Ulevi uliopindukia ni hatari kwa kongosho

Friday December 7 2018

 

By Dk Shita Samwel, Mwananchi

Kongosho ni moja tezi chirizi kubwa za ndani ya mwili ambayo ni muhimu kutokana kuwepo kwa seli ndani yake zinazokuhusika na utengenezwaji wa homoni muhimu mwilini ijulikanayo kama Insulini na Glucagon.

Vichochezi hivi ndivyo ambacho vinahusika na udhibiti wa kiwango cha sukari katika damu. Vile vile kongosho ndio inayotoa vimeng’enya mbalimbali kwa ajili ya usagaji wa vyakula.

Tezi hii ambayo iko chini pembeni mwa mfuko wa chakula ina umbile kama vile majani majani ya mwembe, inatazamana na kifuko cha nyongo.

Kongosho linaweza kupata shambulizi la kawaida na kuambatana na maumivu makali sana yasiyovumilika, lakini pia tatizo hili linaweza kuwa sugu hapo baadaye.

Tatizo hili linaweza kumpata mtu yoyote ambaye ana kongosho lenye afya. Kongosho linapoaathirika sana ufanisi wake unaweza kuathirika na kushindwa kutiririsha vichochezi na vimeng’enya.

Kutokea kwa shambulizi katika kongosho husababisha vimeng’enya vilivyomo ndani yake kutoka na hivyo kusababisha maumivu katika maeneo ya nje ya kongosho.

Mara nyingi chanzo kinachosababisha kutokea kwa shambaulizi katika kongosho ni pombe hasa wale wanywaji sugu wa pombe ambao wanaokunywa pombe kupita kiasi.

Uwepo wa mawe katika kifuko cha nyongo na kongosho vinaweza kusababisha kujitokeza kwa tatizo hili.

Wakati mwingine tatizo huwa ni madhara yatokanayo na uwepo wa maambukizi ya virusi, bakteria na parasite, sumu, vidonda vya tumbo, ajali ya maeneo ya tumboni na madhara ya dawa za matibabu.

Vilevile uwepo wa kinga ya mwili inayoshambulia mwili wake wenyewe ikiwamo kongosho, kuumwa na wadudu au wanyama wenye sumu ikiwamo nyoka na nge sumu yao inaweza kusababisha tatizo hili.

Ukubwa wa tatizo hili unaweza kuwa wa kati mpaka kuwa kali na inaweza hali hii kujidhibiti yenyewe bila matibabu. Endapo tatizo litakuwa kali huweza kusababisha kongosha kuharibika na kuvujisha damu.

Shambulizi la kongosho linaweza kuwa la muda tu na kuisha lenyewe pasipo hata matibabu na linaweza kuwa sugu na kuwepo kwa muda mrefu mwili na kuambatana na madhara makubwa.

Shambulizi sugu la kongosho huwapata zaidi wanywaji wa pombe ambao kwa kunywa kiasi kikubwa cha pombe pasipo kujua kuwa wanadhuru kongosho.

Tezi hii inapopata shambulizi mara kwa mara huweza kusisimua vimeng”enya vilivyomo ndani na kutoka nje ya kongosha na kuleta shambulizi katika tishu zilizopo jirani. Kwa kawaida vimeng’enya hivyo hutoka tu pale chakula kinapokuwepo katika mfuko wa chakula baada ya kutoka katika mfuko wa chakula.

Dalili na viashiria vya shambulizi la kawaida la kongosho ni pamoja na maumivu makali eneo la juu ya tumbo ambayo husambaa mpaka mgongoni, kuchefu chefu na kutapika, kupata homa, mapigo ya moyo kuwa ya kasi, tumbo kuvimba na kuuma linapotomaswa.

Endapo tatizo likiwa sugu huweza kuambatana pia na maumivu kama livyo kwa shambulizi la kawaida ila maumivu huendelea kuwepo na kusambaa mpaka mgongoni.

Maumivu ya tumbo huchochewa zaidi na ulaji wa vyakula vya mafuta kwa sababu vimeng’enya vya kongosho ndiyo vinavyohusika na usagaji wa vyakula hivyo.

