Tuwasaidie wanafunzi wa Irugwa kutimiza ndoto zao

Tuesday February 13 2018

 

Katika Shule ya Sekondari Irugwa iliyopo wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza, ni wasichana wawili tu wanaoishi katika bweni lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 48.

Bweni hilo lilijengwa kwa jitihada za Serikali na wazazi, ili kupunguza adha ya wanafunzi hasa wa kike ambao hulazimika kuvuka ziwa kutoka kisiwa hadi kisiwa kufuata shule.

Aidha, bweni hilo lilijengwa kwa kuzingatia umuhimu wa kuwapa ahueni wanafunzi, ili wapate muda zaidi wa kuzingatia masomo na kuepukana na vishawishi wanapokuwa mbali na mazingira ya shule.

Kwa mujibu wa Mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Malubalo, shule yake inahudumia wanafunzi kutoka visiwa vinne.Visiwa hivyo ni Irugwa, Kurazu, Buruza na Yegoba na hilo linaifanya shule hiyo kuwa na ulazima wa kuwa na bweni.

Ilivyo ni kuwa baadhi ya wazazi wanalitazama suala la kuwalipia wanafunzi wao waishi bwenini ni sawa na kugharimia familia mbili; kumlisha mtoto shule na kuilisha familia iliyopo nyumbani jambo wanaloliona kuwa mzigo mzito kwao.

Mwamko duni wa wazazi kuhusu umuhimu wa wanafunzi kuishi bwenini pamoja na uduni wa kipato cha wazazi, kunawafanya wanafunzi wengi wa shule hiyo kuendelea kukaa na ndugu au kulazimika kupangisha vyumba vya gharama nafuu ili waweze kukaa karibu na shule.

Gharama za kuishi katika bweni hilo ni Sh 450,000 kwa mwaka na zinalipwa ili kugharimia uendeshwaji wake, kwani shule hiyo ni ya kutwa na haipo katika mpango wa kupokea fedha za kugharimia wanafunzi wa bweni kutoka serikalini.

Hatua hii huwalazimisha wanafunzi kulipia gharama za bweni, wakati wakiisubiri Serikali iifanye rasmi kuwa shule ya bweni ili ianze kupokea fedha za uendeshaji.

Wakati tunasubiri uamuzi wa kuifanya Irugwa kuwa shule ya bweni, kama wazazi tujiulize, ni kiasi gani mtoto anaweza kutumia kwa chakula akiwa nyumbani kwa mwaka? Kati ya hizo ni kiasi gani atatumia akiwa shuleni?

Ukigawanya Sh 450,000 anazopaswa kuchangia mzazi kwa mwanafunzi wa Irugwa akikaa bweni kwa siku 365 za mwaka, utapata ni Sh 1,233 kwa siku.

Lakini kwa sababu siku za masomo ni takribani 198 tu ukitoa siku za likizo na siku za mwisho wa juma, ukiigawa Sh 450,000 kwa siku 198 za masomo utapata gharama ya matumizi ya mwanafunzi kwa siku ni Sh 2,272.7 kwa kupata chakula cha asubuhi, mchana na usiku na hapa hatujaweka gharama za matibabu ama gharama nyingine zisizoonekana ambazo wanafunzi hawachangii.

Je, wazazi wa Irugwa wanafahamu hili? Kama kweli tunaona Sh2,272.7 ni gharama, tujiulize tunapata nini kuwaacha watoto wetu katika hatari ya kutofanikisha ndoto zao?

Tunatambua kwamba wapo wazazi wasiomudu gharama za kuwaruhusu watoto wao wakae bwenini kama walivyoeleza watoto na walimu wa Irugwa.

Ndiyo maana uongozi wa shule unatamani kuona shule yao inakuwa ya bweni ili ipate fungu la Serikali kuendesha gharama za kuwalea wanafunzi bwenini.

Lakini ni vyema wazazi wakatafakari kwani wakati haurudi nyuma na watoto wetu wanazidi kukatisha ndoto zao kwa kigezo cha kushindwa kumudu gharama.

Kwa Serikali, ni vyema ikaona umuhimu wa kuifanya Irugwa kuwa shule kamili ya bweni, ili inufaike na fedha za uendeshaji. Lengo hapa liwe kuwanusuru watoto hawa watimize ndoto zao.