Serikali iongeze nguvu katika Saratani

Friday December 7 2018Dk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

Niliwahi kushiriki semina ya mafunzo ya tiba ikihusisha wataalamu wa saratani kutoka Tanzania na Kenya na kuratibiwa na ushirikiano wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), ikishirikisha pia wataalamu wa afya kutoka Chuo cha Afya cha Royal cha nchini Uingereza. Ni mpango wa kuandaa utaratibu wa usajili wa watu wenye saratani hapa nchini ambayo ni sehemu ya sera mpya ya afya katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Nikiwa kama daktari ambaye pia nimejikita kwenye masuala ya saratani, nakutana na changamoto kadha wa kadha kwenye idara ya magonjwa ya saratani, moja ya changamoto ninazokutana nazo siyo tu kutibu wagonjwa wa saratani, lakini pia kuhakikisha natoa elimu kwa wagonjwa wangu na jamii zinazowazunguka kuhusu ukubwa wa tatizo hili hapa nchini na kasi ya kuenea kwake ili kuwaepusha watu na mazingira hatarishi yanayosababisha magonjwa ya saratani.

Kukabiliana na magonjwa ya saratani kunaanzia tangu hatua za awali za kujikinga nayo na hata kuyadhibiti yasiendelee kuongezeka, hivyo sisi madaktari tunategemea sapoti kubwa kutoka serikalini ili kutusaidia kutoa elimu kwa wagonjwa wetu.

Hivyo, kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa sababu imeliona hili na hivyo imeamua kushirikiana na taasisi zingine ikiwamo ile ya Benki ya Maendeleo ya Afrika ya Mashariki (EADB), na Chuo cha Afya cha Royal cha nchini Uingereza kuunda mpango wa muda mrefu wa kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya wapatao zaidi ya 600 kutoka Afrika Mashariki.

Lengo ni kutusaidia sisi watumishi wa afya kutoa elimu kwa wananchi juu ya utambuzi wa mapema, utafiti na matibabu ya saratani kwa ujumla hususani katika jamii na maeneo ambayo yana changamoto ya wataalamu wa magonjwa haya.

Kwa sasa Taifa linategemea takwimu za saratani kutoka kwenye hospitali na vituo vingine vya afya, kwa maana kwamba wale wagonjwa wanaoripoti huko ndio wanaoingia kwenye takwimu

Hivyo, usajili huu utaiwezesha Serikali kufahamu ni maeneo gani ambapo ugonjwa huu umeenea zaidi hivyo kuwa katika nafasi ya kugawa rasilimali zake katika kukabiliana na janga hili.

Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinathibitisha kuwa idadi ya kesi zinazohusiana na saratani duniani zinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 75 katika kipindi cha miongo miwili ijayo.