UCHAMBUZI: Sera ya viwanda ilete mapinduzi ya kilimo

Sera nzuri ya viwanda haina budi iende sambamba na mapinduzi ya kilimo. Kilimo cha jembe la mkono; mkulima anaweza kulima siyo zaidi ya hekta tatu.

Kilimo cha sasa cha jembe la mkono ni lazima kibadilike na kiwe cha kutumia plao na trekta. Vishamba vidogovidogo vilivyotawanyika nchi nzima haviwezeshi kutumia zana bora za kilimo.

Ili kufanikisha malengo ya kilimo cha kisasa, watunga sera lazima washirikishe wataalamu wa kilimo, uchumi, ushirika na wanasosiolojia ili kilimo kiwe cha kisasa na chenye tija zaidi.

Kila mkulima alime hekta kumi na kuendelea, ili matumizi ya trekta yawe na manufaa kwa mkulima na mwekezaji. Wataalamu wakishirikishwa katika kilimo watawezesha kuleta mageuzi makubwa ya kilimo. Mkulima hufanya shughuli nyingi za uzalishaji mali, kilimo na ufugaji.

Wakulima wakiwa katika ushirika wa hiari bila kulazimishwa na yeyote, wataweza kutumia zana bora za kilimo kwa manufaa zaidi.

Hali ya sasa ya michezo ya kubahatisha nchini pamoja na kufanya waliobahatika kupata pesa, kujenga nyumba bora, kupata bajaji, kilimo hakiwezi kuwa kipaumbele cha wateule hawa.

Michezo hii nailinganisha na ndoo iliyojaa maji iliyoko kilingoni na kwenye kitako ina tundu dogo na maji kuvuja tone moja moja na mwenye kubahatika tone kumdondokea basi anashukuru kwa kupata neema ya utajiri.

Wateule hawa ni matokeo ya kuchangiwa na mamilioni ya watu wenye kukaa na matumaini ya kutajirika na hawajui lini watafanikiwa na neema hii.

Mapinduzi ya kilimo hayawezi kufikiwa kwa mtazamo huu na uchumi wa kati mwaka 2025 ni shakani kufikiwa kama mageuzi ya kilimo hayapo.

Mageuzi haya ya kilimo yanaweza kuvutia wawekezaji wengi wenye kupenda kusaidia wajasiriamali wadogo wadogo. Benki ya Amana katika tangazo la kwenye runinga 19/11/2018 imeonyesha nia yake ya kuweza kutoa mikopo bila riba kwa wajasiriamali wadogo wadogo.

Hii ni dalili njema kufanikisha juhudi za Serikali katika mipango yake ya maendeleo kuboresha maisha ya wananchi. Ushirika wenye madhumuni mengi utaleta mapinduzi ya kilimo na kuwezesha kufikia uchumi wa kati mwaka 2025.

Uchumi wa kati maana yake wakulima waondokanae na kilimo cha kujikimu na kuingia katika kilimo cha biashara.

Hali hiyo itasababisha uzalishaji mali na mzunguko wa fedha kuongezeka vijijini na kutokomeza umaskini.

Pato la Taifa litakuwa kama mageuzi ya kilimo yatakuwapo, kilimo kisitegemee mvua tu, bali umwagiliaji pia, mbegu bora na zana bora za kilimo.

Wafugaji waelimishwe kuhusu ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhama hama na mifugo kutafutiwa malisho.

Wakulima kupitia vyama vya ushirika na bodi washirikishwe katika upangaji wa bei ya mazao yao. Bei nzuri itawapa motisha ya kukuza kilimo chao.

Vyama vya ushirika kuanzia ngazi ya chini, wilaya, mkoa hadi Taifa, vikiwa makini katika kazi vitasikika kwa watunga sheria ili kuleta mageuzi imara zaidi.

Ili kufanikisha ukuzaji wa kilimo hapa nchini, bodi ielekeze sera ya kutoa mikopo kwa wakulima kwa masharti nafuu hasa kwa vyama vya ushirika vya msingi vyenye madhumuni mengi.

Tangu nchi kupata uhuru, sera kuhusu vyama vya ushirika imekuwa ikibadilika kabla ya Azimio la Arusha mwaka 1967 na vijiji vya ujamaa.

Vyama vya ushirika vilikuwa vya kununua mazao, mikopo kutolewa kwa wakulima matajiri (wakubwa), na maskini kutopata mikopo (wakulima wadogo).

Hali ya sasa ya soko huria, vyama vya ushirika vimekosa nguvu ya kumudu ushindani katika biashara na matajiri. Kwa hiyo wakulima wakubwa hupata mikopo kutoka kwa taasisi za fedha kwa urahisi huku wakulima wadogo wakikosa kwa sababu hawana dhamana. Siku hizi kuna Saccos mbalimbali na nyingi zipo mijini na hazina lengo la kukuza kilimo. Hivyo, wakulima maskini si rahisi kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha.

Wakulima wadogo hawana uwezo wa kubuni na kuendesha biashara kwa faida, wanaogopa kukopa wasije kupoteza dhamana zao wakashindwa kurejesha mikopo hiyo.

Njia salama ya mikopo kwa wakulima wadogo ni ushirika. Ukomo wa madeni katika ushirika ni kinga ya mikopo. Wataalamu wa ushirika, kilimo ni rahisi kutoa elimu hiyo na kukuza ushirika. Kilimo cha kujikimu kibadilike na kuwa cha biashara.

Vyama hivi vya ushirika vyenye madhumini mengi ni lazima viwe na hati ya kumiliki ardhi na kujiunga na chama cha ushirika cha Taifa.

Hati ya kumiliki ardhi ni dhamana ya kupata mikopo. Uongozi imara wa kuendesha chama lazima uwepo. Wataalamu mbalimbali waajiriwe kuendesha chama hicho.

Mwandishi wa uchambuzi huu ni msomaji wa gazeti hili kutoka, Chanika Handeni; anapatikana kwa namba 0784 603 570