UCHAMBUZI: Tujiandae kuchambua pumba, mchele

Naandika makala haya nikiwa na matumaini kwamba wapo watakaonielewa na kuzingatia ninayoeleza na wapo watakaonibeza kutokana na kile wanachokiamini au masilahi yao binafsi.

Nitautaka ushindi wa wananchi dhidi ya maneno na ahadi hewa. Nitafurahia kama wananchi watasimama wao kama wao. Nitafarijika sana kama wataamua kutumia sawasawa haki yao ya kikatiba.

Ni wakati wa kuanza kutambua mchele na pumba. Ndiyo, lazima ujue pumba ni pumba na mchele ni mchele. Usije kuambiwa ni usiku kumbe ni mchana nawe ukaamini ni usiku.

Si wakati wa kukubali kuambiwa pale kuna shimo utaanguka nawe ukakubali wakati una uwezo mzuri wa kuona kuwa ile ni nyekundu na ile ni nyeupe. Ni wakati wa kuamua maisha ya miaka mitano ijayo iweje.

Huu ni mwaka wa uchaguzi. Ni mwaka ambao wananchi watapata fursa ya kuchagua rais, wabunge na madiwani ambao watatuongoza kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Oktoba mwaka huu.

Kuna sura mpya zitafika kwenye maeneo yetu kunadi sera na kila aina ya maneno ili tuwape fursa ya kutuongoza. Kuna sura za zamani yaani wale walioanza kuongoza kata au majimbo tangu mwaka 2000 au zaidi nao watarejea.

Ndiyo maana nasema ni wakati wa kuchambua pumba na mchele na kila kimoja kikae sehemu yake na kuupata mchele msafi kabisa.

Kwa wale viongozi wanaomaliza muda wao, licha ya kujinadi kwa wananchi kuwaomba wawachague tena watapaswa kuwaeleza je, zile ahadi walizotoa mwaka 2015 wamezitekelezaje?

Kama aliahidi ina maana alipaswa kutekeleza. Hahitaji kwenda kutoa porojo kwa wananchi, anapaswa kutoa sababu zinazojitosheleza kujua hasa kwa nini alichoahidi hajatekeleza lakini kuwaeleza wananchi kipi amekifanya katika miaka yake mitano.

Lakini kwa vyama vya siasa, nanyi mnapaswa kuteua watu ambao wanakubalika. Teueni wagombea kwa matakwa ya wanachama wenu. Si mtu A anakubalika lakini kwa kuwa tu hana fedha au mizengwe anakatwa.

Hii ya kukata majina ya wanachama wanaokubalika ndio sababu tumekuwa tukishuhudia baadhi ya maeneo baadhi ya wanaoshindwa si kwamba amemshinda mpinzani wake kwelikweli bali mizengwe ya upande mwingine au mpasuko kwa chama pinzani umesabisha kupoteza ubunge au udiwani.

Hili limekuwa likijitokeza katika maeneo mbalimbali na hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka jana ulikuwa hivyo.

Hii ina maana kwamba vyama vinapaswa kuwarahisishia wapiga kura, wasikubali kupitisha mtu kwenda kugombea wakati wakijua kuna shida dhidi yake iwe ya kutokukubalika, kutokuwa mtekelezaji wa yale anayowaahidi hali inayowapa wakati mgumu kumnadi kwa wananchi.

Lakini unaweza kujiuliza kuwa uchaguzi huwa na mambo mengi, kuna yale yanayofanyika mchana na yanayofanyika usiku. Lakini wewe mpigakura unahakikisha unatumia vyema nafasi yako bila kununuliwa? Au unakubali kununuliwa ili uweze kumpigia kura mtu? Kwa nini unakubali kuuza utu wako? Huyo anayekununua ana malengo gani na wewe? Baada ya kukununua na wewe ukanunulika unajua anajilipa vipi?

Kama umekubali kununulika utakuwa na uwezo wa kumuuliza kwa nini umeshindwa kukitekeleza hiki na kile? Ikiwa aliyekupa fedha akikuuliza ulipokea zawadi yangu na nafasi ipi, utamjibu nini?

Je, kama unakubali kurubuniwa kwa senti kidogo utawezaje kudai maendeleo kwenye eneo lako iwapo wewe umeshindwa kutumia uwezo wako kumchagua mtu anayestahili hadi upewe chochote?

Wewe binafsi huwezi kujipikia chakula kizuri na kukila hadi upikiwe? Huwezi kuchambua mchele na kuondoa chuya na kuubakisha safi hadi usaidiwe?

Kuna wakati udhaifu wetu wa kukubali vitu vidogo vidongo ndio unatuwa chanzo cha kutufanya tusipige hatua. Hii ina maana kama utamchangua mtu bila kushinikizwa au kununuliwa utakuwa na uwezo wa kumbana.

Tusipokubali zawadi za ovyo, jamii inayomzunguka mbunge au diwani itaweza kumbana kwelikweli, naye atahakikisha anawatumikiwa ki sawa sawa. Tujiandae vyema kuchagua pumba na mchele ili wakati wa kura tule chakula kilicho safi.

Mwandishi wa Mwananchi anapatikana kwa namba 0716-386 168