UCHAMBUZI: Unawezaje kutumia choo ukakiacha kichafu?

Kama umewahi kutumia vyoo vya umma utakuwa si mgeni wa uchafu uliokithiri katika maeneo hayo licha ya kuwapo kwa utaratibu wa kila anayeingia kulipia ili kupata huduma.

Harufu kali na mbaya inayozalishwa na uchafu huwa imetanda katika vyoo hivyo, ingawa wapo baadhi ya wanaovisafisha lakini mandhari yake hayana mvuto.

Inawezekana wateja wanapoingia na kukuta uchafu, lawama zao zinaangukia kwa wanaofanya usafi kwenye maeneo hayo, lakini uchambuzi huu utawaangazia watumiaji wa vyoo hivyo.

Kiuhalisia anayetoa Sh200 mlangoni kulingana na taratibu za matumizi ya vyoo vya umma, hategemei kukutana na uchafu ndani na lazima akereke anapokuta mtu mwingine ametumia na kuacha uchafu.

Japokuwa watu wamezoea kukuta hali ya vyoo vichafu maeneo ambayo wanatumia watoto kama shuleni, ndiyo maana inashangaza hali hiyo kuwapo katika maeneo ambayo ni nadra kufika watoto.

Ukiingia katika vituo vya mabasi, masoko, kanisani, maeneo mbalimbali ya starehe kama baa hali ya vyoo vinavyotumika ni mbaya kutokana na uchafu uliokithiti hadi inaibua maswali.

Ninapoona maeneo hayo muhimu yakiwa machafu huku wateja wake wakiwa watu wazima, inanipa msukumo wa kuhoji watumiaji kuwa nini kinawashawishi kutumia choo na kukiacha kichafu?

Inawezekana ni ile fikra kwamba wapo watu wanaofanya usafi kwenye maeneo hayo, hivyo inawapa wateja ujasiri wa kuacha pakiwa pachafu baada ya kutumia.

Pengine wateja wamejijengea mazoea kutokana na kulipa Sh200 wanapoingia mlangoni, basi inawaruhusu kuacha choo kikiwa kichafu.

Ninapojaribu kuangazia kero hii, inazidi kunipa taswira ya watumiaji wa vyoo hivyo kuwa wanafanya makusudi.

Nasema hivyo kwa sababu siwezi kushawishika kuwa wanayoyafanya kwenye maeneo hayo yanafanana na wanayafanya kwenye vyoo vyao nyumbani.

Hii inaweza kudhihirisha hulka ya ubinafsi inayodhoofisha dhana ya uungwana, watumiaji hao wanapotumia hawafikirii kama kuna wengine watahitaji kutumia, nikiamini kuwa anayewajali wengine hawezi kutumia akakiacha choo kichafu.

Kama watumiaji wa vyoo hivi, tunahitaji kupata ufumbuzi wa changamoto hii ambayo inatokana na watumiaje wenyewe.

Binafsi, ninakuwa mzito kuamini kuwa huenda wanajisahau baada ya kumaliza shughuli zao, nikiamini kuwa kukosa ustaarabu ndiko kunasababisha kuacha sehemu hiyo muhimu ikiwa chafu.

Mathalani, kwenye vituo vya mabasi wengi wanaweza kuwa na mawazo kuwa hata wakichafua hawafahamiki lakini hii haiwezi kuwa ngao ya kupoteza ustaarabu kwa kuwa ustaarabu haujali kufahamika au kutofahamika.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kama mazingira ya choo siyo safi na salama, uwezekano wa kukumbwa na magonjwa ya milipuko ni mkubwa ikiwa ni pamoja na kipindupindu, kuhara, homa ya tumbo na maambukizi katika njia ya mkojo (UTI).

Pamoja na kampeni mbalimbali za kuhamasisha matumizi ya vyoo bora, haziwezi kufanikiwa kama jamii endapo haitabadili mitazamo na kuhamasika kwa kutambua umuhimu wa kutunza mazingira ya vyooni.

Usafi wa vyoo katika maeneo ya umma ni jukumu la kila mtu na linahitaji liangaliwe kwa umakini ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza hasa magonjwa yanayotokana na uchafu. Ikumbukwe kwamba athari zake hazichagui aliyeacha uchafu, kukiibuka magonjwa ya mlipuko huathiri jamii nzima hivyo kila mmoja awe mhamasishaji katika usafi wa vyoo hususani vya umma.

Ninaamini kuwa, changamoto hii ya uchafu wa vyoo vya umma inaweza kuisha pale jamii itakapobadilisha mtazamo wa kuamini kuwa wenye jukumu la kutunza mazingira hayo ni watu maalumu walioajiriwa kufanya usafi.

Hata hivyo, wanaohusika kusafisha vyoo hivyo wasibweteka kwa kuwa lawama zitawaendea pale wateja wanapokuta vyoo haviko katika hali ya usafi.

Emmanuel Mtengwa ni mwandishi wa Mwananchi, anapatikana kwa simu namba; 0753590823