Uhai Cup itoe matokeo chanya

Monday June 11 2018

 

Michuano ya Kombe la Uhai inayodhaminiwa na Azamtv inatarajiwa kuanza Juni 9 na kumalizika Juni 23, 2018 mkoani Dodoma ambapo timu za vijana za timu 16 za VPL zenye umri wa chini ya miaka ishirini zitashiriki.

Tumeshuhudia uundwaji wa makundi manne yenye timu nne kila kundi. Uongozi wa Azam kwa ujumla wake unastahili pongezi kwa kuonyesha kwa vitendo kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu nchini. Tumeshuhudia udhamini katika VPL na CECAFA ngazi ya klabu na sasa kupitia bidhaa yake ya maji ya Uhai. Ni matarajio yangu kwamba timu husika ziliifahamu ratiba hii na hivyo wadau kupata burudani wanayoitarajia. Mambo ambayo ni vyema yakazingatiwa wakati wa mashindano hayo ni haya yafuatayo:

Makocha wahakikishe kwamba wachezaji vijeba hawashiriki

Ni kweli kwamba makocha wangependa timu zao zifanye vizuri na kuwa washindi wa michuano hiyo, lakini katika ile dhamira ya mchezo wa kiungwana, uungwana huo uanzie kwa makocha kuhakikisha kwamba wanawateua wachezaji wenye umri huo ili waweze kushiriki. Ikumbukwe kwamba kumchezesha mchezaji kijeba ni kuhujumu dhamira ya TFF, Azam na wadau wa mpira, ile ya kuwajengea uwezo wachezaji wetu wakiwa bado na umri mdogo na hivyo kuwa hazina kwa Taifa

Makocha wawafundishe vijana soka la ufundi na lenye nidhamu

Katika mashindano haya kwa kuzingatia kwamba hawa ni wachezaji wadogo, makocha na benchi la ufundi kwa ujumla wawafundishe vijana wao nidhamu nzuri ya kimchezo ndani na nje ya kiwanja.

Ninaamini kwamba timu yenye nidhamu ya aina hiyo itapata mafanikio kwa sababu ndiyo misingi ya timu yoyote kupata mafanikio.

Wachezaji wayachukulie mashindano hayo kama njia ya kwenda VPL.

Wachezaji wote watakaoziwakilisha timu zao wasiyachukulie mashindano hayo kama sehemu ya kujistarehesha bali wayachukulie kama ni sehemu ya kwenda ngazi ya VPL kwa aidha kujiunga na timu zao za wakubwa au kwa timu zilizoko VPL au zile ambazo zimepanda mwaka huu VPL kutafuta wachezaji wa kuimarisha timu zao. Uzoefu unaonyesha kwamba timu ya U-20 iliyoandaliwa vizuri inao uwezo wa kutoa wachezaji wazuri wa kucheza VPL.

Wasimamizi na viongozi wasiwe na matokeo kabla ya mchezo.

Wasimamizi wa michezo hiyo katika awamu hii ya mwisho (watawala na waamuzi) ni vyema wakahakikisha kwamba anayestahili kushinda anashinda na si kwa baadhi ya viongozi na waamuzi kuingia uwanjani na matokeo.

Hayo yakifanyika yatasababisha vurugu katika baadhi ya mechi au zote na hivyo kupoteza maana ya madhumuni hayo. Hili lismamiwe kwa umakini na yeyote atakayehusika na vitendo vya namna hiyo, aodolewe mara moja.

Timu ya Taifa ya U 23 inaweza kuchaguliwa kupitia mashindano hayo.

Mashindano haya yanaweza kutumiwa kwa TFF kuchagua wachezaji ambao watakuwa timu ya Taifa ya U 23 na hivyo kuufanya msingi wa uundwaji wa timu hiyo ambapo baadhi ya wachezaji watatokea timu ya Ngorongoro Heroes kwa sababu ni timu inayoundwa na wachezaji wenye umri chini ya miaka 20.

Makocha wa kuifanya kazi hiyo wapo na ni vyema TFF waitumie fursa hiyo. Tahadhari tu ni kwamba kwa sababu hapa tunazungumzia timu ya Taifa, watafutwe makocha ambao wadau hawatakuwa na mashaka na uwezo na uadilfu wao.

Nirudie tena kuupongeza uongozi wa Azam kwa mchango wao mkubwa katika kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu na nimatumaini yangu na wadau wengine kwamba kila mmoja atatoa ushirikiano.