Tuungane kuhimiza chanjo ya saratani kwa wasichana

Friday April 13 2018Lilian Timbuka

Lilian Timbuka 

Uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV Vaccine) iliyozinduliwa wiki hii na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, inafungua matumaini mapya kupitia kwa mabinti wao katika kupambana na ugonjwa huo hatari unaoua maelfu kama siyo mamia ya wanawake karibu kila mwaka nchini. Wataalamu wa afya wanatwambia chanjo hiyo ambayo ni kinga dhidi ya virusi vya HPV, ni salama na imethibitishwa na Shirika la Afya la Kimataifa (WHO) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA). Wanasema inatolewa kwa wasichana wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14 na tayari utafiti unaonyesha, chanjo hii inaleta matokeo chanya pale inapotolewa katika umri huo na hutoa kinga ya muda mrefu.

Hapo mwanzo nimesema ni faraja, kwa sababu takwimu zinaonyesha hadi sasa, saratani ya mlango wa kizazi inachangia vifo vitokanavyo na maradhi ya saratani kwa asilimia 38 kila mwaka nchini.

Tunaona ni kwa namna gani tunavyopoteza nguvu kazi ya Taifa kwa maradhi yanayoweza kutibika na kuyakinga kabla hayajawadhuru walengwa. Imeelezwa pia saratani hiyo ya mlango wa kizazi inachukua asilimia 32.8 ya wagonjwa wote wanaougundulika kuugua saratani nchini kila mwaka. Kwa maana nyingine, saratani ya mlango wa kizazi ndiyo inayoongoza kwa kuua kwa mujibu wa takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI). Hivyo, tukiwa Watanzania, tuna kila sababu ya kuhakikisha tunalinda maisha ya wanawake wa kesho badala ya kuwaacha wakipukutika kupitia maradhi hayo. Kwa sababu kupitia chanjo hiyo, Tanzania inatarajia kuwachanja wasichana 616,734 waliotimiza umri huo. Hivyo huu ni uwekezaji katika uchumi wa Taifa lolote lile duniani linalojali afya za wananchi wake. Na niwakumbushe Watanzania wenzangu kuwa chanjo hiyo inatolewa bure kama anavyosisitiza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.

Shime kwa wazazi na walezi, muwahimize mabinti zenu kwenda kuchanja chanjo hiyo mapema ili waepukane na saratani.

Chanjo hiyo ambayo tayari imeanza kutolewa mkoani Dar es Salaam, itasambaa nchi nzima.

Kama kweli wazazi tunawapenda mabinti zetu, tusiache kuwahimiza kwenda kuchanja badala ya kuanza kuweka mikingamo kama inayotokea kwenye kampeni ya chanjo zingine. Tumeendelea kushuhudia baadhi ya wazazi na walezi nchini, wakiwazuia watoto wao kupata chanjo kadhaa kwa kile kinachaminika ni kutokana na imani potofu. Nikitolea mfano wa chanjo za watoto wa chini ya miaka mitano na zile za kampeni ya kutokomeza mabusha na matende. Kuna baadhi ya watu walidiriki kuwazuia watoto wao shuleni kupata chanjo hizo kwa madai zinaharibu uzazi, jambo ambao si la kweli.

Hivyo, ningependa kuwasisitiza wazazi na walezi, wapelekeni mabinti zenu wakapate chanjo hiyo kusudi muwakinge na ugonjwa huo mapema. Kwa sababu wazazi wanaowajibu wa kuhakikisha wanawasimamia wasichana hao hatua kwa hatua zile zinazoelekezwa na wataalamu wa afya kuwa baada ya miezi sita kwa wale ambao tayari wamechanjwa, warudi kuchanja tena ili kukamilisha dozi.

Siku ya uzinduzi, Waziri Ummy alisema wizara tayari inazo chanjo 600,000 pekee kwa mwaka huu. Lakini wanachangamoto ya kuwafikia wasichana wote nchini ambao idadi yao ni zaidi ya chanjo zilizopo.

Hata hivyo, faraja kubwa ni kuwa, ifikapo 2019 Serikali inatarajia kupata chanjo milioni 3.9 zitakazosaidia kuwachanja wasichana wote wenye umri wa miaka tisa hadi 14, hali ambayo sasa itatufanya Watanzania tuanze kutembea kifua mbele kuwa tumedhibiti maradhi hayo.

Wataalamu wa afya wanasema saratani ya shingo ya kizazi hivi sasa inakua kwa kasi ya asilimia 36 kati ya zile zinazoshambulia hivi sasa na wanawake wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi (HIV) ndiyo wanaathirika zaidi wakiwa na umri mdogo.

0713-235309

Takwimu za ORCI zinasema kati ya wanawake 100 wanaougua saratani 60 ni saratani ya shingo ya kizazi na katika kila kinamama 100,000, wagonjwa wapya wanaopatikana ni 39,000. Wakati saratani inayofuatia kuua ni ile ya matiti kwa asilimia 12.

Shime Watanzania tuwahimize mabinti zetu wenye miaka tisa hadi 14, wakapate chanjo hii, kampeni hii isiachwe mikononi mwa Serikali pekee, bali ni ya mimi, wewe na yule.

Lilian Timbuka ni Mhariri wa Jarida la Afya