Mgonjwa hupungua uzito wa mwili kutokana na kukosekana kwa vimeng’enya vya kusaga chakula hasa vyakula vya mafuta.

Baadaye mgonjwa anaweza kupata tatizo la kisukari endapo seli zinazotengeneza kichochezi cha Insulini kupata madhara, hali hii husababisha kiwango cha sukari katika damu kutodhibitiwa.

Mgonjwa anapofika kwa huduma za afya daktari atachukua historia na kumchunguza mgonjwa kimwili, baada ya hapo vipimo vya uchunguzi vinaweza kuchukuliwa na kufanyika.

Kipimo cha uchunguzi ni pamoja na kupima kiwango cha vimeng’enya viwili muhimu (lipase na Amylase), kiwango kikiwa juu ni moja ya ishara ya uwepo wa shambulizi la kongosho.

Vipimo vingine ni pamoja na kipimo cha kupima utendaji/ufanisi wa kongosho, kipimo cha sukari ya mwili (glucose tolerance test) ili kujua endapo kuna uharibifu wa seli zinazozalisha kichochezi cha insulini.

Vipimo vya picha ikiwamo xray maalum ya tumbo, picha za CT scan na MRI zinaweza kufanyika pia ili kujua ukubwa wa tatizo kiundani.

Uchukua wa sampuli ya tishu za kongosho kwa kutumia sindano maalum kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa tishu.

Katika hatua za mbeleni za ugonjwa daktari anaweza kuchukua sampuli za mkojo, damu na haja kubwa ili kuthibitisha bainisho (diagnosis).

Matibabu hutegemeana na bainisho, kama ni shambulizi la muda la kongosho matibabu huwa ni upewaji wa maji kwa njia ya mshipa na dawa za maumivu katika huduma za afya.

Tatizo hili linaweza kuwa kali na kusababisha athari kubwa hivyo kuhitaji mgonjwa kuweka katika uangalizi maalum (ICU), mgonjwa atauguzwa kwa ukaribu hii ni kutokana na shambulizi kali la kongosho linaweza kuleta madhara katika moyo, figo au mapafu.

Baadhi ya wagonjwa wanaweza kupata tatizo hili na kongosho kuharibika kabisa au tishu za kongosho kufa, upasuaji mkubwa wa dharura utahitajika ili kuondoa tishu zilizokufa au zilizopata uambukizi.

Kama chanzo cha shambulizi la kawaida ni uwepo vijiwe katika kifuko cha nyongo upasuaji unaweza kufanyika na mgonjwa akapona na kongosho kurudi katika utendaji wake kama hapo awali.

Kwa upande wa shambulizi sugu la kongosho matibabu huwa yana changamoto sana kutokana kutokea kwa madhara makubwa yanayojitokeza.

Mgonjwa atahitaji kupewa dawa za maumivu ili kupata utulivu na vile vile kuboresha mfumo wake wa chakula ili kuweza kukabiliana na hali ya ukosefu wa vimeng’enya.

Mgonjwa anaweza kupewa dawa zilizotengenezwa zenye vimeng’enya vya kongosho na pia sindano zenye kichochezi cha insulini ili kukabiliana na ukosefu wa vitu hivi muhimu.

Mgonjwa atahitajika kutumia mlo usio na mafuta kutokana na watu wenye tatizo hili wanakosa vimeng’enya vya lipase na amylase vinavyomeng’enya mafuta.

Kwa upande wa shambulizi sugu la kongosho upasuaji unaweza kufanyika ili kupunguza maumivu makali ya tumbo, kuboresha mifereji nayopita vichochezi na vimeng’enya.

Vile vile uzibuaji wa kifuko cha nyongo kama ndiyo ilikuwa chanzo cha tatizo na kupunguza kupata shambulizi la mara kwa mara.

Ili kujikinga na tatizo hili ni vizuri kujiepusha na unywaji pombe uliopitiliza, fika katika huduma za afya mapema utakapoona una dalili za shambulizi la kongosha.