UCHAMBUZI: Tuwasaidie wakulima kulima kwa tija

Herment Mrema

Mkakati wa kusajiliwa wakulima unaotekelezwa na Serikali ni muhimu katika kupata taarifa za msingi zao za ili waweze kuhudumiwa.

Nafahamu kuwa Serikali inao uwezo wa kuwahudumia wakulima kwa kuweka miundombinu imara, kutengeneza sera, sheria, kanuni na kusimamia utekelezaji wa sera za kilimo kufuatana na mipango yake.

Ukweli kwa mazingira ya kilimo huria, imekuwa ni tatizo sana kuwa na taarifa za kutosha kwa Serikali za kuiwezesha kupanga mipango ya uhakika ya kilimo, kiuchumi na huduma kwa wakulima na watu wake.

Kama ilivyo ada, mkulima huria anafanya analojua bila kutoa taarifa kwa yeyote wakati wa kuvuna na kuuza kufuatana na utaratibu wake ambao hauna taarifa kamili za tanzi data.

Mfumo wa kilimo biashara unawezesha utekelezaji na utaratibu wa ongezeko la thamani unaosimamiwa na wakulima wakishirikiana na wadau wengine.

Vikundi hivi vinatakiwa kuwa kwenye mfumo wa kilimo mseto ambao ni mazao yote ya kilimo yanayolimwa na wakulima, ufugaji, uvuvi na biashara za mazao ya misitu.

Wakulima hawa wanajengewa uwezo wa kulima, kusindika na kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani katika masoko ya wakulima ambayo wanashiriki kupanga bei badala ya kupangiwa bei.

Mkulima ambaye yuko kwenye kilimo mseto atakuwa anauza bidhaa mbalimbali kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi na mazao ya misitu na kipato chake kitakuwa kikubwa kama atauza bidhaa zilizoongezewa thamani kwa bei ambayo mkulima anashiriki kuipanga kwa mwaka mzima.

Katika usajili huo, vikundi vya kilimo biashara ambavyo ni muunganiko wa kaya 20 vitaingizwa kwenye bar code ili bidhaa ambazo zinatokanana kaya moja ziwe zinatambuliwa.

Sababu ya kuwa na namba ambayo inatambulisha kila kaya kwenye mazao yanayozalishwa ni kuwa na uhakika wa bidhaa zinazotokana na kila kaya ili kusiwe na udanganyifu au tatizo la kutambua bidhaa kama inavyojitokeza sasa kwenye korosho.

Namba hizo maalumu zitakuwa zinaunganisha kaya na idadi ya mashamba waliyonayo, ukubwa wa mashamba yao, aina ya mazao ya mkulima anayolima na mategemeo ya kiasi kitakachozalishwa kwa msimu mmoja.

Hii itasaidia sana kujua ukubwa wa uzalishaji na kujua ukubwa wa soko la uhifadhi, la usindikaji, na ukubwa wa soko la walaji ili mazao yatakayozalishwa yaweze kuhifadhiwa kwa uhakika, kusindikwa na kuuzwa kwa masoko ya walaji ya uhakika.

Tunapendekeza kuundwa vikundi vya kaya ili kujenga mfumo wa kaya zinazozungumza lugha moja ya kilimo biashara ili kupata mafanikio.

Vikundi hivi vya kilimo biashara, vinatakiwa kuwa na mipango ya utekelezaji wa biashara ya mazao hasa kuunganishwa na masoko ya vitendea kazi na masoko ya bidhaa watakazouza.

Pia, kuna haja ya kuwa na mikataba ya kisheria kati ya wakulima na wadau mbalimbali ambao watakuwa wanatoa huduma za kibiashara kuanzia mikopo, elimu, ugani, usimamisi, shughuli za utayarishaji mashamba, kuvuna, kusindika na kusambaza bidhaa zenye nembo ya mkulima na zote hizi zinafanywa na wadau kwa niaba ya wakulima.

Ili mikataba hii iwe na tija kwa kila mdau kwa kuongeza uwajibikaji, inatakiwa iwe imesajiliwa wilayani ili itambulike serikalini.

Mikataba ambayo imesajiliwa itakuwa na uwazi mkubwa na itakuwa imetoa taarifa za wadau wote ambao wanashiriki kwenye eneo husika.

Pia, ni vyema Serikali ikatengeneza sera ya kilimo biashara (Agribusiness Policy) yenye mfumo wa mnyororo wa ongezeko la thamani kwa wakulima ambao utalenga kuongeza thamani ya mkulima mwenyewe na wadau wengine kwa kukumbatia kilimo biashara.

Vilevile sera hiyo ilenge kuongeza thamani ya mashamba na shughuli nyingine za kilimo kama uvuvi, ufugaji na mazao ya misitu kwa kuhakikisha kuna matumizi ya pembejeo za uhakika, kama mbolea, dawa, mbegu bora, utaalamu sahihi na vitendea kazi vingine.

Sera hizi nazo zilenge kuongeza thamani ya mazao yaliyozalishwa kwa kuhakikisha mkulima hauzi malighafi badala yake anauza bidhaa zilizoongezewa thamani iwezekanavyo.

Wakulima wakifanya kazi zao na kuwa na uhakika wa kupata faida hata Taifa litafaidika pia.

Mwandishi wa uchambuzi huu ni msomaji wa gazeti hili kutoka Africa Rural Development Support Initiative (Arudesi). Anapatikana kwa simu namba 0715301494