Unapaswa kuzijua sheria, haki na wajibu wako

Muktasari:

  • Vijana wanapaswa kuijua, kuifahamu kwa sababu ndiyo kizazi kinachotegemewa kuhamasisha jamii au kushiriki moja kwa moja katika kudai haki.

Uwekezaji kwa tafsiri na lugha rahisi ni kuingiza fedha au kuweka kitu fulani kwa ajili ya kujipatia faida.

Unaweza kuwa ni uwekezaji wa muda mrefu au mfupi, jambo la muhimu ni kufikia malengo ambayo ni kupata faida, bila shaka faida kubwa.

Kila eneo, wananchi na jamii kwa ujumla ina taratibu zake za kuishi iwe kwa kufuata tamaduni za dini au kabila.

Namna hii ya maisha inajenga jamii bora na inayoishi kwa kuzingatia mfumo wa maisha iliyojiwekea, badala ya kujiendesha kama watu wasiokuwa na dira.

Ili jamii iwe na maendeleo inapaswa kuishi katika mifumo ya namna hiyo, isipofuata taratibu ilizojiwekea itakuwa ngumu hata kupata maendeleo.

Taratibu ilizojiwekea ndizo zitasimamia misingi ya utendaji katika nyanja zote, ikiwamo kuwalea vijana kwa kuifuata na kuhakikisha inarithiwa kizazi kwa kizazi kwa lengo la kuwa na mfumo imara unaotawalika. Misingi hiyo, taratibu hizo na mifumo ya maisha ya namna hiyo kitaalamu ndiyo inaitwa utawala wa sheria, ambao kila mmoja anapaswa kuufuata.

Kwa hivyo kutokana na maendeleo yaliyopo sasa kila jamii kubwa kustaarabika, jamii, miji, mikoa na hata nchi haiendeshwi kwa kufuata mifumo ya mila au dini, badala yake mfumo rasmi wa sheria.

Hivyo kila mwanajamii anapaswa kuzifuata sheria, hawezi kuzifuata kama hazijui, kwa hiyo jambo la msingi ni kujua haki zako zipo wapi, unalindwa vipi kisheria, ukifanya yapi unakuwa umezivunja.

Kama ambavyo ibara ya 12 hadi ibara ya 29 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, ambayo imefanyiwa marekebisho mara kadhaa inaelezea haki na wajibu wa kila mwananchi.

Vijana wanapaswa kuijua, kuifahamu kwa sababu ndiyo kizazi kinachotegemewa kuhamasisha jamii au kushiriki moja kwa moja katika kudai haki.

Kujua sheria ni jambo muhimu kwa sababu kuna watu wamekuwa wakifanya mambo kiholela, lakini ukiwasikiliza unabaini hawakuwa wakijua wanatakiwa na hawatakiwi kufanya nini.

Inajulikana na unapaswa kujua kama kijana kuwa kutojua sheria si utetezi wa jambo lolote unalolifanya kinyume nayo.

Kuna ibara kwenye katiba ya nchi zinakuruhusu na kukubana kwa wakati mmoja, hivyo usipozijua sheria na haki zako utajichanganya. Miongoni mwa ibara hizo ni ya 18 ya Katiba ya nchi inayotoa uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.

Kwa upande mwingine ibara ya 30 ya katiba ya nchi imeweka mipaka na namna ya kuutumia uhuru huo bila kubughudhi au kuingilia uhuru wa watu wengine.

Sasa ukiyajua yote haya utaishi katika mipaka yako na kuendana nayo huku ukidai haki zako, lakini wakati huo huo ukikumbuka kuwa hakuna haki isiyo na mipaka.

Kila mara kumekuwa na kukumbushana kusoma Katiba ya nchi na sheria, miongoni mwa faida za kusoma ni pamoja na kuzitambua na kuziishi sheria za nchi.

Kama ilivyo ada anayesoma ndiye anayepata maarifa, hivyo basi kama unapenda kusoma mbali ya vitabu vya hadithi au mafunzo mengine jitahidi upate nafasi ya kusoma sheria pia.

Huwezi kujiamini kubishana kwa jambo lolote hata la haki yako kama hujui sheria, inawezekana ukawa unadai haki yako kwa mtutu wa bunduki jambo ambalo litakutia hatiani.

Lakini ukizijua sheria hautatumia nguvu kudai haki yako, wala hutapata shida kujitetea na kuwatetea wengine, kwa sababu utakuwa unafahamu unatakiwa kufanya nini, kusema nini na maamuzi ya hayo uyasemayo ni yapi.

Utafahamu namna ya kudai haki yako unayoona inataka kupokwa na waliopo katika mamlaka za kisheria, Serikali au mtu binafsi, tofauti na hapo utakuwa ni mtu wa kuitikia hata yale unayopaswa kuyapinga.

Ukiijua sheria pia utakuwa na nafasi nzuri ya kutetea haki na maslahi ya taifa kwa kuzilinda na kujenga hoja unapoona zinatumika ndivyo sivyo.

Mwongozo huo umetolewa kwenye Ibara ya 27 ya katiba ya nchi ya mwaka 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kadhaa, ambapo imebainishwa wazi kuwa kila mwananchi ana haki ya kulinda na kutunza mali za umma na kuheshimu za mtu mwingine.

Utajuaje haya yote kama husomi au hauna utaratibu wa kujifunza sheria, ukijifunza utafahamu mengi zaidi ya haya na utajikuta kumbe kwa kipindi kirefu umekuwa ukijinyima haki zako za msingi kwa kutoijua.

Hili la kujua sheria linakupa wajibu gani wa kulinda mali za umma linapaswa litiliwe mkazo na vijana wengi ambao wanategemewa kuamsha mijadala ya namna hiyo hususani hapa nchini ambapo kuna rasilimali nyingi zinazohitaji jicho la tatu kuzilinda. Nasisitiza jifunze sheria ikulinde katika mambo mengi, usisubiri kukumbushwa kwa nguvu.

Kibaya zaidi utakumbushwa kwa nguvu pale tu, utakapokuwa umeikiuka na umeingia hatiani, kwa sababu huijui haitakuwa sababu ya kuchukuliwa hatua, lakini utapata wakati mgumu kujitetea.

Narudia tena, kijana soma sheria, ijue, ifanyie kazi, itumie kujitetea, kutetea wengine, kulinda nchi yako dhidi ya wadhalimu wanaotumia vibaya rasilimali zilizopo.