UCHAMBUZI: Mgogoro wa Yanga kwa masilani ya nani nchini

Filamu ya uchaguzi wa Yanga imefika patamu. Hiyo ndiyo lugha nyepesi unayoweza kusema baada ya mchakato huo kupigwa ‘stop’.

Awali, wanachama wa Yanga walibakiza muda mfupi kabla ya kufanya uchaguzi mdogo jana kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

Uchaguzi huo uliitishwa kujaza nafasi ya mwenyekiti, makamu mwenyekiti na baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji.

Hata hivyo, wakati wanachama wakijiweka tayari kwa uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ally Mchungahela, alitangaza kusitishwa hadi leo atakapotoa taarifa rasmi.

Mchungahela alisema uchaguzi umesitishwa baada ya baadhi ya wanachama kufungua kesi katika Mahakama kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Morogoro.

Muda mfupi kabla ya kutangaza kusitishwa kwa uchaguzi huo, mwenyekiti huyo alikuwa katika kikao cha mwisho kupanga namna shughuli hiyo ikavyofanyika.

Mbali ya Mchungahela, kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk Harrison Mwakyembe, Makamu wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Itakumbukwa kwamba tangu mwanzo, uchaguzi huo uligubikwa na utata mkubwa huku kila upande kwa maana ya Yanga, TFF na Serikali ukivutana kabla ya kufikia mwafaka kwamba ufanyike Januari 13 (jana).

Kitendo cha baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kwenda mahakamani kupinga, kinaonyesha jinsi gani Yanga inavyopitia kipindi kigumu.

Wengi tulitarajia kwamba uchaguzi huo ungerejesha hali ya utulivu ndani ya klabu hiyo ambayo tangu alipojiweka kando aliyekuwa mwenyekiti wake Yusuf Manji, imekumbwa na mtikisiko wa kiuchumi.

Licha ya kufanya vyema katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga inashinda kwa mbinde na kama siyo uvumilivu wa wachezaji na benchi la ufundi timu hiyo ingekuwa inaburuza mkia.

Pongezi kwa Kocha Mwinyi Zahera ambaye ameamua kuibeba Yanga mgongoni kwa kuwajenga kisaikolojia wachezaji sanjari na kutoa fedha zake za mfukoni kuwapa vijana wake kupunguza makali ya maisha.

Kimsingi suluhisho la kudumu ndani ya klabu ilikuwa ni kupata viongozi wapya kwa njia ya uchaguzi ambao naamini wangekuja na mpango mkakati wa muda mfupi, kati na mrefu ili kuipa Yanga mafanikio.

Kitendo cha uchaguzi huo kupigwa ‘stop’ kinatoa taswira kuwa Yanga itaendelea kusota kwa muda mrefu na watakaokuwa wanaumia ni wachezaji na benchi la ufundi ambao wanavuja jasho kuipigania klabu katika mashindano.

Hatua ya Yanga kubakiwa na wajumbe wasiopungua saba huku wawili tu, Hussein Nyika na Samuel Lukumay wakionekana ndiyo wenye nguvu kubwa ya ushawishi kwa wanachama wa klabu hiyo kunaashiria hali inaweza kuwa mbaya zaidi kama uchaguzi huo utaendelea kupigwa danadana.

Idadi kubwa ya wajumbe wa kamati ya utendaji waliobaki ndani ya klabu hiyo hawaonekani wakijituma kwa kingo kinachoridhisha kuiondoa Yanga katika hali iliyonayo sasa zaidi ya kushiriki mikutano ya wanachama au mara chache timu hiyo inapocheza na timu pinzani katika mchezo unaohitaji nguvu kubwa ya pamoja.

Kimsingi hakuna njia ya mkato kurejesha hali ya utulivu ndani ya Yanga zaidi ya kujaza nafasi za uongozi ambazo zipo wazi.

Hata hivyo, uchaguzi huo unapaswa kutawaliwa na busara zaidi kwa kuwa tayari kuna mpasuko mkubwa ndani ya klabu hiyo.

Kuna kundi kubwa la wanachama wenye ushawishi ambao kama busara haitatumika kuwatuliza, hali ya utulivu itakuwa ndoto hata kama utafanyika uchaguzi.

Kwa mfano, mchakato wa uchaguzi ulipotangazwa na kampeni kuanza, wapo baadhi ya wanachama ambao walidai kuwa hawatapiga kura kwa kuwa bado wanamtambua Manji kuwa bado ni mwenyekiti.

Pia wapo wanaowapinga baadhi ya wanachama waliojitokeza kuwania uongozi wakisema hawatoshi kuziba pengo la viongozi waliokuwapo wakitilia shaka kama wataweza kuipa neema klabu hiyo kongwe nchini.

Kwa mzatamo wangu busara inatakiwa kutumika kwa pande zote zinazokinzana ili kuinusuru Yanga ambayo pia ni miongoni mwa klabu kubwa Afrika.

Ushindani wa aina yoyote ile kati ya pande zinazovutana hauwezi kuwa suluhisho la mgogoro wa klabu hiyo na mwisho wake hakuna atakayeibuka mshindi zaidi ya kuwaumiza wavuja jasho ambao ni wachezaji.

Klabu ya Yanga ni kioo katika soka la Tanzania na nje kwa ujumla, hivyo ni vyema viongozi wakatumia busara kuinusuru na mgogoro unaofukuta.