MAONI: Udhibiti stika za TRA usiache maswali

Wednesday June 13 2018

 

Mwishoni mwa wiki iliyopita, maofisa wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walikamata chupa tupu za pombe, nembo na vizibo vya chupa za konyagi ambavyo vilikuwa vimeandaliwa kutumika kutengenezea vinywaji bandia.

Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah aliyeongoza operesheni hiyo iliyofanyika katika nyumba ya mkazi mmoja iliyopo eneo la Msaranga mjini Moshi, walifanikiwa kunasa chupa tupu za Highlife 2,400, chupa zisizo na nembo 230, vizibo vya chupa za Konyagi, lita 750 za spiriti na jiko la ‘mchina’ linalotumika kufungasha pombe hizo.

Mbali na malighafi hizo na zingine zilizojazwa pombe, katika nyumba hiyo polisi na maofisa wa TRA walikuta stempu za mamlaka hiyo ambazo hubandikwa katika vileo hivyo kuonyesha uhalali wa malipo ya kodi.

Wakati polisi wakiendelea na uchunguzi kuhusiana na utengenezaji huo haramu wa pombe kali, suala linaloumiza vichwa kwa upande mwingine ni namna watengezaji hao wa pombe walivyofanikiwa kupata stempu na stika za TRA, ilhali kwa mujibu wa maofisa wa mamlaka hiyo, hawatambuliki katika ofisi zao.

Hali hiyo ndiyo inayoibua hoja ya uwepo wa uchunguzi makini ili kujua namna gani hati hizo nyeti na muhimu za kiserikali zinavyoingia mikononi mwao na kuzikitumia kufanikishia malengo yao.

Ingawa ofisa mwandamizi wa kodi kutoka TRA mkoani Kilimanjaro, Tilson Kabuje anasema mamlaka hiyo itachunguza kujua uhalali wa stempu zilizokamatwa, lakini ni vyema taasisi zingine za kiuchunguzi zikahusika katika kubaini ukweli wa suala hilo.

Kabuje anasema inapotokea mtu hajapewa stempu kwa taratibu zinazokubalika na wakamkuta nazo, hali hiyo huichukulia kwamba ni wizi kwa mujibu wa taratibu za TRA.

Tunajua kwamba stempu za TRA zinapobandikwa kwenye bidhaa zinakuwa na uzito wa aina yake kwa sababu zinatambulisha mambo kadhaa kuhusiana na bidhaa husika ikiwamo uhalali wa bidhaa na ubora wa bidhaa yenyewe.

Madhara ya stempu au stika hizo kuangukia mikononi mwa wahalifu ni makubwa. Hayapaswi kuangaliwa juu juu kwa sababu kuu mbili. Kwanza ni juu ya afya za watumiaji wa bidhaa husika kuwa shakani kwa sababu bidhaa zenyewe hazina viwango, lakini pili ni kutolipwa kwa kodi halali ya Serikali.

Inafahamika kwamba, stika hizo za TRA huwekwa katika bidhaa zinazolipiwa kodi na pia zilizothibitishwa na taasisi zingine za kiserikali kwa ajili ya kutumiwa na binadamu, sasa zinapoangukia mikononi mwa wahalifu ni tatizo, tena kubwa.

Ni vyema Serikali ikalichukulia suala hili kwa uzito wa aina yake na kufanya uchunguzi wa kina kwa sababu yumkini wanaojihusisha na utengenezaji huo wa pombe bandia watakuwa na watu ndani ya TRA wanaowasaidia kupata stempu hizo.

Pia, katika uchunguzi huo tunashauri Serikali iufanye kwa wazalishaji na wasafirishaji wa bidhaa zingine ikiwamo katika maeneo ya mipaka ya nchi yetu ili kujiridhisha juu ya matumizi ya stika au nembo ya TRA zinazokuwa kwenye bidhaa mbalimbali.