UCHAMBUZI: Simba itumie vyema fursa ya ujio wa Sevilla FC

Monday May 13 2019Abdallah  Mweri

Abdallah  Mweri 

Simba inatarajiwa kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya timu inayoshiriki mashindano ya Ligi Kuu Hispania (La Liga) Sevilla.

Simba itacheza na Sevilla kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Mei 23 na timu hiyo inatarajiwa kuwasili nchini Mei 21.

Sevilla iliyoanzishwa miaka 129 iliyopita nchini humo, inakuja nchini kwa udhamini wa kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa Tanzania.

Hii ni mara ya pili SportPesa kuzileta nchini klabu maarufu zinazoshiriki Ligi Kuu Ulaya. Mwaka 2017 Everton ya England ilicheza na Gor Mahia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

SportPesa imefanya jambo jema ambalo linapaswa kuigwa na kampuni au taasisi nyingine nchini kuzileta klabu za Ulaya kucheza na timu zetu mechi za kirafiki.

Ujio wa Sevilla ni fursa kwa klabu ya Simba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Serikali kwa ujumla kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamadumi na Michezo.

Sevilla ni klabu kubwa Ulaya na ujio wake unaweza kufungua milango kwa Simba, TFF na Serikali endapo zitatumia vyema fursa hii.

Miongoni mwa fursa ambazo maeneo hayo yanaweza kutumia ni kutengeneza mtandano baina ya Simba au klabu zetu na Sevilla ambao unaweza kuwa na tija hapo baadaye.

Fursa ya kwanza ambayo Simba inaweza kuitumia vyema katika mchezo wake na Sevilla ni kucheza soka ya kiwango bora ili kuishawishi klabu hiyo kutambua Tanzania kuna vipaji.

Endapo wachezaji wa Simba watajipambanua kwa kutumia uwezo wao kucheza kwa kiwango bora mchezo huo bila kujali matokeo ya uwanjani, watakuwa na nafasi ya kuishawishi Sevilla kwamba Tanzania kuna vipaji.

Kiwango bora cha Simba kinaweza kuishawishi Sevilla kutupia jicho timu yao ya vijana kwa kuangalia baadhi ya wachezaji wenye vipaji wanaoweza kwenda kucheza soka Hispania.

Kwa bahati njema, Simba ina utaratibu mzuri wa timu ya vijana kwa muda mrefu imekuwa ikitengeneza wachezaji wanaochipukia ambao baadaye wanakuwa tishio katoka kikosi cha kwanza.

Baadhi ya wachezaji wa Simba waliopikwa kutoka timu ya vijana ni Jonas Mkude, Saind Ndemla, Abdallah Seseme Mwadui ya Shinyanga, William Lucian ‘Gallas’, Miraji Athumani (Lipuli), Ibrahim Ajibu (Yanga), Ramadhani Singano (Azam) na Miraji Adamu wa Coastal Union.

Wengine wanaocheza kwasasa katika kikosi hicho ni chipukizi Rashid Juma na Ali Salim ambao Kocha Patrick Aussems amekuwa akiwatumia katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Kwa mantiki hiyo Simba ina nafasi ya kutumia fursa hiyo kuanzisha uhusiano wa kirafiki na Sevilla ambao utakuwa na manufaa kwa upande wao na Taifa.

Naamini Simba ikianza kushirikiana na Sevilla itakuwa na nafasi nzuri ya kuwatoa wachezaji wake kwenda Hispania kucheza sola la kulipwa. Hii ni fursa ambayo Simba haitakiwi kufanyia mzaha.

Ni vyema viongozi wa Simba wakatumia ujio wa Sevilla kutengeneza mtandano mpana ambao utakuwa daraja kwa wachezaji wake kwenda kucheza soka nje ya nchi.

Sevilla ni klabu kubwa duniani ina uzoefu wa kutosha katika medani ya soka ikiwa na madaraja tofauti ya timu za vijana ambazo zimekuwa chimbuko la kupata timu imara ya kikosi cha kwanza.

Kwa muda mrefu Tanzania tumeshindwa kupata mafanikio katika mashindano ya kimataifa kwa kuwa hatuna msingi bora wa wachezaji walioandaliwa katika timu za vijana.

Endapo tungekuwa na mfumo mzuri kama zilivyo baadhi ya nchi za Afrika zilizopiga hatua katika soka kwa kuwa na idadi kubwa ya akademi, Tanzania tungekuwa mbali katika mchezo wa soka kulinganisha na hivi sasa ambapo tumekuwa tukiungaunga timu zetu za Taifa. Kocha wa zamani wa Taifa Stas, Kim Poulsen aliwahi kusema kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya wachezaji wenye vipaji, lakini inakosa timu imara za Taifa kwa kuwa hakuna muunganiko mzuri kuanzia ngazi za akademi, klabu na timu za Taifa.

Baada ya miaka 39, Tanzania tumepata tiketi ya kucheza Fainali za Afrika nchini Misri, hii inathibitisha jinsi gani tusivyokuwa na mipango ya muda mfupi, kati na mrefu wa kutengeneza idadi kubwa ya wachezaji hodari kwa kutumia akademi.

Kwa muktadha huo, ujio wa Sevilla utumike kama njia mojawapo ya kutengeneza mtandano mpana kwa klabu zetu ambao utakuwa na manufaa ya kuzalisha wachezaji waliopitia misingi ya uchezaji.

Hii ni fursa pekee ambayo Simba inaweza kuitumia kwa ustawi wa maendeleo yao ya soka kwa maana ya klabu na Taifa kwa ujumla.