UCHAMBUZI: Tunahitaji suluhisho la athari za mafuriko

BELLA BIRD

Wakati viongozi wa Serikali na wataalamu wa kiufundi wanapokutana kushiriki mkutano wa tatu wa kila mwaka wa “Understanding Risk Tanzania”, uzoefu unaotokana na mafuriko ya Dar es salaam unasisitiza haja ya kupata suluhisho endelevu kwa ajili ya miji stahimilivu.

Uchumi na miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam huathiriwa sana na mafuriko makubwa ya mara kwa mara, na hali itakuwa mbaya zaidi ikiwa hazitachukuliwa hatua madhubuti kukabiliana na hali hii. Mwezi Mei, 2019, mvua za muda mrefu zilisababisha mafuriko makubwa yaliyolazimisha kaya 1,215 kuhamishwa. Pia barabara na madaraja yaliharibika na nyumba 1,560 kusombwa na maji.

Athari hizi ni mwendelezo wa mafuriko jijini ya mwaka 2009, 2010, 2011, 2014 na 2015. Dar es Salaam pia imekumbwa na mafuriko mara saba kati ya mwaka 2017 na 2018 pekee. Huu ni ukumbusho wa mara kwa mara kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua thabiti kushughulikia athari za mafuriko katika miji yetu. Athari hizo ni katika usafiri, utaratibu wa kawaida wa maisha ya watu mijini kama mahudhurio kazini au shuleni, na kibaya zaidi magonjwa yanayotokana na maji machafu ya mafuriko. Athari za kiafya hudumu miezi mingi baada ya mafuriko kuisha. Bila kuchukua hatua, hatari na athari za kiafya zitaendelea kwa miongo ijayo, hasa kwa kuzingatia kasi ya ukuaji wa miji.

Athari hizo pia ni kikwazo katika juhudi za kupunguza umasikini na ukuaji wa uchumi kitaifa. Utafiti wa Benki ya Dunia wa hivi karibuni unaonyesha ukubwa wa tatizo hilo; watu walio hatarini kuathiriwa na mafuriko wako maeneo mengi, huku asilimia 39 ya wakazi wa Dar es Salaam (watu milioni 2) wameathiriwa moja kwa moja au kwa njia nyingine.

Mafuriko ya Aprili 2018 peke yake yaliathiri kati ya watu 900,000 na milioni 1.7 huku asilimia 47 ya kaya zilizoathirika (sawa na 18% ya watu wote wa jiji) ziliathirika kiafya. Utafiti pia unaonyesha jinsi umaskini unavyochangia uwezekano wa kukabiliwa na mafuriko, kiwango cha upotezaji wa hali ya maisha na mali na ni kwa kiasi gani walioathirika wanaweza kurejea katika hali yao ya kawaida kiuchumi na kijamii. Sasa tunaelewa nani anaathirika na mafuriko, wanapoteza nini na kwa kiwango gani walioathirika wanaweza kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Jedwali la mgawanyo wa vipato, linaonyesha wanaokabiliwa na mafuriko ni maskini na idadi yao ni kubwa; wale wanaopata athari za moja kwa moja, kwa mtu mmoja wana wastani wa matumizi yaliyo chini kwa asilimia 14 kuliko ambao hawajaathirika na pia uhakika wao wa upatikanaji wa chakula ni chini ya wastani.

Somo jingine katika utafiti huu ni kuwa kaya zinazoongozwa na wanawake, ambao mara nyingi hawana zana za kutosha kupambana na maafa, ziko kwenye hatarini zaidi kuathirika.

Kwa matokeo ya utafiti huu katika ngazi ya jiji, mafuriko ya April 2018 yaligharimu kati ya asilimia 2 na 4 ya pato ghafi (GDP) sawa na upotevu kati ya Sh249 bilioni 249 na Sh530 bilioni. Kwa wastani, kaya zilipoteza asilimia 23 ya matumizi yao ya mwaka. Hii ni sawa na matumizi ya siku 84 za mwaka. Hata hivyo, matokeo ya tathmini upande wa utetevu yalikuwa ya kushangaza kidogo. Maskini sana hawakupoteza mali sana, hii ni kwa sababu wana rasilimali chache na hawana uwezo mkubwa wa kufanya ukarabati wa majengo.

Hii haimaanishi maskini si waathirika wakubwa wa mafuriko. Maji kutuama ndani kunaongeza hatari ya kupata kipindupindu na magonjwa ya ngozi. Mafuriko yanapozidi wazazi huhangaikia zaidi kuwatoa watoto kwenye maji. Kwa hiyo, tishio la mafuriko husababisha msongo, uchovu wa mwili na kukosa raha, athari ambazo si rahisi kuzibaini katika tathmini. Isitoshe, maafa yasitazamwe kipekee. Kujirudia kwa mafuriko huwa baadhi ya watu katika hali ya kutarajia wakati wote kukabiliana nayo, hili likichangiwa athari hasi zilizojirundika.

Takwimu zinathibitisha kuwa kuna uhusiano kati ya umaskini na uwezo mdogo wa kurejea katika hali ya kawaida. Upatikanaji fedha husaidia watu kurejea katika hali zao za kawaida baada ya mafuriko, lakini si rahisi kwa maskini kufikia huduma hizo. Hali hii hasa inajionyesha katika kaya ambazo zinaongozwa na wanawake ambao si rahisi kwao kujiwekea akiba kwa kiwango cha asilimia 11.5 na pia si rahisi kwao kuwa na akaunti ya benki kwa asilimia 9 ukilinganisha na kaya zinazoongozwa na wanaume.

Uwekezaji katika kudhibiti mafuriko utasaidia kupunguza umaskini. Uwiano mzuri wa mbinu za utengenezaji wa miundombinu (kuchimba, kupanua na kutengeneza kingo za mifereji, kutengeneza mifereji mipya) pamoja na ubunifu katika matumizi ya njia za asili zinaweza kufanywa pamoja na mipango ya kitaalamu ya matumizi ya ardhi inayozingatia taarifa za hatari zinazotukabili, miongozo ya ujenzi na usimikaji wa mifumo ya utabiri wa hali ya hewa.

Katika kujenga umma wenye uwezo wa kukabiliana na maafa uwekezaji unatakiwa uzingatie pia masuala ya jinsia, ushirikishwaji katika masuala ya kifedha na hifadhi ya jamii.

Mwandishi ni mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia (Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe).

**Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Uingereza (UKAid), na Benki ya Dunia kwa pamoja wameandaa ‘Understanding Risk Tanzania’ - Kongamano kuhusu Stahamala ya miji – kuanzia kesho tarehe 2 - 3 Oktoba, Jumba la Makumbusho – Dar es Salaam.