UCHOKOZI WA EDO - Mzee Membe anapofurahia “airtime” ya bure kabisa

Wednesday December 5 2018

 

Wanasiasa watu wa ajabu sana. Huwezi kuwaelewa vema. Wakati mwingine wanajiandalia kuzama kwao na wakati mwingine kuibuka kwao. Wakati mwingine wanaandaliwa kuzama au kuibuka kwao.

Jana niliahidi kutomzungumzia mwanasiasa anayeitwa, Benard Membe. Sikutaka kumpa “airtime” jana. Sikutaka kuwa miongoni mwa watu wanaomuibukia kwa kasi kwa sasa. Nilidhani ningesaidia kumuondoa katibu wa chama kile katika mtego alioingia. Mtego wa sisimizi kabisa. Kwa nini Membe aongelewe?

Tangu ulipomalizika uchaguzi mkuu uliopita Membe hajawahi kuongea chochote hadharani. Kama kuna kitu anaongea au kuwa na nia yoyote basi huizungumza na wasiri wake, nao wamejua kuitunza siri sirini na kubaki kuwa siri.

Hata katibu wa chama kile na mabosi wake walipogundua siri hiyo walipaswa nao kushughulika nayo chinichini tu. Kwa nini wameiweka hadharani katika nyakati ambazo watu bado wamegawanyika kihisia jinsi nchi inavyokwenda? Kuna wanaosapoti na wapo wasiosapoti.

Vyovyote ilivyo, ghafla wale wasiosapoti wamepata sauti. Membe ametengenezwa hadharani kuwa mpinzani na mwenyewe itakuwa anafurahia. Alipaswa kuachwa kama alivyo au kushughulikiwa chinichini asipate “airtime”. Sasa hivi atakuwa anatabasamu kila dakika. Jina lake lipo katika kurasa za mbele, katuni za Masoud Kipanya, Twitter na leo kwa mara ya pili lipo katika safu hii.

Hiki ndicho ambacho mwanasiasa kama yeye anakihitaji. Kutajwa sana katika namna ya kuonewa kwa kuwa hajazungumza chochote hadharani kabla ya shutuma dhidi yake kutajwa na watu wawili, mmoja akiwa katibu wa chama. Alipaswa kushughulikiwa kwa baruapepe au kwa kupigiwa simu bila ya wambea wa Twitter na kwingineko kujua.

Katibu ametengeneza tatizo ambalo hakujua linamnufaisha Mzee Membe. Nadhani ndiyo maana baadaye akaanza kubadili kauli zake. Hata hivyo, bado inakuwa faida kwa Membe kwa sababu inamuweka katika chati kama ile ambayo hasimu wake wa zamani, Mzee Edward aliipata katika utawala uliopita alipoanza kushutumiwa mara kwa mara kuhusu kuhujumu utawala uliokuwa madarakani na nia ya kugombea urais.

Ukitaka kumkera mwanasiasa basi usimuongelee. Iwe kwa mazuri au mabaya. Usimuweke katika chati hata kama ni tatizo. Shughulika na tatizo lake kimya kimya tu. Usidhani Mzee Membe amenuna.