Unayajua maharagwe lishe? Hizi ndizo faida zake

Licha ya maharagwe aina tofauti kuwa miongoni mwa mboga zenye faida mwilini, wataalamu wa masuala ya afya wanasema maharagwe lishe, ndiyo mazuri zaidi.

Mbali na kutumika kama mlo wa binadamu, majani yake hutumika pia kama chakula kwa binadamu na mifugo.

Nyuzi lishe zilizomo wenye maharagwe hayo husaidia mwili kumeng’enya chakula vizuri.

Mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe, Wessy Meghji anasema maharage lishe ni yameongezwa madini ya chuma na zinki kwa wingi kwa ili kufanya yawe na manufaa bora mwilini.

Meghji anasema maharagwe hayo hayana tofauti na maharagwe mengine katika kulima na hata katika kupika.

Hata hivyo, uanzishwaji wake ni moja ya mkakati wa kupunguza tatizo la upungufu wa madini ya chuma ambayo husaidia kutengeneza chembechembe nyekundu za damu.

Chembechembe hizo husaidia kuondoa tatizo la upungufu wa damu mwilini ambao huwapata zaidi wajawazito na watoto wadogo chini ya miaka mitano.

“Madini ya zinki yalipo katika maharagwe lishe husaidia ukuaji wa watoto na kinga dhidi ya magonjwa, kwa sababu hapa nchini kuna aina tatu za maharagwe ambazo tayari zimeshafanyiwa utafiti na kupitishwa,” anasema Meghji na kuzitaja aina hizo ambazo ni Jesca, Seliani 14 na Seliani 15.

Anasisitiza wananchi watumie maharagwe lishe ili wapate manufaa ya ukuaji wa afya ya mwili na akili.

Hata hivyo, maharagwe yana kiwango kikubwa cha protini ambayo ni muhimu katika kujenga mwili wa binadamu. Kwa msingi huo yanafaa kuwa mbadala wa nyama, maziwa, mayai au samaki. Vilevile husaidia kukinga kiwango cha sukari kwenye damu kuongezeka ghafla baada ya mlo, hivyo ni muhimu kwa watu wenye kisukari au wanaoelekea kupata tatizo hilo.

Virutubisho vilivyomo katika maharagwe vinamwezesha mlaji kukabiliana na maradhi yanayotokana na upungufu wa protini au madini ya chuma na zinki.

Makala haya yameandikwa na mwandishi wa gazeti hili, Hadija Jumanne.