UCHAMBUZI: Tupambane dhidi ya genge hili la waandishi wabovu

Muktasari:

  • Chanzo cha vita ya Kagera ni uvamizi na uporaji wa ardhi ya Tanzania uliofanywa na Idi Amin Dada katika Mkoa wa Kagera katika eneo liitwalo Kyaka.

Vita ya Kagera ilipiganwa na Watanzania dhidi ya aliyekuwa rais wa Uganda, Idi Amin na hatimaye Watanzania kuibuka washindi.

Chanzo cha vita ya Kagera ni uvamizi na uporaji wa ardhi ya Tanzania uliofanywa na Idi Amin Dada katika Mkoa wa Kagera katika eneo liitwalo Kyaka.

Kuna sababu nyingi zilizotufanya tushinde vita ile. Miongoni mwa sababu hizo ni uimara wa aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu Mwalimu Julius Nyerere na uwezo wake mkubwa wa ushawishi na kuwatia hamasa Watanzania.

Pia, ubora wa jeshi letu na ukweli kuwa wananchi wa Uganda hawakuukubali uongozi wa Amin.

Pamoja na sababu hizo, kuna siri moja tu ya Watanzania kuibuka ‘kidedea;’ nayo ni umoja na ushirikiano wa Watanzania.

Katika vita ile wananchi karibu wote walipigana. Walichokuwa wanafanya wanajeshi wetu ni kuongoza tu mapambano kwa kuwa wao ndio waliokuwa katika eneo la mstari wa mbele.

Kila Mtanzania alipigana katika vita ile kutegemeana na nafasi aliyokuwa nayo. Kuna matajiri waliochangia fedha; kuna wengine walitoa magari yao kusaidia kusafirisha wanajeshi, vifaa, na chakula.

Wananchi walichangia mifugo yao kama vile ng’ombe, mbuzi kwa ajili ya chakula cha wanajeshi. Kuna waliotoa mazao kwa ajili ya chakula cha wanajeshi.

Baada ya Watanzania kuunganisha nguvu zao na ‘kumfurusha’ Idi Amin kwa masilahi mapana ya taifa letu, sasa ameibuka mvamizi mwingine na pengine ni hatari zaidi kuliko huyu.

Huyu wa sasa anaua elimu yetu. Adui huyu hapa namaanisha waandishi wa vitabu vibovu vinavyotumika katika shule zetu kuanzia elimu ya awali hadi sekondari. Rai yangu Watanzania wote tuungane na kumpiga vita ‘mhalifu’ huyu kwa mtindo uleule tulioutumia wakati wa vita vya Kagera.

Mimi siwatofautishi waandishi hawa wa vitabu vibovu na genge la wahalifu. Naomba tuwapige vita watu hawa kwa nguvu zetu zote. Maadui hawa wanarudisha nyuma juhudi za Serikali katika kuboresha kiwango cha elimu katika nchi yetu.

Serikali imejitahidi kuongeza na kuboresha vyumba vya madarasa, kuongeza idadi ya madawati katika shule zetu, na sasa iko katika mchakato wa malipo ya walimu ikiwa ni pamoja na kupunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo la malimbikizo ya stahiki zao.

Hata hivyo, juhudi zote hizi zinavurugwa na hili ‘genge’ la waandishi bomu wa vitabu Nitoe mfano. Nikiwa mtaalamu wa uhasibu, nashangaa kuona mpaka sasa vitabu vyote vya kiada na ziada vimepotosha maarifa kuhusu mada ya ‘Accounting’ inayofundishwa kama sehemu ya Hisabati kwa ngazi ya kidato cha tatu.

Kukosea ni suala la kawaida, lakini linapokuwa kwa kiwango kikubwa, lazima tukiri kuwa mfumo wa elimu umo hatarini. Unaweza kukosea herufi, mpangilio wa maneno, sarufi, lakini sio kupotosha maarifa kama ilivyo katika vitabu hivi.

Napata mshangao zaidi baada ya kuona kwamba hata baada ya kufanya uamuzi wa kizalendo ya kuiandika upya mada hiyo na kuipeleka katika mamlaka stahiki, wahusika wanapiga chenga na kukataa kuipokea kazi hiyo tangu mwaka 2016.

Kinachoniacha hoi ni kuwa mamlaka imeshakiri kuwa mada hiyo imekosewa mwanzo hadi mwisho. Sasa kigugumizi cha kukataa kazi iliyo bora kinatoka wapi?

Tuunganishe nguvu zetu katika hili, ili kumuunga mkono Rais wetu John Magufuli kwa kuwaokoa watoto wetu waliopo shuleni wasiendelee kupotoshwa na genge hili ovu.