Tuongeze juhudi na kuotesha miti ya asili

Dk Felician Kilahama

Muktasari:

  • Kabla na baada ya kupata Uhuru mwaka 1961, hali na afya ya misitu ya asili (forest health) ilikuwa nzuri sana. Kwa upande mwingine hata tangu kuwa chini ya utawala wa Wakoloni (Wajerumani 1891) na Waingereza baada ya vita ya kwanza ya Dunia hatujawahi kuwa na takwimu kamili zinazoonyesha eneo kamili la misitu ya asili nchini ni kiasi gani.

Kabla ya utawala wa Waingereza, eneo la Afrika Mashariki, ikiwemo maeneo ya Burundi, Rwanda, Tanzania Bara na Buganda; kuanzia 1885 hadi 1919 yalikuwa chini ya utawala wa Wajerumani na kujulikana kama “Deutsch-Ostafrica”.

Wakati wa vita ya kwanza ya Dunia (kuanzia 1914), majeshi ya Waingereza ikiwa ni pamoja na wanajeshi wa majini wa ardhini kutoka Waingereza na India yalipambana na Wajerumani na kuwazidi nguvu hivyo mwaka 1916 Waingereza wakaanza kukalia ardhi yetu na waliendelea kuwepo hadi vita ya kwanza ya Dunia ilipomalizika 1918. Baada ya vita hiyo kwisha, kukaundwa chombo kidunia kilichoitwa: “The League of Nations” ikiwa ni jitihada ya kutafuta amani duniani.

Kupitia chombo hicho Waingereza walikabidhiwa madaraka ya kusimamia eneo la Tanzania Bara. Ilipofika mwaka 1922 (mwaka aliozaliwa marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa); Waingereza wakaanza kusimamia rasmi lakini wakifahamika kama waangalizi na ndipo jina la Tanganyika likaanzishwa.

Kabla na baada ya kupata Uhuru mwaka 1961, hali na afya ya misitu ya asili (forest health) ilikuwa nzuri sana. Kwa upande mwingine hata tangu kuwa chini ya utawala wa Wakoloni (Wajerumani 1891) na Waingereza baada ya vita ya kwanza ya Dunia hatujawahi kuwa na takwimu kamili zinazoonyesha eneo kamili la misitu ya asili nchini ni kiasi gani.

Kwa mfano, kwa miaka ya nyuma imekisiwa kuwa eneo la misitu nchini ni kati ya asilimia 34 na 48 ya ardhi nzima ya Tanzania Bara na asilimia 90 ikiwa ni misitu aina ya Miombo. Vilevile, asilimia 37 ni eneo lenye misitu iliyohifadhiwa Kisheria.

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2015 zinaonyesha kuwa eneo lenye misitu ya asili na mashamba ya miti ni jumla ya hekta 48.1 milioni (zaidi ya asilimia 50 ya eneo lote).

Pamoja na kuonekana kuwa Tanzania tunayo misitu ya kutosha lakini matumizi yake yamekuwa siyo endelevu. Miti mingi imekuwa ikikatwa sana hasa kwa kupata mbao, nguzo na mkaa.

Wengi wetu tukiona msitu kinachotujia akilini ni miti gani inafaa kwa mbao. Hata wataalamu wa misitu mafunzo yetu yalielekea zaidi kusimamia misitu kwa minajili ya kuzalisha mbao kupitia viwanda vya kuchakata magogo.

Hivyo mkazo ulielekezwa zaidi kwenye mashamba ya miti na sanasana miti ya kigeni (Pines, Cyprus na Mikaratusi). Wataalam tukapikwa zaidi kushughulikia mashamba ya miti kwa kutupatia utaalam wa kutosha tangu mbegu, kupanda miti, kuitunza hadi inapofikia umri wa kuvunwa.

Kutokana na hali hiyo misitu ya asili ilionekana kutopewa umuhimu wa kutosha na hali hii imekuwa hivyo tangu ukoloni mpaka leo bado mtazamo ni uleule.

Wakati wa ukoloni Wajerumani na Waingereza walihifadhi baadhi ya maeneo ya misitu Kisheria. Lakini mkazo wao uliwekwa zaidi kuanzisha mashamba ya miti kwa misingi ya kupata miti inayofanana na rahisi kutunza ili kupata mbao nyingi kwa wakati mmoja na kuingiza fedha nyingi kupitia viwanda vya misitu.

Misitu ya hifadhi ilianzishwa lakini haikupewa kipaumbele kiutunzaji na kuwepo usimamizi wa kutosha kama ilivyokuwa kwa mashamba ya miti. Ndiyo tukawa na maeneo mengi ya misitu ya hifadhi kwa unadharia zaidi kuliko kivitendo.

Wakati tukikazania kuimarisha mashamba ya miti, uvunaji wa miti ya asili uliendelea kwa kasi sana na kwa kuwa hatukuwa makini katika kusimamia hali imekuja kuwa mbaya sana.

Aina za miti iliyokuwa maarufu kwa mbao hapa nchini na nchi za nje kama Mivule, Mininga, Mipingo, Mipangapanga, baadhi ya Miombo ikavumwa sana. Sasa hali ni mbaya na tangu uhuru hatukuwa na mkakati wa kuanzisha mashamba ya miti ya asili pengine hali ingekuwa tofauti.

Sasa aina za miti ya asili yenye manufaa kwa binadamu na utunzaji wa mazingira hapa nchi imo hatarini kutoweka. Hata hivyo hali haijawa mbaya kiasi cha kutukatisha tamaa. Bado tunayo nafasi ya kuirejesha miti ya asili kwenye uhalisia wake. Tutaweza kufanya kweli kupitia mbinu za kitaalam na kisayansi kutokana na matokeo ya tafiti kwenye misitu ya asili na kutoa matokeo chanya.

Sasa ni wakati muafaka kuweka nguvu kwenye mitiasili. Hebu tuanze na aina zenye faida nyingi kiuchumi. Mfano, pamoja na ile ya mbao kuna miti kama Misandali (sandalwood – Oryris lanceolata) inatumika viwandani kutengeneza manukato na dawa; Mikimbo (Allanblakia stulmanii) ilikuwa inapatikana sana sehemu za Lushoto.

Kuna miti aina ya Amarura (Sclerocarya birrea) inafaa sana Kibiashara na matunda yake chanzo kizuri cha vitamini C na dawa pia. Miti kama hiyo inaweza kuchangia uchumi wa viwanda Tanzania tiwekee mkakati mzuri wa kuiendeleza kwa manufaa yetu wote. Nawapongeza Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) maana wameanza kulifanyia kazi suala hili muhimu kwa kuanzisha mashamba ya miti ya asili.

Taasisi ya Utafiti wa Misitu nchini (TAFORI) iwezeshwe na TFS pamoja na wadau wengine kwenye tasnia ya misitu na kwa kufanya hivyo tutaweza kufanikisha na kusonga mbele ipasavyo. Hakuna lisilowezeka penye nia pana njia.