Serikali ijitahidi kuwapa motisha walimu

Friday February 9 2018

 

Hatimaye kilio cha muda mrefu cha walimu kutopandishwa madaraja kimesikika.

Juzi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Joseph Kakunda alisema Serikali imeshamaliza mchakato na mapitio ya upandishaji madaraja walimu uliokuwa umesimamishwa kwa muda mrefu.

Kakunda alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalumu (Chadema), Susan Lyimo aliyetaka kujua hatima ya mchakato wa kuwapandisha walimu madaraja aliosema ulikwama kwa siku nyingi.

Walimu pamoja na mengineyo wamekuwa wakilalamika kusitishwa kwa upandishwaji wa madaraja, jambo ambalo kwa wengi lilikuwa likiwavunja moyo wa uwajibikaji.

Hii bila shaka ni habari njema kwa walimu, ambao siyo tu sasa watapumua kwa kupandishwa madaraja lakini pia Serikali imeeleza kuwa walimu hao watapandishwa madaraja kwa mserereko ili kusiwepo urukwaji wa madaraja kwa wahusika.

Tunapongeza hatua hiyo ya Serikali kwa kuwa inaleta faraja kwa walimu ambao sasa tunaamini siyo tu watafarijika, lakini hatua hiyo ni motisha kwao ya kuwajibika zaidi. Pamoja na usemi kuwa ualimu ni wito, lakini kiukweli moyo wa uwajibikaji kwa walimu hukua zaidi, pale mwajiri wao anapowathamini ikiwamo kuwapandisha madaraja.

Tafiti na uzoefu vinaonyesha kuwa walimu wakipewa motisha kwa namna mbalimbali, ari yao ya kufundisha huongezeka na hivyo kuleta matokeo chanya katika ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Mathalani, ripoti ya utafiti wa kiujifunza iliyotolewa na Twaweza mwishoni mwa mwaka 2017, inaonyesha asilimia 91 ya walimu waliohojiwa walikiri kuwa motisha kwao inachochea kiu ya kufundisha na mwishowe kufaulisha wanafunzi.

Tunaamini upandishaji wa madaraja ni mfano mmoja wa aina za motisha ambazo Serikali inapaswa kutoa kwa walimu tena mara kwa mara.

Serikali ikiwa mwajiri wa walimu haina budi kukumbuka kuwa kusitisha upandishaji wa madaraja, kulimbikiza stahili zao, ni vichocheo vya kukwaza jitihada za walimu ambao kimsingi hapa nchini bado wanafanya kazi katika mazingira magumu.

Serikali inaweza kukwama kuwajengea walimu nyumba, ikashindwa kuwaendeleza kielimu, lakini inapojihimu kuwapandisha madaraja na kulipa stahili zao, kunawapa walimu ari ya kuwajibika.

Hatuna budi kukubali kuwa kiuhalisia katika shule nyingi, uwajibikaji wa walimu sio wa kuridhisha na ndio kwa kiwango kikubwa unaochangia kuporomoka kwa kiwango cha kujifunza na mwishowe elimu yetu kwa jumla.

Tunaishauri Serikali kuwa hatua hii ya kupandisha madaraja iwe mwanzo wa kuzifanyia kazi kero mbalimbali zinazowasibu walimu nchi nzima.

Inatia moyo kwa mfano kuona Serikali ikilipa malimbikizo ya walimu, ambapo hadi Juni 2017, Waziri Kakunda alisema Serikali ilishalipa Sh14,236 bilioni kati ya Sh69,461 bilioni ambazo walimu walikuwa wakiidai Serikali hadi kufikia mwaka 2015/16

Hata hivyo, Serikali isiishie kulipa malimbikizo au kupandisha madaraja pekee, lazima iendelee kuwatazama walimu kwa jicho karibu kama kada muhimu ya utumishi wa umma na mhimili wa maendeleo ya Taifa letu.