TFF isijisahau mafanikio haya ya timu zetu za vijana

Monday May 14 2018Dk Mshindo Msolla

Dk Mshindo Msolla 

Katika makala zangu zinazohusu timu zetu za vijana- Serengeti na Ngorongoro, nilianisha umuhimu wa kuwa na mkakati makini wa kuzihudumia timu hizo, moja ikiwa imefuzu moja kwa moja katika fainali zitakazofanyika hapa ambapo Tanzania tutakuwa wenyeji na nyingine ikiwa imefuzu kuingia mzunguko wa pili wa michezo ya CAF ya vijana chini ya miaka 20.

Matumaini ya Watanzania sasa yanahamia kwenye timu hizi za vijana.

Serengeti wameonyesha wanaweza kwa kuchukua kikombe cha Cecafa kwa vijana chini ya miaka 17 yaliyomalizika hivi karibuni huko Burundi.

Pamoja na mafanikio hayo, naishauri TFF iendelee na programu za kuzithamini timu za vijana wa umri mdogo kwa kufanya yafuatayo:

Kuimarisha kituo chake cha Karume na kuhamasisha uanzishwaji wa vituo kama hivyo Mkoa wa Dar es Salaam

TFF kwa kipindi kirefu imekuwa na utaratibu wa kuwa na mazoezi ya vijana wa umri tofauti na vijana wengi wametokea hapo, kama Thomas Ulimwengu na wengine wengi ambao sasa wanacheza nje au wanaendelea na mafunzo katika nchi nyingine.

Hakuna ubishi kwamba idadi ya timu na wachezaji wa mpira kwa ujumla ni kubwa Da es Salaam kuliko mikoa mingine. Kwa kuwa uongozi wa TFF uko Dar na pia makocha wengi wako Dar, ninashauri TFF iongee na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na vyama vya wilaya zake ili kwa pamoja vianzishwe vituo vingine huko ili kuweza kuwapata wachezaji wengi zaidi wa umri wa chini ya miaka 10, 12 na 15. Mafanikio ya Serengeti iliyopita (ambayo sasa ni Ngorongoro) na Serengeti ya sasa ninaamini wazazi wenye watoto wenye vipaji watakuwa na shauku ya kutaka watoto wao washiriki.

TFF ihamasishe uanzishwaji wa vituo vya namna hiyo mikoani

Utaratibu unaotumika sasa pale Karume unaweza kabisa kuanzishwa katika mikoa mingine na ikaratibiwa na vyama vya makocha vya mikoa na wilaya husika kwa kushirikiana na vyama vya mikoa na wilaya.

Hakuna gharama kubwa ambazo zitahusisha wanaoandaa kwa sababu hapo ni mipira tu ambayo itatakiwa iwepo.

Wazazi/walezi wa wachezaji watatakiwa kuwawezesha wachezaji wao kuwa na vifaa vya michezo.

Ikiwa hayo yatafanyika, vijana wengi watapatikana. Mashindano ya kitaifa ya Copa Coca-Cola, Airtel Rising na Umitashumta yasaidie kuibua vipaji.

Mashindano hayo niliyoyataja na mengine ambayo yatakuwa yamejitokeza, yatumike vizuri kuweza kuwapata wachezaji wenye vipaji.

TFF pia ivifuatilie vituo vyote vya kuendeleza vipaji vilivyosajiliwa (football academies) ili nao wajumuishwe.

TFF iendelee kuunda Serengeti nyingine kwa kuwa kila mwaka miaka inabadilika na wanatoka miaka 17 na kuhamia umri mwingine na si wale tena wa U-17. Maisha yanakwenda kasi sana.

Utaratibu huu ulioanzishwa na uongozi wa TFF uliopita na ukaendelezwa na uongozi wa sasa wa kuweka misingi ya kuwa na timu za vijana kuanzia miaka 12, uendelee.

Maana yangu hapa ni kwamba TFF sasa hivi iunde timu nyingine ya vijana wa umri wa miaka chini ya 12 na wawekwe sehemu moja kama msingi wa uundwaji wa timu hiyo.

Aidha, utaratibu uliotumika wa kuiboresha timu ya U-12 kwa kuongeza wachezaji wengine wenye vipaji wanaojitokeza uendelee.

Changamoto zilizojitokeza awamu hii baina ya TFF na mmiliki wa Shule za Alliance unatakiwa usijirudie ili kuwashawishi wengine wenye shule kama hizo (mathalani Lord Baden Powel ya Kanali mstaafu Kipingu) wasisite kuwapokea vijana kama hao.