UCHAMBUZI: Tutawapima wanafunzi wa St Francis mwaka 2021

Tuesday February 12 2019

 

Uite kwa kila jina ulitakalo; ufaulu wa kishindo, ufaulu wa ajabu, ufaulu wa kipekee na majina mengineyo kedekede.

Hii ndio Shule ya St Francis, kinara wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne kwa miaka miwili mfululizo yaani kuanzia 2017 hadi 2018.

Aidha, ndani ya miaka minne kuanzia 2015, shule hiyo iliyopo jijini Mbeya imekuwa ikiingia katika orodha ya shule 10 bora kwa miaka yote.

Unapowasikiliza walimu, unapowasikiliza wanafunzi, hukosi kubaini kuwa shule hii ina sifa za kipekee.

Mikakati na mipango yake kitaaluma si ya masihara. Kwa hakika uongozi wa shule, na wanafunzi wenyewe wamejipanga; wanastahiki nafasi hiyo kila mwaka.

Katika ufaulu wa mwaka huu, zaidi ya nusu ya watahiniwa 91 walipata daraja la kwanza kwa alama saba, maarufu kama ‘single digit’. Ni ufaulu wa kushangaza! Matokeo ya kidato cha nne yameshapita, vinara wetu hawa wasichana tumewaona. Hata hivyo, swali langu, je, moto huu wa kidato cha nne watauendeleza hadi kidato cha sita na pengine vyuoni?

Miaka miwili iliyopita, walipokuwa kidato cha pili, watahiniwa wote walipata daraja la kwanza kwa alama saba.

Ufaulu huo wa kipekee ukajiakisi kama ulivyo katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka hivi karibuni.

Nausubiri kwa hamu mwaka 2021. Namuomba Mwenyezi Mungu anipe uhai wa kuwepo na kushuhudia rekodi hii ikilindwa na pengine kuvunjwa.

Kidato cha sita hakuna ufaulu wa alama saba. Kuna alama tatu kama daraja la juu la ufaulu kwa maana ya kuwa na alama A tatu katika masomo ya tahasusi.

Nina hamu na shauku nije kuona daraja la kwanza za alama tatu za wanafunzi hawa wote. Hii itakuwa rekodi ya karne na pengine yenye sifa ya kuingizwa katika kitabu cha maajabu cha Guiness.

Nataka waje kuwadhihirishia watu ambao huku mtaani wanasema sio bure, eti wanamezeshwa kila kitu mpaka maswali ya mitihani.

Wapo wanaodai kuwapo kwa ujanja unaofanyika ili wanafunzi wafaulu. Sijui hawa wana ushahidi gani na kama upo, basi nawasihi wamtoe mwali uwanjani.

Kubwa zaidi ni wale wanaotoa changamoto kuwa wanasubiri waje kuona ufaulu wao wakiwa vyuoni.

Kuna madai kuwa vinara wengi wa kidato cha nne, safari yao huishia matokeo yanapotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (Necta).

Eti hawana chao kidato cha sita na chuoni ndio kabisa, ama masomo huwashinda au hufaulu kwa mbinde wakirudia masomo kila mwaka.

Unajua kwa nini wanapata tabu vyuoni? Huko hakuna mwalimu wa kuwamezea kwa kujibu mitihani iliyopita wala hakuna kukariri kilichoandaliwa na walimu.

Ikiwa ni kweli katika shule zetu walimu wanawatafunia watahiniwa kila kitu, huko ni kuwaandalia mazingira magumu ya kujifunza wakiwa kidato cha tano na cha sita na baadaye kwenye elimu ya juu yaani vyuoni.

Inatia wasiwasi pale mhitimu wa kidato cha nne anapofanya vizuri mno kitaaluma, lakini anashindwa kuendeleza moto wake ule wa mafanikio katika madaraja ya juu.

Hawa ndio wanaowapa watu nafasi ya kusema kuwa pengine ufaulu wao wa kidato cha nne una mikono ya wengi, na sio uwezo binafsi wa watahiniwa husika.

Mazingira ya vyuoni ni tofauti mno na yake ya sekondari ambayo mwanafunzi bado anachukuliwa kama mtoto anayepaswa kutazamwa karibu kwa kila kitu. Pengine udhibiti wa nidhamu na maadili ndio unaowasababisha wakiamka wakilala wajali masomo.

Vyuoni mambo haya yote hayapo. Hakuna mtu wa kukushurutisha kusoma, hakuna wa kutazama tabia na nidhamu yako. Usipokuwa makini, utakwenda na maji.

Na hili ndilo linalotokea kwa baadhi ya vinara wa mitihani ya ngazi za chini, wanaposhindwa kufurukuta katika madaraja ya juu.

Ndio maana natamani nije kuwaona vinara wetu hawa mwaka 2021 watakapohitimu kidato cha sita panapo majaaliwa.

Si hawa tu watahiniwa wa St Francis, shauku yangu pia ipo kwa mwanafunzi bora, Hope Mwaibanje. Kama ilivyo kwa dada zake, natamani pia kuja kuona umwamba wake katika matokeo ya kidato cha sita.

Je, ataivunja rekodi yake, ataulinda ufaulu wake au ataangukia pua? Tusubiri nyakati zitanena!

Abeid Poyo ni mhariri wa makala gazeti la Mwananchi