Televisheni nzuri ila sio kwa watoto

Friday December 7 2018

 

Sio mtu mzima wala mtoto asiyependa kukaa na kutazama televisheni. Wengi tunatazama tena wakati mwingine hata kupitiliza mipaka na hatimaye utazamaji huo kuathiri afya zetu.

Katika athari hizo, zipo maalumu kwa watoto ikiwamo kumsababishia mtoto uzito wa mwili, jambo ambalo sio zuri kwa afya ya mtoto.

Wanasayansi nchini Uingereza wamefanya utafi na kubaini kuwa mtoto atazamapo televisheni, kitendo hicho kinaweza kumuongezea uzito.

Mtoto anapokuwa na kifaa hiki katika chumba chake anakuwa huru zaidi kuangalia kwa muda anaoutaka na huenda wengine wanakosa muda wa kula na hata kulala kwa wakati.

Watafiti hao walibaini kuwa watoto wa kike ndio wanaoathirika zaidi kwa kuangalia televsiheni kwa muda mrefu, hivyo wanakuwa na uwezekano mkubwa wa uzito wa miili yao kuongezeka

Utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la Kimataifa la International Journal of Obesity ulitathmini takwimu kutoka kwa watoto wadogo zaidi ya 12,000 nchini Uingereza.

Mtafiti Dk Anja Heilmann, alisema utafiti unaonyesha kuwa kuna ushahidi wa wazi wa uhusiano kati ya kuwa na televisheni chumbani na kuongezeka kwa uzito wa mwili wa mtoto.

Wataalamu nchini

Dk fazeel Sajeed kutoka hospitali ya Sanitas anaunga mkono utafiti huo kwa kusema mara nyingi watoto huwa wanatazama televisheni wakiwa wanakula.

Anasema mtoto ambaye anaangalia televisheni akiwa anakula huwa anakula chakula kingi ukilinganisha na yule ambaye anakula bila kutazama.

‘’Nakubaliana na utafiti huu kwani mtoto anapokuwa karibu na televisheni anakuwa na uzito. Mara nyingi watoto hupenda kuangalia huku wanakula na unakuta vyakula wanavyokula ni vile vyenye sukari na mafuta, mfano viazi (chips)’’anasema

Dk Sajeed anashauri wazazi wawapunguzie watoto muda wa kuangalia televisheni hasa kwa wale waliowakea kifaa hicho vyumbani.

Anaongeza kuwa si vibaya mtoto kutazama runinga ila anatakiwa kutazama vitu ambavyo atajifunza kama mtoto na tena sio kuangalia kwa saa nyingi hali inayoweza kumletea madhara kiafya.

“Kama chumbani kwa mtoto kuna televisheni basi ni jukumu la mzazi kuhakikisha kwamba mtoto anapangiwa muda wa kuangalia na mzazi ana jukumu la kuhakikisha mtoto haathiriwi na ile runinga aliyomuwekea chumbani,”anasema.

Kwa upande wake, Dk Katoto Nestory anasema huenda kweli mtoto kuwa na luninga chumbani kwake kunaweza kumsababishia uzito, kwa sababu mtoto anakuwa amekaa sehemu moja kwa muda mrefu

“Ifahamike kuwa uzito wa mwili hupungua kwa kufanya mazoezi kwa hiyo kama mtoto anachukua muda mwingi kukaa akitazama televisheni ina maana mwili unakuwa umetulia hivyo kusababisha uzito kuongezeka”

Dk John Vicent anasema suala la mtoto kuwa na uzito kupindukia halina uhusiano wa moja kwa moja na mtoto kuangalia runinga kwa muda mrefu lakini huenda likachangia

Anasema mara nyingi watoto wanapokuwa likizo au siku ambazo hawajaenda shule, hutumia muda mwingi kuangalia televisheni hasa katuni.

Anadai kwamba mtoto anapokaa kwa muda mrefu sehemu moja anajijengea tabia ya uvivu hii inafanya hata chakula anachokula kutomeng’enywa vizuri na hatimaye mtoto anakuwa na uzito mkubwa na hata kunenepa zaidi.

Dk Vicent anaongeza kuwa tatizo la kuwa na uzito mkubwa si kwa watoto pekee, bali hata kwa watu wazima ambao wanakaa sehemu moja kwa muda mrefu

Nashauri wazazi wawe makini na watoto wao suala la afya kwa mtoto linahitaji umakini wa hali ya juu watambue kuwa mtoto anapokuwa na televisheni ndani ya chumba chake sio tu ataongezeka uzito kama utafiti unavyoeleza, bali inaweza kuvunja maadili ya mtoto

Wazazi wazungumza

Mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam Maimuna Shabani amesema mzazi kumuwekea mtoto televisheni katika chumba cha kulala sio tu itamsababishia madhara kama kuwa na uzito wa kupindukia lakini pia anaweza kupotoka kimaadili.

Anasema ni vyema wazazi wakatumia utafiti huu kujifunza na kutambua kwamba runinga chumbani kwa mtoto si jambo jema

“Wanasayansi wamefanya kazi yao kwa kutafiti juu ya madhara yatokanayo na mtoto kuangalia tv kwa muda mrefu awapo chumbani kwake sasa ni jukumu la mzazi kuwa makini,”anasema.