Vijana wasizipe nafasi dawa za kulevya

Tazania kama zilivyo nchi nyingine bado inakabiliwa na changamoto ya dawa za kulevya.

Dawa hizi huathiri shughuli za ujasiriamali hasa taasisi ndogo za fedha ambazo ni nguzo muhimu ya huduma za fedha kwa wajasiriamali wa chini na kati.

Kama ilivyokuwa maeneo mengine, ujasiriamali na biashara ndogo zinazojumuisha taasisi ndogo za fedha zinaathirika kutokana na lolote linaloendelea kwenye jamii inayojihusisha nayo kila siku kutokana na bidhaa au huduma zake.

Kutokana na ukweli kuwa watumiaji na waathirika wengi wa dawa za kulevya ni vijana wa rika la uzalishaji wenye nguvu za mwili na akili, basi ni vizuri kutambua kuwa dawa hizi zinaharibu rasilimaliwatu ambayo ingeweza kufanyakazi kwenye miradi tofauti na kuchangia kukuza uchumi.

Vijana hawa, kama hawatakuwa wamiliki wa biashara basi wanaweza kufanya shughuli nyingine itakayochangia kuimarisha na kuongeza mnyororo wa thamani ukapata fedha na faida nyingine za kutoa huduma.

Vilevile, taasisi ndogo za fedha zinawahitaji vijana wasomi kwa ajili ya uendeshaji, uongozi na ubunifu utakaofanikisha huduma zenye tija kwa wananchi na kukua kwa ofisi husika.

Dawa hizi zinafanya idadi yao kupungua kwenye soko la ajira hivyo kuwafanya kuwa adimu kusimamia taasisi hizi pendwa hivyo kupunguza na kupoteza nafasi ya kuwa na wataalamu wengi kwenye sekta hii muhimu ya fedha.

Dawa za kulevya zinaua soko la bidhaa na huduma za wajasiriamali na taasisi ndogo za fedha kutokana na ukweli kuwa uwezo wa kununua bidhaa kwa watu wengi utakuwa unapungua kutokana na uwapo wa waathirika ambao hawana nguvu ya kufanya kazi.

Licha ya hivyo, kukosa kipato cha uhakika kutokana na kushindwa kufanya kazi kunawanyima nafasi na uwezo wa kununua bidhaa na huduma za wajasiriamali na watu watakaokuwa wanawalea waathirika hawa kuanzia ngazi ya familia uwezo wao wa kiuchumi utapungua kutokana na gharama za kufanya hivyo.

Kwa sababu gharama za kuwalea vijana hawa ni kubwa kiasi cha kuyumbisha shughuli za wajasiriamali, athari hizo hufika mpaka kwenye taasisi ndogo za fedha ambazo hupata ugumu wa kufanya biashara na kundi la watu wa namna hii kwa sababu kufanya hivyo ni kuhatarisha fedha zao.

Kupungua na kupotea kwa usalama kwenye mazingira ya kufanyia kazi kwa wajasiriamali na taasisi ndogo za fedha, kutokana na kukua kwa kundi la waathirika wa dawa za kulevya hasa wenye kipato cha chini mara nyingi huwafanya wahusika wajiingize kwenye uhalifu wakati mwingine wa kutumia silaha ili kutafuta fedha za kuwawezesha kununua tena dawa hizo.

Ikifikia kwenye hatua hii wajasiriamali wadogo pamoja na mali zao wanakuwa hatarini kuvamiwa na kuporwa au wakati mwingine kupoteza maisha kitu kinachodhoofisha ukuaji wa uchumi.

Suala hili pia huziathiri taasisi ndogo za fedha na kuziweka kwenye hatari ya kuvamiwa na kupoteza mtaji hivyo huleta hasara na kupoteza muelekeo wa watu wengi sana wanaonufaika na huduma zao. Pasipokuwa na amani na utulivu ni ngumu kutengeneza uchumi imara na wenye nguvu.

Kujihusisha na dawa za kulevya ni kosa kisheria hivyo ni vizuri taasisi na ofisi husika zikaendelea kupambana na tatizo hili bila kuchoka kwa ushirikiano na wadau wengine kwa kufuata utaratibu ili kuhakikisha vijana wanaacha kujihusisha nazo na kufikiria kufanya mambo tofauti yenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Tufumbue macho na kuingia kwenye ujasiriamali, kila mtu kwa nafasi yake, ili kuitengeneza Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.

Kufanikisha hilo, pamoja na mahitaji mengine, ubunifu na wepesi wa vijana unahitajika zaidi ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi ili kuondoa umasikini hasa uliokithiri nchini.

Takwimu zinaonyesha kuna takriban masikini milioni 12 nchini wanaoshindwa kukidhi mahitaji yao muhimu kutokana na kutokuwa na kipato cha uhakika.

Hali hiyo inachangiwa na kukosekana kwa ajira hasa kwa vijana. Takwimu zinaonyesha kuna zaidi ya watu milioni 24 wenye umri wa kufanyakazi lakini hawana ajira ya namna yoyote.

Mwenendo uliopo, unabainisha kwamba vijana 800,000 huingia kwenye soko la ajira kila mwaka kutoka taasisi tofauti za elimu.

Licha ya taaluma walizonazo, wapo wanaojiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya hivyo kuondoa matarajio ya jamii inayowazunguka. Serikali, mashirika na asasi za kiraia zinapaswa kuweka mipango itakayosaidia kuwashughulisha vijana kwenye uzalishaji mali.