UCHAMBUZI: Tunasubiri kilichokwama miaka mingi mkoani Tanga

Muktasari:

  • Lengo la utafiti huo ni kuiwezesha Serikali kutambua kina hicho kitakavyoongezwa na kumsaidia mkandarasi atakayeshinda zabuni ya kuchimba kina kutambua maandalizi ya aina gani au nguvu zipi atumie kukiongeza kutoka mita 3.5 hadi mita 15, ili meli kubwa duniani ziweze kutia nanga.

Ni habari zenye kutia moyo kwamba wataalamu kutoka Kampuni ya Bico Engineering ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha utafiti wa udongo katika kina cha Bandari ya Tanga.

Lengo la utafiti huo ni kuiwezesha Serikali kutambua kina hicho kitakavyoongezwa na kumsaidia mkandarasi atakayeshinda zabuni ya kuchimba kina kutambua maandalizi ya aina gani au nguvu zipi atumie kukiongeza kutoka mita 3.5 hadi mita 15, ili meli kubwa duniani ziweze kutia nanga.

Taarifa hizo zilijulikana wakati wa maonyesho ya sita ya biashara ya Mkoa wa Tanga yaliyofikia tamati wiki iliyopita baada ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuuliza hatua zilizofikiwa.

Meneja wa Bandari ya Tanga, Pervical Salama alisema wameanza mchakato wa upimaji udongo ambao una umuhimu kwa sababu kupitia hatua hiyo itajulikana miamba ya aina gani iliyopo na nguvu gani zitumike kuchimba hadi kufikia kina kinachohitajika.

Kazi hiyo kwa mujibu wa Salama, ilistahili kumalizika Agosti 2018 ili kutoa nafasi ya mchakato wa kumtafuta mkandarasi wa uchimbaji kuanza, lakini dalili zinaonyesha Bico Engineering itamaliza mapema.

Meli zinazopita Bandari ya Tanga kwa sasa zinalazimika kutia nanga umbali wa mita 300 kutoka gatini kutokana na kina chake kuwa kifupi. Ili meli kubwa zaidi zitie nanga kinahitajika kina cha kuanzia mita tisa.

Kutokana na kina cha sasa, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) hulazimika kusomba shehena kutoka melini kwa kutumia matishari hadi bandarini, jambo ambalo Rais Magufuli alisema hataki kulisikia.

Agosti 5, 2017, Rais akiwa na mwenzake wa Uganda, Yoweri Museveni alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko kuhakikisha anachimba kina hicho ili meli za ukubwa wowote ziweze kutia nanga.

Rais alikwenda mbali akisema kina hicho kichimbwe kwa gharama yoyote ile ili kurahisisha shughuli za uwekezaji mkubwa ambao unatarajiwa kufanywa katika Mkoa wa Tanga, pamoja na kuhudumia shehena za nchi za maziwa makuu.

Kauli hiyo ya Rais ilianza kutiliwa shaka palepale uwanjani kabla hata hajaondoka na baadhi ya wananchi ambao walisema itashangaza kuutafuna mfupa ambao marais wa awamu zilizopita walishindwa.

Wananchi hao walitilia shaka kauli hiyo kwa sababu kuu mbili; mosi ikiwa ni kutokana na taarifa zilizokuwa zikitolewa wakati wa utawala uliopita kwamba kuchimba kina cha Bandari ya Tanga ni kazi isiyowezekana kwa sababu chini upo mwamba mkubwa ambao si rahisi kuubomoa.

Sababu nyingine zilitokana na vita ya kiuchumi iliyokuwa ikipigwa kuhakikisha bandari hiyo haikui wala kushamiri kwa hofu ya kuhatarisha biashara ya bandari nyingine za jirani.

Kutokana na sababu hizo mbili ikawa kila siku zinatolewa sababu za kudhoofisha Bandari ya Tanga.

Awali ulielezwa kuwapo mkakati wa kujenga bandari nyingine katika eneo la Ndumi jijini Tanga hadi wenye nyumba na mashamba wakatolewa baada ya kulipwa fidia na sasa miaka inayoyoma hakuna kinachoendelea.

Serikali ikaja na wazo jingine la kujenga bandari kubwa katika pwani ya Bahari ya Hindi, eneo la Kigoimbe lakini hilo pia likapingwa kutokana na eneo hilo kuwa katika hifadhi ya wanyama wakubwa adimu duniani aina ya silikanti.

Mambo hayo kwa kweli yaliwakatisha tamaa baadhi ya wananchi wa Tanga wakisema Serikali inafanya njama za kuudhoofisha mkoa wao na kuiinua kiuchumi mikoa mingine.

Lakini, kauli ya Rais Magufuli kwamba anataka kuirejesha Tanga katika historia yake imewapa nguvu wana-Tanga na sasa wanatembea kifua mbele wakiona kwamba amekuwa mkombozi wao kiuchumi.

Haitakuwa mara ya kwanza kwa Bandari ya Tanga kuongoza katika uhudumiaji wa shehena, kwani historia inaonyesha mwaka 1960 ilihudumia tani 212,000 kwa sababu ndiyo bandari iliyokuwa kubwa.

Kimkakati bandari hiyo ni jirani zaidi na rahisi kufikika kwa nchi saba ambazo ni Malawi, Zambia, Congo DRC, Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya, lakini pia kijiografia panafikika kwa urahisi na meli za kutoka nchi nyingi zaidi duniani.

Wakati tukisubiri matokeo ya utafiti huo, tuna hamu ya kutambua kama kweli mwamba huo mkubwa upo au haupo, na kama upo unachimbika au la.

Kubwa zaidi ni kauli ya Rais kwamba anataka kuona meli kubwa zikitia nanga kwa gharama yoyote na hivyo, nasi wakazi wa Tanga tunahitaji kuyaona haya yote yanafanyika sasa na si vinginevyo. 0658-376434