UCHAMBUZI: Mtindo huu wa machinga utazalisha kero zaidi mijini

Desemba 6, 2016 Rais John Magufuli aliruhusu wamachinga waachwe wafanye shughuli zao maeneo ya mijini kama ilivyo kwa wafanyabiashara wengine.

Tangu wakati huo amekuwa akisisitiza kwamba viongozi wasiwabughudhi wamachinga iwapo hawatawaandalia maeneo rafiki ya kuendesha shughuli zao.

Kubwa zaidi Agosti 18, 2018 akiwa wilayani Sengerema, Rais Magufuli aliwaeleza wamachinga kuwa hata wakiweza wakapange bidhaa zao mbele ya ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri au mkuu wa wilaya.

Pamoja na kauli hiyo, Rais amekuwa akiwaeleza watendaji wa mamlaka za miji, majiji na manispaa wawaandalie mazingira bora ya kufanya biashara zao badala ya kuwafukuza na kuwanyang’anya bidhaa zao bila kujua cha kufanya.

Kauli yake ya “sitaki kuona watu hawa mamantilie na wamachinga wakibughudhiwa maana na wao wanatakiwa kupata riziki waandalieni mazingira rafiki yatakayowawezesha kufanya biashara zao, maana hakuna mwenye hati ya miji” imejirudia kila mara.

Awali, mathalani kwa Mkoa wa Mwanza, viongozi walipanga maeneo kwa ajili ya wamachinga kufanya biashara zao, lakini baadaye maeneo hayo yalionekana si rafiki na hakuna miundombinu mizuri kama vyoo, hatua iliyomlazimu Rais kuingilia kati na kuwataka waendelee kubaki mijini.

Sitaki kuamini kwamba kauli ya kiongozi huyu ya kutaka kundi hilo liandaliwe mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao kama haikueleweka vizuri kwa watendaji au ni kukosa ubunifu kwa viongozi hao.

Kipindi fulani tena akiwa jijini Mwanza, Rais Magufuli ilifika hatua akasema kama viongozi wameshindwa kuwaandalia machinga mazingira wanaweza kutenga moja ya barabara za mji huo kwa ajili yao, yote hayo ni kuangalia namna ya kuwaweka pamoja, lakini bado viongozi wetu hawaoni cha kufanya.

Kwa sasa katika miji mikubwa kama Arusha, Dar es Salaam na Mwanza hatua hiyo ya kupanga bidhaa barabarani imeonekana kuwa kero kwa wapita njia maana wametumia kivuli hicho kulazimisha kupanga bidhaa kwenye barabara na kuacha sehemu ndogo ya kupita.

Hali imekuwa mbaya zaidi katika jiji la Mwanza ambapo hivi karibuni Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) umefanya ukarabati na ujenzi wa barabara za katikati ya mji. Hata hivyo barabara hizo zimefungwa kwa kugeuzwa maeneo ya wamachinga.

Watu hawa wamechukua jukumu la kupanga hadi katikati ya barabara hizo kiasi kwamba hata gari linapata wakati mgumu kupita katika barabara hizo hususani za Pamba, Lumumba, Nyerere na Kenyatta.

Pamoja na Rais kutaka waendelee kufanya shughuli zao wakati wakiandaliwa mazingira, pia aliwaonya wasitumie fursa hiyo kupanga bidhaa zao katikati ya barabara.

Tena kwa kiburi hichohicho hata mpita njia akipita na kugusa bidhaa zao hutolewa matusi na kukoromewa vikali, wengine kudiriki kuwapiga baadhi ya watu kwa kukanyaga bidhaa zao.

Kero hiyo si tu kwa watembea kwa miguu pekee maana hata kwa baadhi ya barabara magari yanapata shida kupita kutokana na mpangilio mbovu wa bidhaa hizo.

Mathalani katika jiji la Mwanza, barabara za Kenyatta, Nyerere, Pamba, Stesheni, Miti Mirefu na hazipitiki kwa raha.

Kukosa mpangilio maalumu kimekuwa kichaka pia cha hata wafanyabiashara wa maduka makubwa kuondoa bidhaa zao na kuzipanga nje wakitumia kivuli cha umachinga.

Pengine kauli ya Rais inaweza kuwa mtego kwa watendaji hao, ambapo imedhihirisha ukweli kwamba wengi wao hawana mipango madhubuti ya kukabiliana na kero za wananchi.

Hata hivyo, hakuwaambia wamachinga kwamba wapange bidhaa zao katikati ya barabara lakini wamekuwa wakitumia kauli hiyo vibaya kudiriki kupanga bidhaa hizo katikati ya barabara bila kujali kama pia ni hatari kwa maisha yao.

Wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya wakiongozwa na wakuu wa mikoa husika katika hili hawawezi kukwepa lawama kwamba wameshindwa kulipatia ufumbuzi wa kudumu.

Inashangaza kuona kila jambo wanasubiri kupewa maelekezo na maagizo kutoka juu, ilhali Rais amewaweka ili wamsaidie kuondoa kero za wananchi na kusimamia miradi ya maendeleo.

Hili pia limejidhihirisha pindi Rais, makamu wake Samia Suluhu au Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wanapokuwa kwenye ziara mbalimbali kukutana na mabango lukuki ya wananchi yanayoeleza hisia, kero na masaibu waliyonayo, maana yake watendaji wa ngazi za chini hawashughulikii kero hizo.

Ifike wakati sasa tuamke, tuwajibike na kutambua majukumu yetu bila kuelekezwa na kusukumwa, tuondoe kero hii badala ya kusubiri majanga yakitokea ndipo tunahangaika kukimbizana kutafuta ufumbuzi.

Jesse Mikofu ni mwandishi wa Mwananchi Mwanza anapatikana kwa simu namba 0755996593.