MAONI: TFF imeligawa Taifa kwa Twiga Stars

Monday November 25 2019

 

Timu ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars, jana ilikuwa ikicheza na Uganda katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati, inayojulikana zaidi kama Kombe la Chalenji.

Lakini cha ajabu, wakati Twiga Stars ikicheza mechi hiyo kwenye Uwanja wa Azam ulio Chamazi, mabingwa wa soka nchini, Simba walikuwa wakicheza mechi ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa.

Mechi hiyo ni moja ya mechi kadhaa za ligi hiyo ambazo zilianza tena mwishoni mwa wiki baada ya Ligi Kuu kusimama kupisha michuano ya kimataifa, ambayo ilikuwa ni kwa ajili ya kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2021 (Afcon) na Michuano ya Ubingwa wa Afrika (Chan).

Si jambo la kawaida kwa timu yoyote ya taifa kuwa na mechi ya aina yoyote ya kimataifa na bado mechi za ligi zikaendelea kama kawaida. Huku ni kutoipa umuhimu timu ya taifa.

Na inapokuwa jambo hilo linafanyika kwa timu ya wanawake, suala hilo huwa kubwa zaidi kwamba Shirikisho la Soka (TFF) haliipa umuhimu timu ya wanawake na linaweka kipaumbele kukusanya mapato ya mechi za ligi kuliko utaifa.

Hii si mara ya kwanza kwa jambo hilo kutokea. Mapema mwaka huu wakati wa mashindano ambayo Tanzania iliomba kuyaandaa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17, TFF iliruhusu klabu za Simba na Yanga kucheza mechi za kirafiki wakati michuano hiyo, iliyogharimiwa na Serikali ikiendelea.

Advertisement

Timu hizo zilicheza mechi za kirafiki mjini Mwanza na Arusha na hivyo kusababisha mashabiki kuelekeza akili zao kwenye klabu zao na kusahau utaifa uliokuwa unawakilishwa na vijana wetu, ambao hawakuweza kulibakiza kombe licha ya nguvu kubwa iliyotumika.

Duniani kote, timu za taifa hucheza mechi zake wakati mashindano mengine yamesimama. Hii husaidia kulifanya taifa lisigawanyike na hivyo kuwa kitu kimoja wakati wote wa michezo hiyo.

Na mechi za mashindano mengine zisipoendelea, maana yake mashabiki wataona umuhimu wa kwenda viwanjani kuangalia timu ya taifa lao na hivyo kwenda kwa wingi na kuiongezea nguvu nchi yao.

Pia unapokuwa na mashabiki wengi ndipo unapopata hata nguvu ya kushawishi kampuni kuwekeza fedha zao kwenye timu hiyo na programu nyingine za maendeleo, sanjari na kuwa na uwezo wa kuuza bidhaa zinazohusiana na timu hiyo. Lakini TFF inaporuhusu mechi nyingine, mshikamano huo unakosekana na mambo mengine mengi kushindikana.

Michuano ya Kombe la Chalenji kwa Wanawake haikuja kama mvua. TFF ndio iliomba kuwa mwenyeji na haikulazimishwa. Hivyo ilistahili kuweka mambo yake sawa kuhakikisha mashindano hayo yanapewa umuhimu unaostahili na mashabiki hawagawanywi katika makundi ya klabu zao kama ilivyofanyika.

Hata michuano ya U-17, TFF iliomba kuiandaa takriban miaka minne iliyopita na hivyo ilikuwa na muda wa kutosha kupanga mambo yake ili wakati huo, Taifa zima lielekeze akili zake kwenye timu moja tu na si kuruhusu mechi za kirafiki ambazo zinaondoa mshikamano na kugawanya utaifa.

TFF haina budi kuhakikisha kuwa inapanga shughuli zake kwa kuona mbali na kuzingatia mambo muhimu kama ushiriki wa timu zetu za taifa katika mashindano ya kimataifa, hasa yanapokuwa yanafanyika ndani ya nchi.