MAONI: Tusiache udhalilishaji kwa watumishi ukaota mizizi

Friday May 10 2019

Umeibuka utamaduni wa baadhi ya viongozi wa Serikali na wanasiasa kuingilia majukumu ya watumishi wa umma.

Katika kutumia vibaya mamlaka waliyonayo, viongozi hao wamefikia hatua ya kuwadhalilisha hadharani watumishi pale wanapofikiri wamefanya makosa ya kiutendaji.

Hili ndilo lililomsukuma Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, kutoa wito akiwataka viongozi wa Serikali kutowadhalilisha wataalamu wa kada ya afya, akisema wanafanya kazi kubwa katika utumishi wa umma.

Akizungumza juzi bungeni, alisema kwa namna wanavyofanya kazi zao katika mazingira ya sasa ya uhaba wa watumishi katika kada hiyo, wataalamu hao wanahitaji kutiwa moyo badala ya kudhalilishwa.

Hata kabla ya Ummy, naye Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, alishawahi kuikemea tabia hii wanasiasa kudhalilisha watumishi wa umma.

Alisema, “sisemi kuwa hakuna watumishi wenye upungufu, la hasha, ninachotaka mimi utaratibu ufuatwe katika kuwaadhibu, si kuwadhalilisha hadharani.”

Jafo alitoa kauli hiyo kufuatia kitendo cha meya wa Jiji la Tanga, Mustapha Seleboss kumkaripia hadharani mwalimu mmoja kwa kile alichodai kuwa alikuwa amechelewa kufika kazini.

Kitendo hicho kilichotokea mapema mwaka huu na video yake kusambaa katika mitandao ya kijamii, kiliugusa umma mpana wa Watanzania huku wengi wakikichukulia kama cha udhalilishaji.

Matukio ya aina hii ni mengi. Mathalani wengi wanaweza kukumbuka tukio la mkuu wa wilaya moja mkoani Kagera aliyeamuru walimu wa shule tatu za msingi kuchapwa bakora kwa madai kuwa hawakuwajibika ipasavyo hivyo shule zao kudorora kitaaluma.

Aprili mwaka huu, tulishuhudia daktari mmoja akivuliwa wadhifa kuongoza kituo kimoja cha afya jijini Arusha kufuatia hatua yake ya kukataa kutii wito wa wajumbe wa kamati ya siasa ya kata wa Chama cha Mapinduzi (CCM) waliomtaka arejee baada ya kumaliza kazi.

Nasi tunaungana na mawaziri hawa kukemea tabia hii ambayo siyo tu inakwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma, lakini bila shaka inachangia kushusha ari ya watendaji. Ni utamaduni tunaopaswa kuupiga vita ili usizoweleke ukawa kama ada katika nchi yetu. Sote hatuna budi kusema hapana kwa tabia hii.

Walimu na wahudumu wa afya ni watumishi wa kada muhimu na nyeti kwa maendeleo ya nchi. Katika mazingira ambayo watumishi hawa wanapitia changamoto mbalimbali za kiutumishi kama vile kuwa wachache, masilahi duni na nyinginezo, haitarajiwi kuona wakiongezewa mzigo zaidi wa machungu wanayoyapitia kila siku.

Tunapojivunia kuwa na Taifa linalofuata utawala wa sheria, ni lazima kila mmoja aheshimu siyo tu sheria za nchi lakini hata taratibu na miongozo mbalimbali tuliyojiwekea katika maeneo mbalimbali ikiwamo utumishi wa umma.

Tunaweza kuwa na watumishi wa umma wasiowajibika na hawa tunakiri kuwa wapo. Hata hivyo, tunapoguswa kwa kutowajibika kwao, bado kila mmoja wetu anapaswa kufuata taratibu ikiwamo kufikisha malalamiko katika mamlaka zinazosimamia nidhamu zao.

Hatuwezi kufika kokote kama Taifa ikiwa kila mtu atatumia mamlaka aliyonayo kwa utashi binafsi kama tuonavyo sasa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao tunaamini tabia hiyo inatokana na wao kulewa madaraka.