Tuondoe vikwazo Uwanja wa Ndege wa Songwe

Muktasari:

  • Julai 25, 2018, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi alitoa taarifa mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipoutembelea alisema ujenzi ulikuwa ukifanyika polepole kutokana na mkandarasi kudai hana fedha licha ya kulipwa kiasi chote.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Songwe uliopo mkoani Mbeya hivi sasa unatumika, lakini ujenzi wake umekuwa na changamoto nyingi. Ujenzi wake ulianza miaka ya 2000, lakini hadi leo bado haujakamilika.

Julai 25, 2018, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi alitoa taarifa mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipoutembelea alisema ujenzi ulikuwa ukifanyika polepole kutokana na mkandarasi kudai hana fedha licha ya kulipwa kiasi chote.

Alitaja changamoto nyingine kwenye uwanja huo kuwa ni mkandarasi kushindwa kuwasilisha vifaa vingi muhimu kama kamera za CCTV, lifti na vinginevyo.

Pia, alisema changamoto nyingine ni kuharibika kwa tabaka la juu la barabara ya kurukia na kutua ndege ambalo lilijengwa katika awamu ya tatu.

Bila shaka changamoto zote za uwanja huo zina sababu zake, lakini Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wa sasa, Albert Chalamila hivi karibuni alitamka wazi kwamba Serikali haina simile.

Chalamila alisema baadhi ya maofisa walioaminiwa katika mradi wa kujenga uwanja huo walitafuna fedha na kusababisha mradi kuchelewa hadi sasa.

Akiwa kwenye furaha ya kuipokea kwa mara ya kwanza ndege mpya ya ATCL aina ya Air Bus A220-300 Dodoma iliyotua uwanjani hapo, Chalamila alisema Serikali ya awamu ya tano imeamua kutoa fedha nyingine Sh18 bilioni ili kukamilisha uwanja huo.

Kauli hiyo imekoga mioyo ya wapenda maendeleo ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Tanzania kwa jumla kutokana na ukweli kwamba yaliyopita si ndwele sasa tugange yajayo.

Kitendo cha Serikali kutoa fedha nyingine kinaonyesha wazi kwamba imedhamiria kuboresha huduma za usafiri wa anga nchini.

Hata hivyo, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) nayo haina budi kuunga mkono juhudi za Serikali, kwa kujibu hoja inazolalamikiwa utokana na urasimu unaodaiwa kufanywa na mamlaka hiyo.

Kwa mfano, Septemba mwaka jana, baadhi ya wafanyabiashara waliilalamikia TAA kwamba haitoi ushirikiano kwa wawekezaji wanaotaka kujenga majengo maalumu ya kuhifadhi mbogamboga, maua na matunda katika uwanja huo.

Baada ya kuyasikia malalamiko hayo, mwandishi wa uchambuzi huu aliwasiliana na Meneja Uhusiano wa TAA, Bahati Mollel ambaye alishauri yaandikwe maswali na yatumwe kwa kupitia barua pepe.

Ushauri wa meneja huo ulitekelezwa Oktoba 3, mwaka jana kwa kutuma maswali manne yakiwamo ya kutaka kujua sababu za kutokamilika kwa ujenzi wa uwanja huo na malalamiko ya wafanyabiashara.

Oktoba 15 baada ya kuona ukimya alipigiwa simu Mollel ambaye alisema aliyaona maswali na kuyafikisha kwa viongozi wakuu ili wayajibu.

Pamoja na kuwapo kwa simu nyingi za kukumbushia kupitia kwa meneja huyo, ukweli ni kwamba hadi hivi sasa maswali hayo hayajajibiwa.

Kwa uzito huo wa kutojibu maswali, TAA imekuwa sehemu ya vikwazo vya kukamilika kwa uwanja huo.

Hivyo kwa ushauri tu, viongozi wa TAA hawana budi kutambua wazi kwamba Uwanja wa ndege Songwe ni mpya na unaweza kuhudumia nchi nyingi za Kusini mwa Afrika, hivyo unahitaji uboreshaji mwingi.

Hata changamoto ya kubadilisha jina la uwanja huo na kuwa Mbeya International Airport inaweza kutatuliwa hata leo, lakini kusiwe na urasimu wa taasisi yoyote ikiwamo TAA kukwamisha ubadilishaji huo.

Ni jukumu la TAA kuondoa utata huo ili kwenda sambamba na juhudi za Serikali za kuimarisha usafiri wa anga badala ya kukaa kimya.

Hali kadhalika ipo haja kwa TAA kushauriana na Mkoa wa Songwe nao utafute eneo la Kiwanja cha ndege sasa ili kuongeza wigo wa usafiri wa anga.

Tunajivunia kuwa katika zama mpya za utendaji wenye ufanisi kwa vyombo mbalimbali vya Serikali.

Kama ilivyo kwa watendaji wa juu wanaoonyesha dhamira ya dhati ya kutaka kuiendeleza Tanzania katika kila nyanja, ni wajibu pia wa wale wanaosimamia vyombo vya kiserikali , kuendana na maono na kasi ya viongozi wa juu.

Huku ndiko kwenda sambamba na kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ Nisisitize wito wangu wa TAA kufanyia kazi changamoto zilizotajwa.

Lauden Mwambona ni mdau wa maendeleo anayeishi mkoani Mbeya. 0767 338897