UCHAMBUZI: Tuboreshe tiba asili kuelekea uchumi wa viwanda

Friday January 18 2019

 

By Marko Higi

Nilipokuwa likizo ya mwisho wa mwaka kijijini, nilishuhudia mama mmoja katika nyumba jirani akihangaika kutafuta dawa ya kumtibu mtoto wake aliyekuwa amepata homa saa chache zilizopita.

Kwa kuwa ugonjwa hauna hodi, mama huyo alikuwa hana mbele wala nyuma kuhusu matibabu ya mwanaye, hivyo aliamua kumtaarifu bibi wa mtoto huyo kuhusu ugonjwa huo.

Bibi huyo aliamua kwenda porini kutafuta dawa, kisha akarejea na mizizi kadhaa ambayo ilichemshwa halafu akapewa mtoto anywe.

Baada ya siku mbili tangu mtoto huyo anywe dawa hizo za mizizi iliyochemshwa, alianza kucheza na wenzake bila kupelekwa kituo cha kutolea huduma za afya kwa matibabu.

Hakika tiba asili zimekuwa zimekuwa zikitumika miaka mingi iliyopita kabla ya maendeleo makubwa ya huduma za afya za kisasa.

Ni ukweli usiopingika kuwa, wengi wetu tumetumia dawa za asili katika maisha yetu na hii inadhihirika kutokana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (Who), kuonyesha kuwa takriban asilimia 60 ya Watanzania wanatumia tiba asili kabla ya kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 54.2.

Katika kitabu cha mafunzo ya kujiendeleza waganga wa tiba asili kilichotolewa hivi karibuni na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kinaeleza tiba za asili ni jumla ya maarifa na utendaji ambao unafaa au haufai.

Pia, kinaeleza kukinga na kuponya ugonjwa wa kimwili au kiakili kutegemea na uzoefu na uchunguzi unaorithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo au maandishi.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto ilianza kuitambua tiba asili mwaka 1969.

Mganga mkuu wa Serikali wakati huo aliagiza maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuchunguza dawa zote za tiba za asili hapa nchini kama zinafaa au la.

Serikali imefanya maendeleo kadhaa mpaka sasa kuhusu tiba asili.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo nchi ya kwanza yenye chombo cha sheria kilichoundwa mwaka 2005 kupitia sheria namba 23 ya 2002 ya tiba asili na tiba mbadala.

Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lina kazi ya kusimamia, kuratibu na kuendeleza tiba asili nchini.

Tiba za asili zina mchango mkubwa katika sekta ya afya nchini na zinapatikana kwa urahisi zaidi, ambapo Tanzania inakadiriwa kuwa na takriban waganga 75,000 wanaotoa huduma za tiba za asili hapa nchini.

Pia, Tanzania imebarikiwa kuwa na mitidawa zaidi ya 12,000 inayoweza kutumiwa katika kutengeneza dawa mbalimbali za kutibu magonjwa ambayo yanagharimu maisha ya Watanzania.

Katika tasnia hii ya tiba asili, viwanda vidogovidogo vya kiasili vya kutengeneza dawa vimekuwa vikitumika kuandaa dawa ambazo zipo katika mfumo wa unga au maji.

Pia, njia mbalimbali zimekuwa zikitumika kuvuna na kutengeneza dawa ambazo ni za kiasili kwa lengo la kuleta ubora wa dawa husika.

Kutokana na mkazo huo, pamoja na nia madhubuti ya Serikali katika kuendeleza uchumi wa viwanda bila shaka ni wakati muafaka wa kuongeza thamani ya viwanda vidogo vya dawa za asili ili kufikia uchumi wa viwanda vya kati au juu pamoja na kuongeza uzalishaji wa dawa za asili.

Pia, ni wakati wa kuhakikisha dawa hizo asili zinawekwa katika hali nzuri ili zisiharibike mapema na zipate masoko ndani na nje ya nchi.

Taasisi na vyombo husika pamoja na wadau wa tiba asili hawana budi kuungana kuhakikisha eneo la tiba za asili linakuwa mkombozi wa mwananchi kwa kutoa ajira katika sekta za kilimo, viwanda, biashara, usafirishaji na utalii.

Pamoja na kueleza hayo, nawatakiwa mwaka mpya wenye heri na fanaka ili tuendeleze mikakati ya kuboresha tiba asili hapa nchini

Mwandishi wa makala hii ni daktari wa magonjwa ya binadamu, anapatikana kwa barua pepe; [email protected] na simu namba +255 788 668 490