Tanzania ina kila sababu ya kushinda kesho

Muktasari:

  • Mechi hiyo ni ngumu kwa kuwa ni lazima Tanzania ishinde huku ikiombea timu nyingine katika kundi hilo, Lesotho ifungwe na Cape Verde, ambayo ina pointi nne katika mechi nyingine ya kundi hilo itakayofanyika Praia wakati mmoja na ya Stars-Uganda.

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kesho itakuwa mwenyeji wa Uganda katika moja ya mechi mbili za mwisho za Kundi L kuwania tiketi ya kucheza fainali zijazo za Mataifa ya Afrika.

Mechi hiyo ni ngumu kwa kuwa ni lazima Tanzania ishinde huku ikiombea timu nyingine katika kundi hilo, Lesotho ifungwe na Cape Verde, ambayo ina pointi nne katika mechi nyingine ya kundi hilo itakayofanyika Praia wakati mmoja na ya Stars-Uganda.

Uganda imeshafuzu kucheza fainali hizo baada ya kufikisha pointi kumi, wakati Stars ina pointi tano sawa na Lesotho, ambayo kanuni za mashindano hayo zinaipa nafasi nzuri ya kusonga mbele iwapo itashinda kwa kuwa katika mechi mbili dhidi ya Tanzania, ilishinda moja kwa na kulazimisha sare kwenye Uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam.

Kwa hiyo, Tanzania inatakiwa kwanza ielekeze macho yake kwenye Uwanja wa Taifa kuhakikisha inashinda na ndipo ifuatilie mechi ya Praia kama itatoa matokeo yanayoweza kuipa tiketi ya kusonga mbele, yaani ama Lesotho ishindwe au itoke sare.

Hii inaweka umuhimu kwa mashabiki wa soka walio jijini Dar es Salaam na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kesho ili kuipa nguvu timu yetu iweze kuandika ukurasa mpya wa mafanikio katika soka barani Afrika baada ya ukurasa wa awali kuandikwa mwaka 1980 wakati Tanzania ilipofuzu kwa mara ya kwanza kucheza fainali hizo.

Baada ya miaka mingi ya kutofuzu, hasa kutokana na kukosa wachezaji wanaostahili, kuwa na ukata, kutoweza kuajiri makocha wenye sifa, Tanzania inaingia kwenye mechi ya kesho ikiwa na sababu nyingi za kuiwezesha kushinda kuliko za kukubali kufungwa kirahisi nyumbani. Karibu wachezaji sita wanachezea klabu za nje, zikiwemo za barani Ulaya na Afrika Kaskazini ambako kiwango cha soka kiko juu; inaongozwa na Mbwana Samatta, ambaye anaongoza kwa ufungaji nchini Ubelgiji, inafundishwa na kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike ambaye ni mshindi wa kombe hilo wakati akiwa mchezaji na pia ana uzoefu mkubwa kutokana na kuchezea klabu kubwa barani Ulaya kama Barcelona.

Pia inaundwa na wachezaji nyota wa ndani, wakiwemo wa Simba ambao timu yao imefuzu kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika na hivyo kupata uzoefu wa kutosha; inaundwa na wachezaji waliokaa pamoja kwa muda mrefu, hasa wale tegemeo kama Samatta, Simon Msuva, Thomas Ulimwengu, Aggrey Morris, Erasto Nyoni na John Bocco.

Pia timu iko kwenye mikono salama baada ya Shirikisho la Soka (TFF) kupata udhamini unaoifanya timu hiyo iweze kuweka kambi sehemu bora na kucheza mechi za kirafiki inazotaka na kusafiri inakotaka kwa lengo la kufanya maandalizi bora.

Hizo ni baadhi tu ya sababu zinazoifanya Tanzania iwe na uhakika wa kutosha kushinda mchezo huo ambao utaandika historia mpya baada ya kukaa nje ya fainali hizo kwa muda mrefu.

Kwa maana hiyo, mashabiki wana kila sababu ya kwenda kifua mbele kwenye Uwanja wa Taifa kuongeza sababu nyingine ya Tanzania kushinda, yaani nguvu ya shabiki wa 12, ambayo ni muhimu sana katika soka.

Mashabiki wanatakiwa kushajiisha ushindi kwa kushangilia wakati wote badala ya kusubiri mabao ndipo washangilie. Kushangilia kuanzia mwanzo kutawapa wachezaji wetu sababu nyingine ya kushinda mchezo huo, yaani kukidhi utashi wa mashabiki kwa kuishinda Uganda.

Ni matumaini yetu kuwa sababu hizo tosha zitaiwezesha Tanzania kushinda na kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika nchini Misri.