UCHAMBUZI: Stempu za kielektroniki zasaidia kutoza kodi stahiki

Tuesday November 5 2019

 

By Veronica Kazimoto

Moja ya mifumo inayotumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika ukusanyaji wa mapato ni pamoja na stempu za kodi za kielektroniki ambao ni mbadala wa stempu za karatasi za kubandika zilizokuwa zikitumika hapo awali.

Mfumo huu mpya ni maalumu kwa bidhaa zote zinazostahili kutozwa ushuru wa bidhaa na ulianzishwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Juni 2018, lakini ukaanza kutumika rasmi Januari 2019.

Ikumbukwe kwamba, ushuru wa bidhaa hutozwa kwa mujibu wa kifungu cha 124 cha Sheria ya Ushuru wa Bidhaa sura ya 147 inayoainisha aina za bidhaa zinazotozwa ushuru huu kwa mujibu wa jedwali la nne (4) la sheria hii sambamba na marekebisho yanayofanyika kupitia Sheria ya Fedha.

Kufuatia sheria hiyo, kanuni za stempu za kodi zilitungwa ili kuhakikisha kuwa utaratibu wa kutambua kiwango cha uzalishaji na uingizaji wa bidhaa nchini unakuwa ni wa uwazi na unafuatwa kwa lengo la kutoza kodi stahiki.

Kabla ya mfumo huu mpya wa kielektroniki, kulikuwa na mfumo wa stempu za kodi za karatasi ulioanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1998 ambapo stempu hizo zilikuwa zinabandikwa kwenye bidhaa za sigara.

Mwaka 2002 Serikali ilipanua wigo na stempu hizo kwa kubandika kwenye bidhaa za mvinyo na pombe kali.

Advertisement

Mwaka 2013, utaratibu wa kubandika stempu za kodi za ushuru wa bidhaa ulianza kutumika kwenye bidhaa za muziki na filamu yaani CDs/DVDs kwa ajili ya kurasimisha na kulinda kazi za wasanii, ili kuwawezesha kufaidika na kazi zao na kuhakikisha Serikali inapata mapato kutokana na kazi hizo za sanaa.

Lengo la kubandika stempu hizi ilikuwa ni kuweza kugundua bidhaa iliyolipiwa kodi, kupata taarifa sahihi za uzalishaji viwandani ili kukusanya mapato stahiki na pia kuzuia udanganyifu uliokuwa unafanyika katika uingizaji wa bidhaa nchini kwa njia zisizo rasmi.

Hata hivyo, zilijitokeza changamoto nyingi katika matumizi ya stempu za kodi za karatasi kama vile upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali kutokana na udanganyifu katika taarifa za uzalishaji zilizotolewa na wazalishaji pamoja na kuibuka kwa wimbi la wadanganyifu waliotumia udhaifu wa mfumo wa stempu za karatasi na kuiibia Serikali kwa kutengeneza stempu za kughushi.

Changamoto nyingine ni kuwapo kwa bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora na zinazoweza kuathiri afya za binadamu na kwa kutumia mfumo wa stempu za kodi za karatasi, haikuwa rahisi kutambua uhalali wa bidhaa iliyoko sokoni kuwa imetengenezwa na mzalishaji halali wa bidhaa hiyo.

Kutokana na changamoto hizo Serikali iliamua kuanzisha mfumo wa stempu za kodi za kielektroniki ambao kama siyo kupunguza changamoto hizo basi utaziondoa kabisa na mwisho wake utasaidia kuongeza mapato ya Serikali.

Akikagua viwanda ambavyo vimefungiwa mfumo huu wa stempu za kodi za kielektroniki hivi karibuni mkoani Mbeya, kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Dk Edwin Mhede alisema faida za kuanzisha mfumo huu mpya ni kuongeza mapato yanayotokana na ushuru wa bidhaa, kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kodi ya mapato pamoja na kuondoa malalamiko ya kutotendewa haki ya makadirio ya kodi zinazosimamiwa na TRA na kuiwezesha Serikali kutambua mapema kiasi cha ushuru wa bidhaa kitakacholipwa.

Faida nyingine ni pamoja na kuziba mianya ya uingizaji bidhaa kiholela nchini ambazo hazijalipiwa ushuru stahiki na zisizokuwa na viwango vinavyokubalika na kuongeza uhiari wa ulipaji kodi kwa kutengeneza wigo sawa wa ushindani kati ya wazalishaji na waingizaji wa bidhaa zinazopaswa kubandikwa stempu za kodi za kielektroniki.

Mfumo huu wa stempu za kodi za kielektroni ulianza kutekelezwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ilihusisha bidhaa za sigara, mvinyo, pombe kali, bia na aina zote za vileo.

Hadi sasa, jumla ya viwanda 85 vya bidhaa za awamu ya kwanza vinatumia mfumo huu katika uzalishaji wa bidhaa ambapo vya sigara ni vinne, bia (7) na mvinyo na pombe kali (74).

Pia, wapo waingizaji wa bidhaa zinazobandikwa stempu za kodi za kielektroniki wapatao 32 wanaotumia mfumo huu hadi sasa.

Awamu ya pili imehusisha bidhaa za vinywaji baridi, maji, juisi na CD/DVDs ambapo matumizi ya mfumo huu kwa bidhaa za vinywaji, laini yalianza rasmi Agosti, 2019.

Ukitazama tangu kuanza kwa utekelezaji wa mpango huu, Serikali imekuwa ikiingiza kiwango kikubwa cha fedha na matarajio yaliyopo ni fedha hizo kuongezeka mara dufu.

Niunge mkono operesheni inayoendelea nchi nzima ya kukamata na kuondoa sokoni bidhaa ambazo hazijafuata matakwa ya kanuni za stempu za kodi za kielektroniki.

Veronica Kazimoto ni ofisa habari wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

0753986541