Tahadhari mvua za masika ituzindue usingizini

Saturday February 15 2020

Tukiangalia kwa mazoea, tangazo la mwelekeo wa mvua za masika ambalo limetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tunaweza kulipuuza na kuona ni mambo ya kawaida.

Lakini ukweli ni kwamba katika utabiri huo unaoeleza kutakuwa na mvua za “wastani hadi juu ya wastani”, kuna mambo ya kutazama na kufanyia kazi ili kuepukana na madhara yanayoweza kutokea kutokana na mvua hizo yakiwamo mafuriko, upotevu wa mali, uharibifu wa makazi na watu kupoteza maisha.

TMA inawashauri wahusika katika kila eneo la nchi linaloguswa na utabiri huo, hasa menejimenti za maafa na watoa huduma za dharura, kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo zitakazonyesha kati ya Machi na Mei.

Kulingana na utabiri huo, maeneo ya mkoa wa Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, maeneo mengi ya mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mashariki mwa mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara yatapata mvua za wastani na juu ya wastani.

Kulingana na tamko la TMA, hata mvua za nje ya msimu zinazoendelea sasa katika maeneo yanayopata mvua za masika hususan maeneo yaliyopo katika pwani ya kaskazini, kuwa zinatarajiwa kuendelea na kuungana na msimu wa masika 2020.

Tumesema tangazo hilo linaweza kuonekana la mazoea kwa kuwa si mara ya kwanza kwa TMA kutoa taarifa kama hii, japokuwa kila mara maudhui yanatofautiana kulingana na utabiri wenyewe, lakini wengi huipuuza na kuichukuliwa kimazoea lakini mwisho wa siku hukumbana na maafa au athari kadha wa kadha.

Advertisement

Kama ambavyo TMA haichoki kutoa tahadhari, hata sisi tunaendelea kuwakumbusha wasomaji wetu kuhusu athari na faida za mvua hizo ili ziweze kutumika kwa manufaa.

Ni vizuri tukabadilika na kuanza kufuatiliwa taarifa za hali ya hewa ili kila mwananchi afahamu siku au wiki inayofuata itakuwaje ili ajiandae katika shughuli zake.

Taarifa hizi ni suala linaloathiri nyanja za kiuchumi, kijamii na kiafya, mfano kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo, wanatakiwa kufahamu kuwa msimu huu wa masika utakavyokuwa kila eneo, hivyo waelewe aina ya mazao wanayotakiwa kupanda na kwa muda gani.

Pia maeneo na mengine ambayo yatakuwa na mvua chini ya wastani, kama mkoa wa Kagera, magharibi mwa mkoa wa Geita, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Pwani na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, nayo yakae mguu sawa kutumia mbinu za kuongeza uzalishaji na kuzingatia ushauri wa wataalamu katika matumizi sahihi ya ardhi na mbegu zinazotoa mazao kwa muda mfupi na kustahimili upungufu wa mvua.

Pia maeneo hayo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani, wananchi wanapaswa kuzingatia mbinu za kuhifadhi maji na kudhibiti ubora wa mavuno.

Si hayo tu, menejimenti ya maafa inatakiwa kutoa taarifa kwa wakazi wa mabondeni, karibu na mito na yale ya tambarare ili wachukue tahadhari.

Ili kuepuka athari zitokanazo na mafuriko, mamlaka za miji zihakikishe mifumo ya njia za kupitisha maji inafanya kazi huku sekta ya afya nayo ikijiandaa vilivyo kukabiliana na athari nyingine za kiafya kama vile magonjwa ya milipuko.

Kwa ujumla sote tunapaswa kujifunza kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuzifanyia kazi.