UCHAMBUZI: Simba, Azam zijipange vizuri mashindano ya kimataifa

Tuesday June 4 2019

 

Fainali ya Kombe la FA iliyochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Ilulu mjini Lindi imehitimisha rasmi msimu wa mashindano ya mpira wa miguu nchini wa 2018/2019.

Azam FC ya jijini Dar es Salaam ilitwaa ubingwa wa Kombe la FA kwenye fainali hiyo baada ya kuichapa Lipuli ya Iringa kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji raia wa Zambia, Obrey Chirwa.

Ushindi huo dhidi ya Lipuli si tu umeipatia Azam taji na zawadi ya Sh50 milioni, bali pia umeipa tiketi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao wa 2019/2020 na kumaliza ukame wa kukosa kushiriki mashindano ya kimataifa kwa misimu mitatu mfululizo.

Wakati Azam wakisherehekea ubingwa huo na tiketi ya kucheza mashindano ya kimataifa msimu ujao, ikumbukwe kuwa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Tanzania itawakilishwa na Simba ambayo ilitwaa taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/2019.

Tofauti na Azam ambao hawajashiriki mashindano ya kimataifa kwa misimu mitatu mfululizo, Simba wanarudi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa na kumbukumbu tamu ya kufika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo msimu uliopita kabla ya kuondolewa na TP Mazembe kwa kipigo cha jumla cha mabao 4-1.

Kwa maana hiyo, Simba wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao wakiwa na deni ama la kufika hatua za juu zaidi au kufika pale ambako walikomea msimu uliomalizika ambao Esperance ya Tunisia ilitwaa ubingwa.

Advertisement

Kwenye upande wa kiufundi, timu hizi zinapaswa kuimarisha mabenchi yao ya ufundi kwa kuongeza makocha wa daraja la juu ambao watawasaidia makocha wao wakuu katika kufanya tathmini ya mechi zao na zile za wapinzani pamoja kuzisoma timu ambazo wamepangwa kukutana nazo.

Timu yenye benchi pana la ufundi ina nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwa sababu kocha mkuu anakuwa hana idadi kubwa ya majukumu na hivyo anakuwa na nafasi nzuri ya kuandaa programu za kiufundi ambazo ndizo msingi wa mafanikio ya timu yoyote ya soka.

Lakini pia hapo kwenye ufundi ni lazima pia Azam na Simba zihakikishe zinapata wachezaji wa daraja la juu ambao wana ubora na uwezo wa kushindana pamoja na uzoefu wa kucheza mashindano hayo badala ya kusajili wachezaji wa kawaida ambao mwisho wa siku watashindwa kuhimili vishindo vya nyota wa timu nyingine.

Usajili huo wa wachezaji wenye hadhi ya kucheza katika Ligi ya Mabingwa Afrika ama Kombe la Shirikisho hauwezi kukamilika kama wawakilishi hao wa Tanzania watatenga bajeti hafifu kwani soko la wachezaji wenye viwango vya juu barani Afrika limepanda kwa sasa.

Mfano timu ya RS Berkane ya Morocco, hivi karibuni imetumia kiasi kinachokadiriwa kufikia Shilingi 2.5 bilioni kusajili wachezaji wawili wa timu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) ambao ni kiungo Fabrice Luamba Ngoma na mshambuliaji Jean Makusu Mundele.

Hawa ni wachezaji ambao walitoa mchango mkubwa mwaka 2018 kuiwezesha AS Vita kutinga hatua ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini pia walikuwa mhimili wa timu hiyo kutinga kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika.

Wakati Berkane wakitumia kiasi kama hicho cha fedha kunasa wachezaji wawili tu, bajeti ya Simba kwa msimu wa 2018/2019 ilikuwa ni Sh7 bilioni ambazo hizohizo zilipaswa kutumika kwenye usajili, kulipa mishahara na posho pamoja na kugharamia usafiri na huduma nyingine kwa timu.

Maana yake thamani ya wachezaji wawili tu wa AS Vita ni kama nusu ya bajeti nzima ambayo Simba walitumia msimu uliopita kwa sababu mishahara ya wawili hao kwa mwezi ni zaidi ya Sh120 milioni hivyo kama ingeamua kuwasajili, pengine isingeweza kujiendesha.

Soka linaendana na uwekezaji. Huwezi kufanya vizuri kama hauna wachezaji wazuri ambao ili wawapate wanatakiwa wajipange hasa kiuchumi, vinginevyo wataishia kusajili wachezaji wa kuokoteza kwa bei rahisi ambao hawatoweza kuwafikisha popote.

Lakini pia kujipanga kiuchumi hakutoishia kwa kusajili na kulipa mishahara wachezaji bali pia kutoa huduma nzuri na stahiki kwa wachezaji jambo ambalo litajenga hamasa na morali ya kuweza kupigania ushindi.

Simba na Azam zinapaswa kwenda kushindana kwenye mashindano ya kimataifa msimu ujao na si kushiriki kwani kwa kufanya hivyo ubingwa wao hautokuwa na maana.