MAONI: Tusiruhusu bidhaa zilizotupwa kurejeshwa sokoni

Wednesday January 16 2019

Ripoti maalumu iliyochapishwa jana na leo katika gazeti hili inaonyesha uwepo wa kasi kubwa ya kupelekwa sokoni kwa bidhaa ambazo zinatupwa katika madampo ya Mkoa wa Dar es Salaam, hususan Pugu Kinyamwezi.

Imeelezwa kuwa bidhaa hizo kama za vyakula; tambi, ngano, mchele, maziwa ya unga, mafuta ya kupikia na sukari pamoja na vipodozi, hurejeshwa mjini kuuzwa baada ya kutupwa jalalani. Bidhaa hizo hupakiwa upya kwenye mifuko na kuuzwa tena kwa walaji.

Aidha, uchunguzi wa mwandishi wetu umebaini kwamba biashara hiyo ni kubwa na ina mtandao mkubwa na baadhi wamediriki kuwa na maghala kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa hizo kabla ya kuzirudisha sokoni.

Tunaamini kwamba hata wanaofanya biashara hiyo wanafahamu fika kwamba kutumia bidhaa ambayo muda wake wa matumizi umepita ni hatari kwa afya lakini tamaa ya fedha na kujipa matumaini ya kijinga kwamba haziwezi kudhuru, ndizo zinazowafanya waendelee na jambo hilo baya.

Lakini wakati tukilaani biashara hiyo, tunashangazwa na ukimya wa vyombo vyenye jukumu la kuhakikisha afya za walaji zinalindwa na kuacha bidhaa hizo ambazo ama zimeharibika au muda wa matumizi yake umepita, zikiuzwa holela mitaani.

Mbali ya tishio hilo la kiafya kwa walaji, kuacha biashara hiyo itamalaki ni kuinyima Serikali mapato yatokanayo ni kodi ya bidhaa halisi zilizo madukani kwa kuwa bidhaa zisizo na ubora au ambazo muda wake umeisha zinauzwa kwa bei rahisi kuliko ile ya bidhaa iliyolipiwa kodi halali ikimsubiri mteja.

Hata hivyo, wakati muuzaji wa sukari ya dampo hatakuwa amelipia chochote, yule anayeuza kwa kufuata maadili ya kibiashara atakuwa amelipia kodi. Kwa maana hiyo, kuiacha biashara hii kushamiri ni kuharibu afya za wananchi na kuinyima nchi mapato stahili na kwa sababu hizo, tunazitaka mamlaka zinazohusika kuchukua hatua mara moja dhidi ya watu wanaojihusisha na shughuli hii.

Tunashangazwa na uzembe wa wanaotupa taka dampo hilo la Pugu kutofuata utaratibu wa kisheria wa kuteketeza bidhaa zilizokwisha muda wa matumizi ambao umeainishwa katika Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003. Kifungu namba 6, Kifungu cha 99(1) cha sheria hiyo kinaelekeza kuwa bidhaa yoyote isiyofaa kwa matumizi ya binadamu inatakiwa kuteketezwa kwa gharama ya mwenye mali.

Kama meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Kanda ya Mashariki, Emmanuel Nkilingi alivyokaririwa, sheria hiyo pia inawaelekeza kushirikiana na taasisi nyingine kama Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (Nemc) na manispaa kwa kuwa ndizo zinamiliki madampo na kwamba kiutaratibu, muagizaji wa chakula au bidhaa pindi tu anapogundua muda wake wa matumizi umepita. Alisema sheria humpa nafasi mbili; kwanza, kuiandikia TFDA kuijulisha uwepo wa kiasi fulani cha bidhaa na chenye thamani fulani kilichoisha muda wa matumizi na kuomba utaratibu wa kuziteketeza.

Akishatoa taarifa, TFDA huelezwa utaratibu wa kuharibu kwa mujibu wa sheria, ikiwamo kukagua bidhaa hizo ili kujiridhisha kama taarifa alizotoa ni sahihi na siku ya kuziteketeza inatakiwa wawepo watendaji wa TFDA, manispaa, Nemc, polisi na watu wa dampo ambao ni waajiriwa wa manispaa.

Swali letu ni je, sheria hii inangatiwa na watupaji wa taka katika dampo hilo. Kama ndiyo, kwa nini biashara hii inashamiri? Kama jibu ni hapana, tunahoji, kwa nini haifutwi?