UpandikIzaji mbegu; matumaini ya uzazi kwa wanawake

Ni kawaida wanawake waliopo kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka mitatu kunyooshewa ‘vidole’ endapo watakuwa hawajabahatika kupata mtoto.

Hakuna mwanamke anayependa hali hiyo, bali hutokea kutokana na tatizo la uzazi kwake au kwa mwenza wake.

Wengi hudhani ni wanawake pekee ndiyo wenye tatizo hilo ilhali wanaume pia huwa chanzo cha kushindwa kumpa mwanamke ujauzito.

Pamoja na changamoto hiyo kuwa katika pande mbili, wanawake ndiyo wamekuwa wakihangaika huku na kule kutafuta njia zitakazowawezesha kupata ujauzito.

Endapo ‘utatembelea’ mitandao ya kijamii, utaona biashara ya uuzaji dawa za wanawake kushika ujauzito ikiwa imeshika kasi.

Mbobezi wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk Clementina Kairuki anakiri kuwapo kwa tatizo la uzazi kwa wanawake na wanaume.

Anasema siku zinavyozidi kwenda ndiyo idadi ya wenye matatizo inaongezeka.

“Asilimia 30 ya wanawake wanaokuja kliniki wana matatizo ya uzazi na hawa tiba zao zinatokana na jinsi walivyoathirika; wapo wanaohitaji dawa, wengine mirija imeziba inahitaji kuzibuliwa kwa upasuaji mdogo au mkubwa na akashika mimba halafu wapo pia ambao mirija yao imeharibika kabisa na hawezi kushika ujauzito njia pekee inakuwa upandikizaji,” anasema mbombezi huyo.

Pia, anasema mitindo ya maisha imekuwa chanzo cha tatizo la uzazi au matumizi ya dawa bila maelekezo ya wataalamu.

“Wanawake wengi wanatokwa na uchafu ukeni lakini wenyewe wanaona ni suala kawaida, ukweli ni kwamba hili ni tatizo linalotakiwa kushughulikiwa kitaalamu, likiachwa na kuwa sugu ndiyo chanzo cha kuziba mirija,” anasema Dk Kairuki.

“Mirija inapoziba, lazima izibuliwe ndiyo mwanamke ashike ujauzito na ikiwa imeharibika kabisa ugumu wa tatizo unaongezeka maradufu hivyo kuhitajika utaaalamu wa hali ya juu kutibu.”

Sababu nyingine ni kuota kwa vivimbe kwenye mirija (fibrods), kutowiana kwa homoni na kwa upande wa wanaume hilo hutokea zaidi ubora wa mbegu unapoathiriwa.

Dk Kairuki anasema miaka ya karibuni kumekuwapo na ongezeko kubwa la wanawake wenye matatizo ya uzazi yaliyogawanyika katika makundi mbalimbali yakiwamo yanayohitaji upandikizaji wa mbegu za kiume (IVF) kuyatibu.

“Kati ya wanawake 20 wenye matatizo ya uzazi wanaokuja hospitalini kwetu, asiliamia sita hadi saba wanahitaji kufanyiwa njia hiyo ya kisasa ya upandikizaji ili kufanikiwa kushika ujauzito,”anasema Dk Kairuki

IVF ni teknolojia ya kisasa ya upandikizaji wa mbegu za kiume kwenye mji wa uzazi kimaabara inayotumika kutatua tatizo la ugumba kwa wenza wawili.

Anaeleza kuwa upandikizaji hufanyika pale mbegu za kiume na yai la mwanamke vinavyokutanishwa pamoja nje ya mfuko wa uzazi kisha kiinitete kinachopatikana kinawekwa ndani katika mji wa mimba siku tatu hadi tano baada ya kuunganishwa.

“Inachukua siku kadhaa kubaini kama zoezi (tiba) limefanikiwa au la. Njia hii ni salama na inakubalika kutumika duniani kote endapo tu kuna mtaalamu mwenye ujuzi wa upandikizaji na upatikanaji wa vifaa vya kufanyia.

Nani anastahili kupandikizwa?

“Nafasi ya kufanikiwa kupandikizwa inategemeana na mambo mbalimbali ikiwamo umri wa mpandikizwaji, chanzo kilichosababisha ugumba, iwapo yai lililopandikizwa lilikuwa la mtu aliyejitolea au hapana, mafanikio ya matibabu ya awali na uwezo wakitaalamu wa mfanyaji,” anasema Kairuki.

Kwa mujibu wa tovuti ya American pregnancy wanawake wenye umri chini ya miaka 35 uhakika wa kufanikiwa ni kati ya asilimia 41 na 43.

Wenye umri kati ya miaka 35 na 37 uhakika wa kupata ujauzito kwa njia hiyo ni kati ya asilimia 33 na 36 huku wenye miaka kati ya 38 na 40 nafasi yao ni kati ya asilimia 23 hadi 27. Wanawake wenye miaka zaidi ya 40 wao uhakika wa kufanikiwa ni mdogo zaidi kati ya asilimia 13 hadi 18.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, aina hii ya upandikizaji inawahusu wanawake ambao mirija yao imeziba na kuathirika na haiwezi kuzibuliwa au kukatwa.

Pia, wanawake wenye uvimbe kwenye ovari na vimeleo vya uvimbe kuzunguka mfuko wa uzazi ni ngumu kushika mimba kwa njia ya kawaida hivyo ili kupata mtoto ni lazima afanyiwe matibabu haya.

Pia, wanawake waliotolewa mfuko wa uzazi lakini ovari zao zimebaki au wale ambao wamemaliza hedhi na wanahitaji mchango wa mayai, nao wanapandikizwa.

Dk Kairuki anasema Hospitali ya Kairuki imeona kuna haja ya kuanzisha kituo maalumu kwa ajili ya kumsaidia mwanamke kupata ujauzito kwa njia ya upandikizaji wa mbegu.

Anasema kituo hicho kilichopo Bunju kitaanza kufanya kazi Julai, kitakuwa cha pili kwa Dar es Salaam na cha tatu kwa Tanzania nzima kikiwa na lengo la kutatua changamoto ya uzazi kwa wanawake ambao hawawezi kupata ujauzito kwa njia ya kawaida.

“Tumeona changamoto hiyo ni muhimu kuifanyia kazi ili kuwapatia matibabu wenye matatizo ya aina hii ambao wapo wengi ingawa sina takwimu kwa namba,”anasema Dk Kairuki.

Wananchi wanasemaje?

Mmoja wa waathirika wa tatizo hilo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Koku, anasema tiba hiyo ni mkombozi kwa wanawake na wanaume wanasombuliwa na tatizo la uzazi.

“Nimeolewa zaidi ya miaka mitano iliyopita; nilikwenda hospitali kupata tiba nikaambiwa sina tatizo, lakini ujauzito sipati. Mume wangu anao watoto aliozaa na mwanamke mwingine. Nafikiri kilichobaki ni kuangalia namna ya kupandikizwa mbegu ili nipate ujauzito,” anasema Koku.

Mkazi mwingine, Mabrouk Othman anasema bado hajaingia kwenye ndoa, ila kuwapo kwa huduma hiyo ni faida kwa wenye tatizo la uzazi.

“Ni nadra mume na mke wote mkawa na tatizo la uzazi, kama mwanamke ana shida atapandikizwa mbegu za mume wake na watapata watoto,” anasema Othman.