Unajua faida ya kula komamanga?

Miongoni mwa matunda ambayo ni nadra sana kukutana nayo yakiuzwa mitaani ni komamanga.

Hili ni tunda lenye asili ya India na kisayansi linaitwa Punica Granatum.

Mtaalamu wa lishe kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Scholastica Mlinda anasema komamanga lina wingi wa vitamin C.

Tunda hilo lenye punjepunje zilizojikusanya kwa ndani, limejaa vitamin, madini na virutubisho vingi vinavyoweza kufanya mwili kuwa na afya na nguvu.

Komamanga husaidia mtiririko wa damu kwenda vizuri katika mishipa, hivyo kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na kiharusi.Ulaji wa mara kwa mara wa tunda hili huzuia meno kuoza na kuhuisha mfumo wa kinga mwilini kwa kuondoa vijidudu, bakteria, maambukizi ya virusi ndani ya mwili, husaidia kutibu maradhi ya tumbo ikiwamo kutopata choo.

Komamanga husaidia kuondoa sumu mwilini, hupambana na tatizo la uzito mwilini, husaidia kutibu magonjwa ya kusendeka (magonjwa ya muda mrefu), kama vile saratani ya tezi dume, saratani mbalimbali, kisukari, baridi yabisi na uvimbe katika maungo (gout).

Uchunguzi uliochapishwa katika jarada la utafiti la kuzuia saratani umeonyesha kwamba, kemikali ziitwazo ellegitannins zinazopatikana kwenye komamanga, zinazozuia kimeng’enyo aina ya aromatase.

Hicho ni kimeng’enyo ambacho hugeuza homoni ya androgen kuwa estrogen. Kushambuliwa kwa kimeng’enyo hicho ndiyo lengo kuu la kupambana na saratani za matiti.

Kiongozi aliyeongoza katika uchunguzi huo, Shiuan Chen anasema kemikali hizo hupunguza uzalishwaji wa estrogen, na kusaidia kuzuia seli za saratani ya matiti kuzaliana mwilini pamoja na tezi za ugonjwa huo kukua.

Uchunguzi huo umeonyesha kuwa katika komamanga kuna kemikali zinazozuia saratani ya matiti kusambaa mwilini.

Makala haya yameandikwa na mwandishi wa gazeti hili Hadija Jumanne.