MAONI: Serikali iwalipe chao wakulima wa korosho

Kwa mara nyingine hoja ya zao la korosho iliibuka bungeni jijini Dodoma juzi, iliibuliwa na mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye.

Nape katika hoja yake alidai kuwa kuna watu waliohujumu zao la korosho akitaka watu hao wawajibike wenyewe na wasipofanya hivyo atawasilisha bungeni kusudio la kutaka kuwataja mmoja mmoja.

Mbunge huyo pia aliizungumzia nia njema ya Rais John Magufuli katika zao hilo, lakini waliokwenda kutekeleza mchakato mzima wa ununuzi walikwenda kuua zao hilo akidai kwamba mchakato huo ulitawaliwa na ubabaishaji, uongo, dhulma na rushwa.

Nape pia alifafanua kwamba wapo wakulima ambao hadi juzi walikuwa hawajalipwa fedha zao licha ya korosho zao kuchukuliwa.

Kwa hatua ambayo imefikia tunadhani ni vyema Serikali ikaangalia namna ya kuwalipa wakulima hasa kwa kuwa ni takriban miezi sita sasa imepita sasa tangu kuanza kipindi cha mavuno na ukusanyaji wa korosho.

Serikali inaweza kuwa na majibu mengi ya matatizo na hata kutangaza idadi ya wakulima waliolipwa lakini kwa kuwa ni wazi kwamba wapo wengine tena wengi tu ambao bado hawajalipwa na itapendeza kwanza ambao hawajalipwa wakilipwa.

Tunasema hivyo kwa sababu mkulima anapokosa malipo yake kwa kipindi cha takriban miezi sita maana yake ni kwamba hali hiyo inaathiri shughuli zake za kilimo pamoja na mahitaji yake mengine ya kijamii ikiwamo elimu kwa watoto na wategemezi wake na mengineyo.

Kumkwaza mkulima katika shughuli zake za kilimo maana yake ni kuathiri kilimo chenyewe jambo ambalo si zuri na ndio maana tunaihimiza Serikali kuhakikisha wakulima wanalipwa stahiki zao.

Inasikitisha kuona kwamba msimu mwingine unaingia wakati wakulima wakihaha kufukuzia malipo ya msimu uliopita, malipo ambayo hadi sasa hawajajua watayapata lini.

Tunatambua kwamba hadi hapa tatizo lilipofikia wapo ambao wamehusika kwa namna moja au nyingine kama ambavyo Nape amebainisha katika hoja yake.

Tunajua kwamba zipo taratibu za kufuatwa kwa watu hawa lakini wakati Serikali ikifikiria hilo, ni vyema kwanza ikawaangalia wakulima na kuweka utaratibu wa kuwalipa na baada ya hapo iwashughulikie hao waliosababisha tatizo kama kweli wapo.

Tunasema hivyo kwa sababu hatutapenda kusikia suala la malipo limesimamishwa ili kuanza kuwasaka waliosababisha tatizo, kufanya hivyo ni kuendelea kumuumiza mkulima ambaye tayari ameumizwa kwa kucheleweshewa malipo yake.

Tunaamini Serikali ikiamua jambo hili linawezekana na hivyo kuwatoa wakulima wa korosho katika unyonge walionao sasa.

Zaidi ya hilo tungependa kuona kilichotokea katika korosho kisijirudie misimu ijayo, tunaamini Serikali imejifunza kitu kuanzia kuihusisha kampuni ya Indo Power Solutions ya Kenya ambayo baadaye ilibainika kuwa haikuwa na uwezo wa kununua korosho.

Kilichotokea kwa kampuni ya Indo Power na matatizo mengine yabaki kuwa somo tosha kwa Serikali ili kuhakikisha wakulima hawasumbuliwi na badala yake wanafaidi matunda ya zao la korosho.