MAONI: Serikali itatue matatizo ya shule zake

Tuesday January 28 2020

Hivi karibuni Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lilitangaza matokeo ya mitihani ya shule za msingi na zile za sekondari.

Necta iliweka hadharani matokeo ya darasa la nne kwa shule za msingi wakati kwa elimu ya sekondari yalikuwa yale ya kidato cha pili na kidato cha nne.

Hata hivyo, matokeo kwa ujumla wake yametoa picha ya shule za umma kufanya vibaya kwenye mitihani ya taifa tofauti na shule za binafsi.

Hali hii inatokea katika miaka ya karibuni kwa shule za binafsi kufanya vizuri tofauti na shule za umma.

Necta ilipotangaza matokeo ya mtihani wa kidato nne mwaka 2019, ilizitaja shule 10 zilizofanya vizuri zikiongozwa na Shule ya Sekondari ya Kemebos ya mkoani Kagera ambayo ilishika nafasi ya kwanza kitaifa.

Shule nyingine tisa zilizofanya vizuri zaidi katika matokeo hayo zilikuwa ni pamoja na St. Francis Girls ya Mbeya ambayo mwaka juzi ilishika nafasi ya kwanza kabla ya kushushwa na Kemebos.

Advertisement

Nafasi ya tatu kwa mujibu wa Necta ilienda kwa Shule ya Sekondari Feza Boys ya jijini Dar es Salaam zilizofuata ni Cannosa (Dar es Salaam), Anwarite Girls (Kilimanjaro), Precious Blood (Arusha) na Marian Boys (Pwani). Nyingine ni St Augustine Tagaste (Dar es Salaam), Maua Seminary (Kilimanjaro) na Musabe Boys ya jijini Mwanza ambayo imeshika nafasi ya 10 kitaifa.

Kwa matokeo hayo, hakuna hata shule moja ya Serikali iliyofanikiwa kuingia katika orodha hiyo, kama ilivyokuwa mwaka jana.

Necta majuzi ilitoa orodha ya ubora wa shule kutokana na matokeo hayo ya mtihani wa kidato cha nne.

Katika orodha hiyo ni shule saba tu za serikali ambazo zimeingia katika orodha ya zilizoshika nafasi 100 za mwanzo.

Matokeo yamekuja kipindi ambacho Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuziimarisha shule zake hasa zile kongwe na maarufu.

Shule hizo ambazo zimeingia katika orodha hiyo ni pamoja na Mzumbe, Kilakala, Msalato, Kibaha, Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, Shule ya Sekondari Ilboru na Shule ya Sekondari Lumumba.

Hata hivyo, shule hizo zimefanya vibaya katika kipindi ambacho Serikali inafanya jitihada kuinua hadhi ya shule hizo.

Kufikia Februari 26, mwaka jana, serikali ilikuwa imetumia kiasi cha Sh42 bilioni kwa ajili ya kukarabati shule 42.

Tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani mwaka 2015, kumekuwa na jitihada za kusaidia kuinua shule hiyo.

Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa pamoja na jitihada za Serikali kumwaga fedha nyingi kwa shule hizo lakini bado zimekuwa zinafanya vibaya.

Ikumbukwe kuwa shule hizo zina mchango mkubwa katika kuinua sekta ya elimu nchini kwa kuwa ndizo zinazopokea wanafunzi wengi zaidi na hivyo ni muhimu kwa Serikali kuyafanyia kazi matatizo yanayozikabili shule hizi.

Katika miaka ya nyuma, ilishuhudiwa wanafunzi bora walikuwa wanakwenda katika shule zinazomilikiwa na Serikali kutokana na ubora wa kiwango cha elimu kinachotolewa huko.

Shule za Serikali bado ni tegemeo kubwa na hasa kwa wale watu wa kipato cha chini wakati shule za binafsi zaidi zinapokea watoto wa familia zenye uwezo.

Kuendelea kwa hali hii kunaweza kujenga tabaka la watu wa kipato cha chini ambao hawapati elimu bora wakati wale wenye uwezo wakipata elimu nzuri, jambo hili linapaswa kuangaliwa kwa mapana na marefu.

Na ndio maana tunaamini suluhisho pekee ni Serikali kuzifanyia marekebisho shule zake ili si tu ili zirudishe hadhi yake bali pia ziendelee kuwa kimbilio la wananchi kutoka familia zisizo na uwezo.