MAONI: TFF itumie muda huu kujadili viporo vya adhabu

Monday March 23 2020

Mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Daraja la Kwanza na Kombe la FA yamesimama kwa muda kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Serikali kupitia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ilisimamisha michezo yote kwa kuhofia maambuzi ya virusi vya corona katika mikusanyiko ya watu.

Maambukizi ya virusi hivyo yamezikumba nchi nyingi duniani na michezo takribani yote imesimamishwa.

Baadhi ya ligi Ulaya zimetangaza mashindano yake kuanza Aprili 3 au 4 na nyingine zimeshindwa kutoa matamko hadi pale hali itakapokuwa nzuri.

Hapa nchini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na klabu za soka zimeitikia vyema agizo la Serikali kwa kuwapa mapumziko wachezaji wao.

Hata hivyo, wakati mashindano hayo yakisimamishwa, kulikuwa viporo ambavyo havikutolewa uamuzi kutokana na sababu mbalimbali.

Advertisement

Baadhi ya matukio yaliyotakiwa kutolewa uamuzi yalijiri katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo hadi sasa hayajatolewa uamuzi.

Baadhi ya klabu zilipeleka malalamiko kwa Kamati ya Saa 72 na nyingine zililalamikiwa kwa madai ya kufanya matukio ya utovu wa nidhamu.

Miongoni mwa matukio yaliyopelekwa Kamati ya Saa 72 ni baadhi ya timu kushindwa kutumia kwa usahihi milango iliyowekwa kwa ajili ya kuingia uwanjani.

Malalamiko mengine ni baadhi ya timu kugomea kutumia vyumba vya kuvalia nguo kwa sababu binafsi jambo ambalo ni uvunjifu wa kanuni za soka.

Mbali na sababu hizo, baadhi ya wachezaji walionyesha utovu wa nidhamu kwa kufanyiana madhambi na makocha kutoa kauli zisizofaa kwa waamuzi.

TFF kupitia kamati zake, imeshatoa adhabu kutokana na matukio hayo, lakini yapo matukio ambayo yamebaki viporo kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa kuwa mashindano yamesimama, ni vyema kamati zinazoshughulikia matukio hayo kutumia kipindi hiki kujadili na kutoa adhabu kwa wahusika ili mashindano yakatapoanza kusiwe na viporo.

Tunasema hivyo kwa sababu yapo matukio ambayo yamedumu ndani ya kamati hiyo kwa muda mrefu bila kutolewa uamuzi ingawa kamati hiyo ni ya saa 72.

Tunatambua kwamba Serikali imekataza mikusanyiko ya watu, lakini kamati husika inaweza kutumia teknolojia ya video kujadili matukio hayo na kutoa uamuzi.

Tayari waziri mkuu ameonyesha njia kwa kutumia njia hiyo kuzungumza na wakuu wa mikoa na viongozi mbalimbali kuhusu maambuzi ya virusi vya corona.

Endapo TFF itatumia teknolojia ya video inaweza kufanya kazi zake kwa usahihi na muda mwafaka kwani haipendezi mashindano hayo kuanza na dosari za viporo.

Mbali na matukio hayo, TFF na Bodi ya Ligi zina wajibu wa kutumia kipindi hiki kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika mashindano kuanzia Ligi Kuu hadi Daraja la Pili.

Bila kufanya mikusanyiko, viongozi wa taasisi hizo wanaweza kutumia uchache wao kuboresha mashindano au ikibidi kutumia teknolojia ya video kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji. Ni vyema ligi ikianza bila changamoto ya viporo vya adhabu au mkanganyiko wa ratiba.