UCHAMBUZI: Tunaweza kushinda kwa kuanza chini kwenda juu

Saturday January 19 2019GASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

Ukitaka kujua kama mkeo unayemtia magumi kila kukicha ni mzuri, mfuate nyumanyuma anapokwenda sokoni. Tazama wanaume anaopishana nao wanavyommezea mate, halafu tazama fungu la kauzu atakalopimiwa ukilinganisha na unavyopimiwa wewe.

Kila kona unayopita watu wanalalama juu ya hali mbaya. Mfagizi wa ofisi anamwambia mchuuzi wa nyanya “bora nyinyi. Sisi tunadanganywa na hizi suti tu, lakini hamna lolote”. Kichekesho ni pale mchuuzi anapoomba wabadilishane kazi...

Watu wanasema ati kabla ya kuja ‘Wazungu’, madini kama dhahabu tulikuwa tukiweka kwenye kombeo na manati kwa ajili ya kupigia tetere. Ati wakaja na makasiki ya kokoto na kutuambia kuwa hizo ndiyo maalumu kwa shughuli ile. Tukazipokea, nao wakazichota hadi kuzichimba.

Kama ni kweli, inathibitisha kuwa chako hakina thamani zaidi ya cha mwenzako. Kama unalala kwenye godoro la pamba hutaona thamani yake hadi Mchina atakapokuja “kukuonea huruma” akubadilishie kwa godoro jipya la sponji. Hatokwambia anakwenda kufanya nini na pamba ile japo ni chakavu.

Mwalimu nyerere aliwahi kutuonya kuwa wajanja wana tabia ya kukandia kizuri chetu, na kutukuza kibovu chao. Anakushikia kipande cha chupa, anakuambia “hii ndiyo dhahabu. Unataka tubadilishane?” Haraka huku udelele ukikuvuja unampa mgodi mzima kwa vipande vya chupa!

Lakini akishazifua “chupa” zako anakufuata tena. Anakuzuga na punguzo la bei (utaijua wapi bei elekezi) iwapo utanunua kwa wingi. Unakenua meno tena na kusahau kuwa ni zile ulizompa mwenyewe. Unachota pesa za chakula na maisha yanaendelea.

Biashara zingine ni ujanja ujanja mwingi tu. Kuna kitu gani ndani ya dhahabu? Chakula au dawa? Mwenzenu jogoo alichakua mchangani akatoka na bonge la almasi. Akalitupa kando na kuendelea na zoezi lake. Hammadi akaibuka na bonge la punje la mtama. Kidume akawa yeye. Ingawa ilikuwa saa tatu za asubuhi, aliwika kwa mbwembwe na kuwaita wapenzi wake kula karamu.

Ati kuna nini ndani ya vitu hivi? Au ndo kama alivyosema Mwalimu kwamba mtu anachukua chuma kwako, anatengeneza bangili, anazichovya kwenye rangi ya fedha kisha anabadilishana nawe kwa shehena ya pamba. Hakomei hapo: akishaichakata pamba hiyo anakushonea suti na kukubadilishia kwa malighafi zingine.

Pengine ndipo tulipoona kweli vyetu si thamani. Mkonge, chai, matunda, wanyama na vingi tu vingine. Tumebaki sasa kuagiza nguo, viatu, nyama ya bifu, juisi ya kopo hadi kamba ya katani. Si vinatoka ng’ambo? Nakumbuka tulipoacha kuku wa kiasili na kupapatikia kuku wa “kizungu”, wakati wenzetu wakipandisha kuku wetu kwao. Tukaanza kuagiza minofu iliyosindikwa kwenye makopo. Jamani! Kichaa ale kwenye kopo, hata mimi nimuige?

Niliwahi kusimulia juu ya dada yetu mmoja aliyekuwa nyuma ya dada wa kizungu katika Mtaa wa Azikiwe hadi barabara ya Upanga. Mbele ya kituo cha YMCA kulikuwa na vibanda vingi vilivyouza hereni na makembe ya dhahabu na yale yaliyotokana na vifuu vya nazi.

Mzungu alisimama mbele ya kibanda kimoja huku dada yetu akisimama kwenye duka la pili yake. Dada akavutiwa na rangi ya dhahabu: “hii ni orijino au ya kuchovya?” Lilikuwa ndilo swali lake kuu wakati akigeuzageuza bidhaa. Akaonekana kuchagua kembe la dhahabu ya kuchovya.

Yule mzungu baada ya kujulishwa bei, akachukua vile vilivyotengenezwa kwa vifuu. Baada ya kuona vile, ghafla dada alighairi naye kuchukua bidhaa za vifuu. Bila shaka hakujua kitu alichohitaji, bali alijipa moyo kuwa alichopenda mzungu ni lazima kiwe bora.

Wakati mwingine ni ile tabia yetu ya kucheka kama wavuta ganja wa kijiweni. Wa kwanza anapiga stori hadi mwisho, watu wanauchuna. Mwingine akianza kwa kusema “siku moja nilikuwa mjini” basi watu watacheka mpaka kugalagala. Kumbe wanacheka ile stori ya kwanza!

Hatufikirii mara mbili mtu anapochukua vyura wa Kihansi. Lakini akishakaa nao mwaka mmoja ndipo tunainuka na kulaani kwa nguvu zote. Naye haraka anaturudishia. Tunabaki kujigamba kuwa tumemuweza, lakini kumbe keshapandisha na kupata mbegu ya vyura hao.

Ile sifa ya kuwa nchi pekee yenye vyura hao inafutika. Wenye shida ya kuwaona au hata kuwanunua wanaenda huko, si kuja huku tena. Hamshangai mtu anafikia kumpinda twiga shingo lake na kumtia kwenye ndege? Kama angetaka supu yake si angemchinja na kumkatakata hukuhuku? Sasa unaambiwa huko ughaibuni kuna “zoo” hata mbuga zetu zikasome. Usicheze na misitu kama Amazon.

Leo tumekuwa watu wa kukodi Faru Fausta, sijui faru John...

Wakati huu tunapoelekea Tanzania ya viwanda ni lazima tuwe makini sana na malighafi. Watu wakumbushwe kuwa baada ya kutoa tui, machicha ya nazi bado yana kazi ya kutoa mafuta ya kupaka. Kifuu kitatengenezwa urembo, katika shina tutapata mbao huku makuti yakifanywa kuwa paa katika kumbi za starehe. Sisi tuna tatizo kubwa ni kujiandaa kushindwa. Kujiandaa huko ni kuandaa Tanzania ya viwanda bila kutayarisha mazingira ya viwanda hivyo. Utashtuka siku moja viwanda kemkem vimetapakaa hadi uani kwako, lakini unahitaji mtaalamu wa kuchagua malighafi.

Tunaweza kuandaa ushindi kwa kuanza chini kwenda juu. Basi tuanze na SIDO.