Unaweza kujiendeleza kitaaluma ukiwa kazini

Friday October 7 2016

Kuajiriwa hakumaanishi mwisho wa safari ya

Kuajiriwa hakumaanishi mwisho wa safari ya kujiendeleza kielimu. Picha na mtandao wa africanprisons.org 

By Frank Victor Mwananchi

Baadhi ya waajiri, wanapendelea wafanyakazi ambao wana mipango ya kujiendeleza, kwani hatua hiyo inaonyesha ukomavu na dhamira ya kufanikiwa katika taaluma uliyopo.

Kujiendeleza ni sawa na kuulisha ubongo wako taarifa mpya ambazo zitakusaidia na kuisaidia kampuni au taasisi unayofanyia kazi, katika kutatua changamoto zake na kuleta matokeo mazuri ya uzalishaji.

Kupanda daraja na mshahara

Kwenye sekta rasmi ambazo mshahara wako utategemea daraja ulilopo kazini, ili ufike hapo inategemea kwa kiasi kikubwa kiwango cha elimu ulichonacho

Mathalani kama unafanya kazi ya uhasibu, ukiwa na shahada ya kwanza, fahamu kuwa utatambuliwa kama mhasibu msaidizi na hilo ndilo daraja lako.

Ikiwa unataka kubadili daraja, hauna budi kujiunga na  mafunzo maalumu ili uwe mhasibu kamili. Na bila shaka yoyote baada ya kupata cheti cha uhasibu, daraja lako litabadilika na kipato kitapaa.

Kubadili ajira

Elimu zaidi na  au vyeti vya kitaaluma ni muhimu wakatiwa  kufanya mabadiliko ya ajira hasa kwa sekta ambazo maarifa maalumu ya ziada yanahitajika  kama vile uhandisi na teknolojia.

Inawezekana umechoshwa na kufanya kazi aina moja kila siku, na unataka kutafuta changamoto mpya na mtindo mpya wa kutatua changamoto.

Ili kufikia lengo hili, hauna budi kujiongezea kiwango cha elimu kitakachokuwezesha kupata ajira mpya kwa urahisi.

Utajiendelezaje?

Katika dunia ya sasa ya ushindani wa ajira baadhi ya watu kwa kuhofia kukosa ajira, wanajikuta katika wakati mgumu kuacha ajira na kurudi shuleni.

Ikumbukwe kuwa mipango ya kujiendeleza kielimu inahitaji uhuru  wa kimahitaji na kujitoa katika muda. Kwa mfano, masomo ya shahada, yanaweza  kukuchukua miaka mitatu hadi minne mpaka unahitimu.

Wakati utakapoona kuna manufaa ya kujiunga na masomo ya juu, bado utatakiwa  kufikiria jinsi utakavyokuwa unafadhili elimu yako.  Mbali na ada ya masomo, unatakiwa pia ufikirie namna utakavyokuwa unajihudumia kwa mahitaji yako mengine ya msingi.

Ukichelea kukosa ajira yako, unaweza kuchagua kozi ya kusomea ya muda mfupi, huku ukiendelea na ajira.

Ikiwa mpango wako ni kusoma nje ya nchi, tafuta maelezo kuhusu vikwazo vinavyoweza kukukumba kama vile  lugha, mahitaji ya viza na malazi.

Shukrani kwa intaneti, kuna vyanzo vingi vya habari ambavyo vinaweza kukusaidia katika maamuzi yako na mchakato wa maandalizi.

Hivyo, kuanza mipango yako na utafiti mapema mwaka mmoja kabla ya kozi yako ni jambo la msingi ili uweze kufanya uchaguzi bora.

Maandalizi ya akili

Usiidharau changamoto ya kushiriki katika masomo wakati umeshapumzika muda mrefu na pia upo katika majukumu na umri umeshaenda.

Ni uamuzi mkubwa kurudi tena kushika vitabu na inahitaji nidhamu, muda na kujitoa kifedha.

Mara baada ya masomo kuanza, utagundua kuwa namna yako ya kujifunza na uwezo haviko  sawa kama ulivyokuwa miaka ya 20 iliyopita..