku, ikiwamo hayo matumizi mabaya ya vifaa vya sauti, ndicho chanzo cha maradhi ambayo mengine husababisha ulemavu wa kudumu.

Vijana ambao kimsingi ni asilimia 60 ya idadi ya watu duniani, hamna budi kujitathmini.

Kwanza ni vyema mkumbuke afya zenu ni mtaji wenu na mtaji wa taifa zima. Pili, ni muhimu kupunguza muda wa kutumia vifaa vya sauti.

Pili, kupunguza muda wa kukaa katika kumbi za starehe zenye sauti kubwa ya muziki.

Si ujanja bali ni ujinga, kufungulia sauti ya juu ya radio kwenye gari au nyumbani kwako, si ujanja bali ni ujinga na kujiletea madhara.

Tumia simu yako ya kisasa kwa akili; unaweza kupunguza kiwango cha sauti na bado ukafurahia muziki wako.

Haina maana kusikiliza muziki kwa kutumia ‘earphone’ zako lakini sauti tunaisikia sisi majirani tulioketi karibu na wewe.

Hatuhitaji sheria kulinda afya zetu wenyewe; cha muhimu ni kujilinda, kujithamini na kujipenda. Yaliyobaki ni ya Mungu.

Florence Majani anafanya kazi Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa). 0764438084