Breaking News

UCHAMBUZI: Tujifunze Afrika Kusini kuandaa makongamano ya Kiswahili

Tuesday July 9 2019

By Dk Caesar Jjingo

Wadau wa Kiswahili kutoka nje na ndani Afrika Mashariki, wamepania kufanya msururu wa makongamano ya Kiswahili.

Kwa mujibu wa taarifa zilizosambazwa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii, makongamano hayo yataandaliwa katika mataifa matatu ya Afrika Mashariki, ambayo ni Kenya, Uganda na Tanzania.

Makongamano hayo ni pamoja na kongamano la nne la Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (Chalufakita), litakalofanyika katika Chuo Kikuu cha St. Augustine, Mbeya Tanzania. Mkutano huo wa siku mbili utafanyika kati ya Agosti 2-3 mwaka huu.

Kongamano la pili ni la Chama cha Kiswahili cha Taifa (Chakita), litakalofanyika katika Chuo Kikuu cha Karatina, Kenya, tarehe 8-9 Agosti, 2019. Kongamano hilo ni la 20 na la pili tangu Chakita kuasisiwa mwaka 1998.

Aidha, kuna kongamano la Chama cha Kiswahili cha Afrika Mashariki (Chakama), litakalofanyika katika Chuo Kikuu cha Maasai Mara, Narok, Kenya, kati ya tarehe 7 na 8 Novemba, 2019.

Kongamano la tano la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (Chaukidu), litafanyika katika Chuo Kikuu cha Kyambogo, Uganda, Desemba 13-15 mwaka huu.

Advertisement

Pazia la msururu wa makongamano hayo litateremshwa na kikao cha tatu cha Kongamano la Baraza la Kiswahili la Zanzibar (Bakiza) ambacho, kitafanyika Zanzibar Desemba, 19-20, 2019.

Tathmini inaonyesha kwamba Agosti pekee kutakuwa na makongamano mawili. Vivyo hivyo, Desemba. Ni Novemba tu ambako kutakuwa na kongamano moja la Chakama.

Tathmini ya maeneo ya kiojiografia inabainisha kwamba ndani ya eneo moja (Tanzania), kutakuwa na makongamao mawili: Bakiza na Chalufakita, na mengine mawili yataandaliwa nchini Kenya. Uganda kutakuwa na kongamano moja tu la Chaukidu.

Taswira ninayoichora hapa ni kwamba ni vigumu kujua vigezo ambavyo watayarishaji wa makongamano haya walivitumia hasa ukizingatia kuwa wahudhuriaji wanatarajiwa kuwa ni walewale.

Wataalamu wa Kiswahili Afrika ya Mashariki na Kati si wengi mno kiasi cha kuweza kugawanywa katika makundi mbalimbali, ili kuweza kuhudhuria makongamano yanayofanyika sambamba na sawia katika maeneo tofauti ila yanayokaribiana kijiografia takribani ndani ya muda mmoja.

Isitoshe, wakereketwa wengi wa Kiswahili wanaotarajiwa kuhudhuria vikao hivyo hujifadhili. Kadhalika, mada ndogo zitakazoshugulikiwa kwenye makongamano haya zinakaribiana kwa kiasi kikubwa licha ya kuwa pia na mwingiliano fulani.

Tunashindwa kuelewa vigezo vinavyotumika kuandaa makongamano. Vyama au mabaraza na mashirika mbalimbali huwa na malengo yao mahususi yaliyochangia kuanzishwa kwao.

Tofauti na ilivyo nchini Afrika Kusini, japo vyama vyao vya lugha vina malengo tofauti, ukifika muda wa kuandaa makongamano ya kitaaluma kama tunayoyatarajia mwaka huu kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, viongozi wa vyama hivyo nchini humo huja kwa pamoja ili kutekeleza majukumu yaliyo nje ya vyama vyao binafsi ila yenye uwiano na malengo ya vyama hivyo.

Kwa mfano, mwaka 2016, mwandishi wa makala haya alipata fursa ya kuwasilisha makala katika kongamano la pamoja lililoandaliwa na vyama vitatu tofauti.

Kongamano hili liliandaliwa katika Chuo Kikuu cha Western Cape. Kadhalika, kongamano lao la mwaka 2017, liliandaliwa na vyama vyote vitatu katika Chuo Kikuu cha Rhodes.

Ikiwa jukumu na azma yetu katika siku za usoni ni kukiendeleza Kiswahili, ipo haja ya ‘kujifunza’ kutoka kwa wenzetu wa Afrika ya Kusini. Kwanza, tuandae makongamano ya pamoja hasa iwapo maeneo yetu ya kijiografia yanakaribiana.

Kwa mfano, makongamano ya Bakiza na Chalufakita yangeunganishwa. Ni jukumu la kamati ya maandalizi au waandaji kukubaliana kuhusu vitovu ambavyo vitakuwa rahisi kuwakongamanisha wadau wao. Vilevile kwa kuwa makongamano ya Chakita na Chakama yanatarajiwa kufanyika nchini Kenya, haya nayo yangeunganishwa pia na kamati husika.

Pia, ipo haja ya kutathmini upya wakati mwafaka ambao utawaruhusu wahudhuriaji kuhudhiria makongamano yaliyoandaliwa. Makongamano yawe ya pamoja na yaandaliwe pale vyuo vingi vikiwa likizoni iwe katikati ya mwaka au mwishoni.

Lengo kuu ni kuwapa fursa wahudhuriaji kujiandaa, hasa kifedha ili kuweza kusafiri na kuhudhuria makongamano ya mwaka husika bila kusumbuka.

Dk Caesar Jjingo ni mhadhiri msaidizi wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda. Mawasiliano: [email protected]